Takukuru yakabidhi mashine za Sh18 milioni kuokoa vichanga

Mwanza. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekabidhi mashine mbili za matibabu, zenye thamani ya Sh18 milioni, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wale wanaopata ugonjwa wa manjano.

Mashine hizo ni Radiant warmer, inayotumika kuwahudumia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati kwa kuwapatia joto maalumu, na phototherapy machine, inayotumika kutibu watoto wanaopata ugonjwa wa manjano kwa kutumia mwanga maalumu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo leo Machi 7, 2026, jijini Mwanza, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila, amesema mashine hizo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo kusaidia kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga nchini.

Chalamila amesema hadi sasa Takukuru imeshatoa jumla ya mashine 15 kama hizo katika hospitali za rufaa za mikoa mbalimbali nchini, huku lengo likiwa ni kuhakikisha hospitali zote 28 za rufaa Tanzania Bara zinapata vifaa hivyo.

“Tunatoa rai kwa uongozi wa hospitali kuhakikisha mashine hizi zinatunzwa vizuri ili ziweze kuwahudumia watoto wengi kwa muda mrefu,” amesema Chalamila.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, Dk Bahati Msaki, amesema hospitali hiyo inapokea idadi kubwa ya watoto wachanga wanaohitaji huduma za kibingwa, jambo linalosababisha uhitaji mkubwa wa vifaa tiba.

Amesema kuanzia Julai 2025 hadi Februari 2026, jumla ya watoto wachanga 1,165 walilazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu mbalimbali.

“Kati ya watoto hao, 482 walikuwa wamezaliwa kabla ya wakati, huku 214 wakipata ugonjwa wa manjano muda mfupi baada ya kuzaliwa,” amesema Dk Msaki.

Ameongeza kuwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati huhitaji kuwekwa katika mashine ya joto (Radiant warmer) ili kusaidia kudhibiti joto la mwili wao, huku watoto wanaopata manjano wakitibiwa kwa kutumia mwanga maalumu kutoka kwenye mashine ya phototherapy.

Dk Msaki amesema ujio wa mashine hizo utaongeza uwezo wa hospitali hiyo kutoa huduma bora kwa watoto wachanga na kusaidia kupunguza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuilika.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali hiyo, Sibtain Maghiee, ameishukuru Takukuru kwa msaada huo na kuahidi kuwa vifaa hivyo vitatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Tunawahakikishia kuwa mashine hizi zitatunzwa vizuri na zitatumika kuwahudumia watoto wachanga wanaohitaji matibabu katika hospitali yetu,” amesema Maghiee.

Muuguzi kiongozi wa kitengo cha watoto wachanga katika hospitali hiyo, Chiku Mbuba, amesema bado kuna uhitaji mkubwa wa mashine hizo kutokana na idadi kubwa ya watoto wanaohitaji huduma hiyo.

Amesema mashine moja inaweza kumhudumia mtoto mmoja kwa wakati mmoja, huku kwa wastani ikiwa na uwezo wa kuhudumia watoto saba kwa wiki kutokana na matumizi yake ya muda wote siku saba za wiki.

Mbuba ameomba wadau mbalimbali, pamoja na sekta binafsi, kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na taasisi mbalimbali katika kuboresha huduma za watoto wachanga kwa kusaidia upatikanaji wa mashine zaidi.

Amesema hospitali hiyo inahudumia watoto wanaohitaji huduma za kibingwa kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza na mikoa jirani, hivyo kuongeza vifaa tiba ni muhimu katika kuimarisha huduma na kuokoa maisha ya watoto wachanga.