Moshi. Pacha Enjolight na Heavenlight Mafuwe (33), wakazi wa Kijiji cha Uduru, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, wameondoa dhana kwamba kazi ngumu, hususan zinazohitaji msuli na ustahimilivu ni za wanaume pekee.
Kazi yao ya upagazi katika Mlima Kilimanjaro imeonyesha wazi kuwa uthubutu, bidii na uthabiti huchaguliwa bila kujali jinsia. Mafanikio yao ni matokeo ya juhudi zao za kweli na uthabiti badala ya maneno.
Kwa zaidi ya miaka mitano sasa, pacha hao walifanya kazi ya upagazi, wakibeba mizigo ya watalii waliokuwa wakipanda mlima huo maarufu na mrefu Zzaidi barani Afrika.
Hata hivyo, leo hii si wabeba mizigo tena, bali ni waongoza watalii, hatua inayodhihirisha kwamba mafanikio si zao la jinsi bali ni matokeo ya bidii, uthubutu, na uamuzi sahihi.
Wakizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika mjini Moshi, pacha hao wanasema maisha yao yalianzia katika mazingira ya kawaida kijijini, ambako walikua wakijifunza mapema thamani ya kuwajibika.
Baada ya kufiwa na mama yao wakiwa wadogo, walibeba jukumu la kusaidia familia yao kama watoto wa kwanza.
Enjoylight, anasema kwamba tangu utotoni walijifunza kushirikiana na kusaidiana, wakitambua kuwa mafanikio yao binafsi yangekuwa nguzo kwa wadogo zao.
Anasema walihitimu kidato cha nne mwaka 2010 katika Shule ya Sekondari Uduru, iliyopo Machame mkoani Kilimanjaro na hapo ndipo swali la “wataishi vipi?” lilipoanza kuwagonga vichwa.
“Tulijiuliza ndiyo tumeshamaliza shule, sasa tunafanya nini baada ya hapa?’” anasimulia pacha huyo na kuongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa mwanzo mpya wa safari yao ya kusaka maisha ya furaha na amani.
Anasema baada ya kuhitimu shule, walijiunga na mafunzo ya hoteli katika chuo cha Intel kilichopo mjini Moshi na huko walijifunza misingi ya mapokezi, huduma kwa wageni na taaluma ya utalii kwa ujumla.
Anasema mafunzo hayo hayakuwa tu nyongeza ya elimu aliyoipata aliposoma sekondari, bali yalikuwa daraja la kumfungulia upeo mpana wa sekta ya utalii, inayochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa.
Ndani ya mwaka huohuo, anasema walipata fursa ya kujiunga na kazi ya kupanda Mlima Kilimanjaro kama wabeba mizigo. Anasema wazo hilo halikuwajia ghafla, bali ilikuwa ndoto yao tangu awali kwamba siku moja watafanya kazi hiyo.
“Tulipowaona wasichana wenzetu wakifanya kazi hiyo kwa ujasiri mkubwa, tuliendelea kuhamasika, huku tukijipa moyo na kujipiga vifua, acha tujaribu,” anasimulia Enjoylight.
Hivyo, anasema kuanzia mwaka 2013 hadi 2018 walifanya kazi ya kubeba mizigo, hiyo ilikuwa miaka mitano ya kujifunza, kuvumilia na kukua kimawazo, kiuchumi, na kijamii.
Kazi ngumu inayohitaji moyo mkuu
“Upagazi mlimani si kazi nyepesi. Ni kazi inayohitaji nguvu za mwili, ustahimilivu wa baridi kali, upepo mkali na hewa nyepesi kadri unavyokaribia kilele. Ni kazi inayomjaribu mtu si kimwili tu, bali pia kiakili,” anasema Enjoylight.
Anasema walipambana si kwa sababu tu walihitaji kipato, bali kwa walitambua wajibu wao kwa familia yao. Walikuwa tegemeo la wadogo zao. Kila safari ya mlima ilikuwa zaidi ya kazi, ilikuwa ni ahadi ya kesho iliyo bora.
Anasema anakumbuka namna alivyoifika kilele cha Uhuru kwa mara ya kwanza, kilivyompa imani mpya.
“Si tu kwamba nilikuwa nimepanda mlima mrefu zaidi Afrika, bali nilivuka mipaka ya hofu na dhana potofu za watu, hasa wanaume wa Kichaga. Kilele hicho kilikuwa ishara kwangu kwamba changamoto yoyote maishani naweza kuishinda kwa ujasiri na kujiamini,” anasema.
Kwa mtazamo wao, wanasema ufanyaji kazi hiyo ngumu mlimani umewasaidia kutuma ujumbe kwa jamii kwamba mwanamke anaweza kubeba mzigo mgongoni mwake na pia kubeba matumaini ya familia yake mabegani mwake.
Enjoylight anasema mwaka 2015 waliamua kujiendeleza zaidi kwa kusoma menejimenti ya hoteli. Uamuzi huo unaonyesha hawakuona kazi ya upagazi kama mwisho, bali kama hatua ya mpito.
