Mbarali. Katika kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kiuchumi, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, imetoa zaidi ya Sh1.7 bilioni kwa vikundi 165 vya wanawake pekee.
Hatua hiyo ni kutekeleza maelekezo ya Serikali, kuzitaka halmashauri nchini kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya wajasiriamali wadogo, kwa lengo la kukuza uchumi wa kipato.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Maendeleo Wilaya ya Mbarali, Groly Komba, leo Machi 7, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyoandaliwa katika Shule ya Msingi Majenje.
Katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi alikuwa mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo, na yalishirikisha vikundi mbalimbali vilivyo nufaika na mikopo ya asilimia 10 kutoka katika halmashauri hiyo. Kauli mbiu ya maadhimisho ni: “Ni haki na usawa kwa wanawake na wasichana ni msingi jumuishi kufikia Dira 2050.”
Amesema kauli mbiu hiyo inakumbusha uwiano wa haki, usawa na uwezeshaji wa wanawake na wasichana katika fursa za kiuchumi, pamoja na kupata elimu ya masoko, elimu ya fedha na kuzuia ukatili wa kijinsia.
“Kwa kuzingatia kaulimbiu hiyo, halmashauri katika kufanikisha uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, tumetoa mikopo ya zaidi ya Sh1.7 bilioni kwa vikundi 165, tofauti na makundi ya watu wenye ulemavu na vijana,” amesema.
Amesema mbali na uwekezaji wa mikopo ya asilimia 10, pia wamefanikiwa kuwaunganisha wanawake wajasiriamali kwenye fursa za majukwaa ya kiuchumi, sambamba na kuwahamasisha kujiunga kwenye vikundi ili kunufaika na mikopo ya taasisi za kibenki yenye riba ya asilimia 7.
Kwa upande wake, mbunge wa Mbarali, Bahati Ndingo, amewataka wanawake kuchangamkia fursa za mikopo ili kujikwamua kiuchumi na kuacha kubweteka.
“Ndugu zanguni, msikae bila kufanya shughuli. Jiungeni kwenye vikundi, mpate mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa kwenye halmashauri, lakini pia kwenye taasisi za kifedha,” amesema.
Ndingo amesema eneo hilo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika kutatua changamoto za wananchi kiuchumi, sambamba na kuhamasisha wanawake kujiamini, kudhubutu na kumtanguliza Mungu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Brigadia Maulid Surumbu, amehamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa pamoja wa bima ya afya, ambao uko katika mchakato wa hatua mbalimbali.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mbarali, Casmri Pius, amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, matukio ya shambulio la mwili 35 yaliyohusisha wanawake yameripotiwa.
Ametaja matukio mengine ni pamoja na ukatili wa kihisia ambapo wanawake 80 waliripotiwa, huku wanaume 17 wakiripotiwa, na kufanya jumla ya matukio 115 yaliyo gusa wanawake, jambo linalodhihirisha bado kuna changamoto ya mfumo wa dume.