WINGA wa Coastal Union, James Msuva amesema bado anahitaji muda kuzoea mazingira ya timu mpya akieleza kuwa kujiunga na kikosi hicho katikati ya msimu kimempa shida kidogo.
James alijiunga na Wana Mangushi kufuatia kuachana na KenGold mwishoni mwa msimu uliopita na baadae kutambulishwa Coastal kipindi cha dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Januari 1, 2026 na kufungwa Januari 30, 2026.
Msuva amesema kwa mchezaji aliyesajiliwa dirisha dogo mara nyingi huwa sio rahisi kuingia moja kwa moja na kuonyesha kiwango bora kutokana na kukuta timu tayari ipo kwenye ushindani mkali wa ligi.
Amesema hadi sasa hajaanza vizuri kama alivyotarajia, lakini anaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na mfumo wa timu pamoja na wachezaji wenzake.
“Sijaanza vizuri, kwanza kwa sababu nimeingia dirisha dogo ambalo kwa wachezaji inakuwa ngumu kufanya vizuri, pia nimekutana na changamoto ya ushindani kwenye eneo la ushambuliaji,” amesema Msuva na kuongeza.
“Coastal ina wachezaji wazuri mbele, hivyo napaswa kufanya jitihada ili kuhakikisha naisaidia timu na kwangu binafsi.”
Pamoja na ushindani huo, Msuva amelipongeza benchi la ufundi kuwapa nafasi wachezaji wote ili kuonyesha uwezo uwanjani.
Tangu ajiunge na Coastal Union, mshambuliaji huyo tayari amecheza mechi tatu, huku mbili zikiwa za Ligi Kuu Bara na moja ya FA.