Mwaka 2016, Enjoylight alipata nafasi ya kufanya kazi katika Hoteli ya Serengeti Safari Lodge iliyopo mkoani Mara. Anasema huko alipata uzoefu Zaidi uliochochea ndoto yake ya kuwa mtoa huduma kwa wageni na kumwezesha kuelewa mahitaji ya watalii, maarifa yaliyokuwa muhimu kwa waongoza watalii.
Anasema kwa ujumla, safari yao iliwaongoza kwenye mnyororo wa fursa zaidi, ikiwamo kupata elimu ya utalii iliyozaa kazi, uzoefu na cheo kipya.
“Hakukuwa na hatua iliyopotea katika mnyororo, tulichokuwa tunakihitaji ni kuboresha kazi yetu,” anasema Enjoylight.
Akizungumzia manufaa, Heavenlight anasema kupitia kazi ya mlimani wamejiingizia kipato kilichobadilisha maisha yao na ya familia kwa ujumla.
“Sasa hivi tumejenga nyumba, tunawasomesha wadogo zetu, na maisha yetu yanakuwa bora kila kukicha. Nyumbani pamebadilika, sasa tunaheshimika kwa watu,” anasema Heavenlight.
Akimnukuu Waziri wa Vijana, Joel Nanauka, anasema mara nyingi anasisitiza kuwa ‘kazi zinazoonekana za kawaida au ngumu ndizo msingi wa mafanikio makubwa kwa vijana’.
Lakini swali la kujiuliza ni kazi ipi unaifanya kwa mtazamo na msingi upi.
Kwa pacha hawa, kazi ya kubeba mizigo haikuwa fedheha, ilikuwa daraja.
Heavenlight anasema moja ya mafanikio anayojivunia zaidi ni kupanda daraja kutoka kuwa wabeba mizigo hadi kuwa waongoza watalii katika Mlima Kilimanjaro.
Anasema hatua hiyo haikupatikana kwa bahati, ilitokana na uzoefu wa miaka mingi, kujifunza kutoka kwa wenzao, na kujituma kwa kiwango cha juu.
“Leo hii hatubebi tena mizigo, sisi ndio tunawaongoza wageni, tunahakikisha wanapanda na kushuka mlimani salama, tunawaelezea historia, jiografia na hadithi za Mlima Kilimanjaro kwa umahiri mkubwa,” anasema.
Anasema wanatambua kwamba kazi hiyo si ya kudumu. “Kila hatua, hata iwe ndogo kiasi gani, inaweza kuwa ngazi ya kupandia juu ili kufikia mafanikio unayoyatamani,” anasema Heavenlight.
Pacha hao wanatoa wito kwa wanawake na wasichana kuacha kusubiri ajira za ofisini pekee au kulalamika hakuna kazi. Wanasema zama za sasa zinahitaji uthubutu na ubunifu.
“Kulaumu pekee hakutaleta suluhisho, lazima kila mmoja atafute fursa zilizopo, hata kama zinaonekana ngumu au zisizo za kawaida.
“Kwetu sisi, kazi ya upagazi, ambayo kwa wengi huonekana ngumu au isiyofaa kwa mwanamke, imekuwa daraja la mafanikio,” anasema Heavenlight.
Zaidi ya simulizi binafsi
Simulizi ya pacha hawa si ya kipekee kwa sababu tu ni pacha wapanda mlimani, bali ni ya kipekee kwa sababu inaakisi mabadiliko yanayoendelea ya kuvunja mipaka ya kijinsia katika soko la ajira.
Katika sekta ya utalii, ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, uwepo wa wanawake katika nafasi za uongozi kama waongoza watalii unaongeza taswira chanya ya usawa na ujumuishi.
Pia unatoa ushawishi chanya kwa wasichana wengine wa vijijini kuamini kuwa ndoto zao zinawezekana.
Kwa ujumla, safari yao inaonesha mambo matatu muhimu ambayo ni elimu, uzoefu wa kazi halali na kujiamini.
Elimu, hata ile ya muda mfupi, inaweza kufungua milango mikubwa. Kazi yoyote halali inaweza kuwa chanzo cha heshima na mafanikio ya mwanamke, kama anavyoainisha Heavenlight. Mwanamke anapaswa kujiamini na kusimamia malengo ya muda mrefu kama silaha dhidi ya changamoto mbalimbali za maisha.
Anasema hata sasa wanaposimama katika njia za kupandia Mlima Kilimanjaro wakiwaongoza wageni kutoka mataifa mbalimbali, wanaona mbali zaidi ya theluji ya kilele.
Anasema wanamshukuru Mungu kwa hatua waliyofikia, wakiamini kuwa pamoja na juhudi zao binafsi, neema imekuwa nguzo katika maisha yao.
“Na ukweli unabaki kwamba mafanikio yetu tunaona yanatokana na zao la maamuzi magumu, kazi ngumu na moyo usiokata tamaa tunaoishi nao mpaka sasa,” anasema.
Katika jamii inayobadilika, simulizi ya pacha hawa inabaki kuwa mwangaza wa matumaini kwamba mwanamke anaweza kupanda mlima wowote, hata kama ni wa mawe ya msingi hadi kilele cha ndoto zake, anasema Heavenlight.