BAADA ya kuanza na pointi moja dhidi ya Azam FC, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Shadrack Nsajigwa amesema hesabu zinahamia kwa Yanga kabla ya mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TMA inayocheza Championship.
Nsajigwa aliyejiunga na maafande hao hivi karibuni kurithi mikoba ya Zedekiah Otieno, juzi aliiongoza timu hiyo ilitoshana nguvu dhidi ya Azam kwa suluhu.
Wajelajela hao wanatarajiwa kushuka tena uwanjani Machi 8 kuwakaribisha TMA katika mchezo wa Kombe la Shirikisho, hatua ya 32 bora, mechi ikipigwa wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Baada ya mchezo huo, maafande hao watarejea uwanjani kuwakaribisha Yanga ukiwa ni mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu utakaopigwa Machi 12 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakihitaji ushindi kujinasua nafasi za mkiani waliko na pointi 13.
Nsajigwa amesema wakati wakijiandaa na mchezo dhidi ya TMA, wanafahamu ugumu wa Yanga, hivyo wanakenda kujipanga ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kujiweka pazuri kwenye msimamo.
Amesema matokeo waliyonayo siyo mazuri sana na kwamba, kila mchezo kwao ni vita ya pointi kuhakikisha wanakuwa salama mwisho wa ligi, akiomba sapoti ya mashabiki wa timu hiyo.
“Tunaanza na Yanga wakati tukiisubiri TMA. Ni mchezo mgumu kwa kuwa ni timu kubwa yenye wachezaji wazuri. Nadhani nitaielezea zaidi huko mbele. Tunaenda mechi kwa mechi,” amesema kocha huyo.
Kwa upande wake beki wa timu hiyo, Dotto Shaban amesema pointi moja waliyoipata dhidi ya Azam imewaongezea nguvu kupambana kwa mechi zijazo ili kujiweka sehemu nzuri.
Amesema matokeo hayo ni salamu kwa timu zinazofuata na kwamba, yeyote wanayekutana naye asitarajie mteremko kwani hawatakuwa wanyonge.
“Tumepata nguvu mpya na hii ni salamu kwa timu zinazofuata. Tunaomba zaidi ushirikiano wa mashabiki na tutapambana kubaki salama,” amesema nyota huyo.
Katika mechi kati ya Azam na Tanzania Prisons kipindi cha kwanza timu zote zilicheza kwa tahadhari na mashambulizi ya kushtukiza hadi mapumziko.
Hata hivyo, Azam wataendelea kujilaumu zaidi kufuatia nafasi za mipira ya kutenga kutozitumia vyema baada ya mashuti yote kutokuwa na madhara langoni mwa Prisons.
Kipindi cha pili Azam ilionekana kutawala mchezo kwa mashambulizi ya mara kwa mara, huku Prisons ikiwa na jukumu la kuokoa zaidi hatari hasa kipa wake Mussa Mbisa aliyesimama imara golini.
Katika dakika ya 77, Prisons ililifanya mabadiliko ya kiufundi kwa kumpumzisha Lambart Sabiyanka aliyempisha Samson Mbangula na Never Kagoma akichukua nafasi ya George Mpole.
Mabadiliko hayo yaliwapa nguvu maafande hao hasa eneo la ushambuliaji ambapo Mbangula aliwapa wakati mgumu mabeki wa Azam kwa kosakosa dhidi ya kipa Aisha Manula ikiwamo ya dakika 90 alipoupisha mpira uliomkuta Never aliyeachia shuti kali ambalo lilipanguliwa vyema na ‘Tanzania One’.
Nayo Azam ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Zidane Seleli na nafasi yake kujazwa na Albogast Kyobya huku James Akaminko akimpisha Sadio Kanoute na licha ya kubadilisha wachezaji matokeo yalibaki vilevile