Trump Aibuka na Onyo Kali kwa Iran Kuhusu Mashambulizi Leo

Global Publishers
March 7, 2026
0 Comments

Rais wa Marekani, Donald Trump

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameionya Iran kuwa itakumbana na mashambulizi makali leo, akidai kuwa nchi hiyo tayari inapata pigo kubwa kutokana na operesheni za kijeshi zinazodaiwa kufanywa kwa ushirikiano kati ya Marekani na Israel.

Trump alitoa kauli hiyo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akisema kuwa Iran imelazimika kubadili msimamo wake na hata kuomba radhi kwa baadhi ya majirani zake katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika ujumbe huo, Trump alidai kuwa Iran imeahidi kutoshambulia tena nchi jirani katika eneo la Ghuba, hatua ambayo alieleza kuwa imesababishwa na mashambulizi makali na ya mara kwa mara kutoka kwa Marekani na Israel.

“Iran, ambayo kwa sasa inapigwa vibaya sana, imeomba radhi kwa majirani zake wa Mashariki ya Kati na kuahidi haitowashambulia tena,” aliandika Trump katika ujumbe wake.

Hata hivyo, rais huyo alionya kuwa mashambulizi zaidi yanaweza kuendelea, akisisitiza kuwa Iran itakabiliwa na hatua kali zaidi za kijeshi.

“Leo Iran itapigwa vibaya sana,” aliongeza Trump, huku akibainisha kuwa baadhi ya maeneo na makundi ambayo hapo awali hayakuwa yakizingatiwa kama malengo ya kijeshi sasa yanaweza kujumuishwa katika mashambulizi kutokana na kile alichokiita tabia mbaya ya Iran.

Kauli hiyo imeongeza taharuki na mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati, wakati hali ya usalama ikiendelea kuwa tete kufuatia mfululizo wa mashambulizi na matamko makali kati ya pande zinazohusika katika mzozo huo.