Arusha. Shirika la Viwango nchini (TBS) limeanza mchakato wa ujenzi wa maabara katika Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya kupima ubora wa bidhaa itakayorahisisha utendaji kazi wa shirika hilo na kupunguza muda uliokuwa unatumika kupeleka sampuli za bidhaa jijini Dar es Salaam.
Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini, Joseph Ismail amesema hayo jana Ijumaa, Machi 6,2026 wakati akieleza mafanikio ya shirika katika kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ubora na ufanisi zaidi.
“Shirika letu kwa kutambua Kanda ya Kaskazini ipo kwenye eneo la kimkakati tukiwa na mipaka 11 na nchi jirani ni muhimu kuwa na maabara itakayorahisisha upimaji ubora wa bidhaa ili kuwapunguzia muda wafanyabiashara kusubiri majibu kutoka Dar es Salaam, kurahisisha ufanyikaji biashara ni muhimu kwetu,” alisema Ismail
Amesema shirika hilo tangu limefungua ofisi ya Kanda ya Kaskazini mwaka 2016 hadi sasa limeweza kuthibitisha ubora wa bidhaa kwa kutoa leseni 492, zikiwemo za wafanyabiashara wakubwa 254 na wafanyabiashara wadogo 238.
“Utoaji wa leseni hizo una maana kubwa kwa shirika letu tukizingatia hii ni kanda ya kimkakati ambayo imepakana na nchi jirani ya Kenya, biashara nyingi zinafanyika ndani ya kanda hii, leseni za ubora zinawezesha urahisi wa kufanyika biashara,” alisema Ismail.
Ismail ameongeza kuwa shirika hilo pia limefanya usajili wa maeneo ya biashara zinazohusika na uzalishaji wa vyakula na usambazaji wa vipodozi, ambapo majengo zaidi ya 5,000 yamesajiliwa kwa ajili ya biashara hizo.
Aidha, amefafanua kuwa shirika limekuwa likiwachukulia hatua wazalishaji na waingizaji wa bidhaa ambao hawafuati sheria na taratibu zilizowekwa na kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, huku tani 46,000 za bidhaa zisizokidhi viwango zenye thamani ya Sh130 milioni zikiwa zimeteketezwa.
Meneja huyo amesema wameendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya bidhaa zilizothibitishwa viwango vya ubora wake kupitia taasisi za umma na binafsi na kuwataka watumiaji kujenga utamaduni wa kutumia bidhaa zenye ubora kwa hiari yao badala ya kulazimika kutumia sheria.
Hata hivyo, amekiri kuwepo na changamoto ya baadhi ya wazalishaji kutokuzingatia ubora wa uzalishaji na bidhaa zao jambo linalosababisha kuharibiwa kwa bidhaa zao na kuwataka kuhakikisha wanapeleka sokoni bidhaa ambazo ni sahihi ili mlaji aweze kupata thamani ya fedha zake.