MCHEZAJI kinda wa Kitanzania, Barka Seif, ameula katika kikosi bora cha vijana wenye umri chini ya miaka 12 kilichochaguliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Catalonia (FCF).
Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji wenye vipaji kutoka klabu mbalimbali ndani ya Catalonia kama vile Barcelona, Espanyol RCD, Girona na Damm.
Barka amechaguluwa katika kikosi hicho kufuatia kufunga mabao 18 katika mechi 20 za ligi ya vijana inayoendelea nchini humo akiwa na Damm FC.
Hivyo ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kuwa sehemu ya kikosi hicho sambamba na makinda mengine kutoka katika klabu kubwa nchini humo kama Barcelona.
Orodha ya wachezaji hao ni pamoja na Teo Rodríguez Lozano, Mauro Artigot Garcia, Arnau Casas Sanchez, Destiny Kosis Ejiofor John na Marc Ribera Martínez kutoka Barcelona.
Iker Pena Langa na Barka kutoka Damm FC, Hugo Garcia Cabello, Jan Treserra Bermúdez na Marti Parraga Vivas wanaocheza Espanyol RCD.
Ahmed Taibi El Ghardouf kutoka FIF Lleida CE, Mariano González Sánchez wa Fundació P. F. Base Reus, Roc Blanquet Cañet na Hiro Rabanal Juan kutoka Girona na Kajetan Pawel Goral wa Mercantil CE.
Kikosi hicho kinatarajiwa kuingia kambini siku chache zijazo kwa ajili ya mashindano mengine ya vijana ikiwa ni mpango maalum wa Catalonia katika kuinua na kuendeleza vipaji.