Wanawake wachimbaji madini Mkoani Geita wamehimizwa kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia benki ya NMB ili kukuza na kuinua shughuli zao za uchimbaji na biashara zinazohusiana na sekta ya madini.
Wito huo umetolewa leo Machi 07, 2026, Mkoani humo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu wakati akizungumza katika kongamano la wanawake wachimbaji madini lililofanyika mkoani Geita.
Dkt. Jingu amesema Serikali imeweka mazingira rafiki ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo na mafunzo ya ujasiriamali, na kuwataka wanawake wachimbaji madini kujitokeza kuomba mikopo hiyo ili kuimarisha shughuli zao na kuongeza tija katika sekta ya madini.
Amesema wanawake ni uti wa mgongo wa familia, jamii na Taifa, hivyo wanapowezeshwa kiuchumi familia zao hupata maendeleo na ustawi.
“Serikali ipo tayari kusaidia wachimbaji madini, hususan wanawake, ili waweze kunufaika na fursa zilizopo katika sekta ya madini na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi,” amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini, Salma Ernest amesema chama hicho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika huduma za kijamii nchini.
salam amesema kupitia chama hicho wamefanikiwa kusaidia miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule mkoani Tanga pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wafungwa katika baadhi ya magereza nchini.
Aidha amesema chama hicho kinaendelea kuwawezesha wanawake wachimbaji madini kwa kuwapa elimu ya fedha, kuwahamasisha kuanzisha miradi ya pamoja na kukuza shughuli zao za kiuchumi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya jamii.