Mwamuzi Amin Mohamed Amin Omar wa Misri, aliyewahi kuchezesha mechi ya ‘Kariakoo Derby’ kati ya Yanga dhidi ya Simba iliyopigwa, Juni 25, 2025, amechaguliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kuchezesha fainali za Kombe la Dunia.
Katika fainali hizo za Kombe la Dunia zitakazopigwa nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico kuanzia Juni 11, 2026, hadi Julai 19, 2026, Amin Omar ni miongoni mwa waamuzi wa kati watano kutoka Afrika walioteuliwa kupeperusha bendera.
Amin ni mwamuzi aliyeingia katika kumbukumbu za kuchezesha mechi ya ‘Kariakoo Derby’, iliyopigwa Juni 25, 2025, Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini, Dar es Salaam, ikiwa ndio iliyowapa ubingwa Yanga wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2024-2025.
Katika pambano hilo la Juni 25, liliingia pia kwenye rekodi mpya baada ya kuchezeshwa na waamuzi kutokea Misri na mwamuzi wa kati alikuwa ni Amin Mohamed Amin Omar, akisaidiwa na Mahmoud Ahmed Abo El Regal na Samir Gamal Saad Mohamed.
Mwamuzi wa akiba, ‘Fourth Official’, alikuwa ni Ahmed Mahrous Elghandour kutokea pia Misri, huku mtathimini wa waamuzi alipangiwa, Alli Mohamed kutoka Somalia, wakati Kamisaa wa mechi hiyo alikuwa, Salim Omary Singano kutoka mjini Tanga.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Pacome Zouzoua kwa penalti ya dakika ya 66, baada ya nyota huyo kufanyiwa madhambi eneo la hatari na kipa wa Simba, Moussa Camara, kisha, Clement Mzize akafunga la pili dakika ya 86.
Ushindi huo kwa Yanga uliifanya kutangazwa rasmi mabingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2024-2025, baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 27, sare moja tu na kupoteza miwili, ikiwa na pointi 82, ukiwa ni ubingwa wa 31, kwa ujumla, tangu mwaka 1965.
Waamuzi wengine wa Afrika walioteuliwa ni Dahane Beida kutoka Mauritania, ambaye anakumbukwa msimu wa 2023-2024, baada ya kulikataa bao la wazi la Yanga, katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini.
Katika mechi hiyo ya robo fainali iliyopigwa Afrika ya Kusini, Aprili 5, 2024, Yanga ilifunga bao kupitia kwa aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Stephane Aziz KI, ingawa mwamuzi huyo alilikataa kwa madai mpira ulikuwa haujavuka kwenye mstari.
Mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya marudiano, ilizua sintofahamu kwa msimu huo, jambo lililoipa faida, Mamelodi Sundowns kushinda kwa penalti 3-2 na kutinga nusu fainali, baada ya timu hizo kutoka suluhu (0-0) kwenye mapambano yote mawili.
Pia, Beida, ndiye aliyechezesha fainali ya Simba ya Kombe la Shirikisho Afrika, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Mei 25, 2025, ambapo kikosi hicho kilitoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Katika fainali hiyo, Simba ilikuwa inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 3-0, ingawa ilikosa ubingwa huo wa Afrika, baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Morocco, Mei 17, 2025, kuchapwa mabao 2-0, hivyo, kukosa taji hilo kwa jumla ya mabao 3-1.
Waamuzi wengine wa kati walioteuliwa ni Mustapha Ghorbal wa Algeria, Jean-Jacques Ndala (DR Congo) ambaye anakumbukwa kwa kuchezesha fainali ya AFCON 2025, mchezo ambao ulikuwa na utata mkubwa na Pierre Ghislain Atcho wa Gabon, huku watatu watasimamia teknolojia ya mwamuzi msaidizi wa video (VAR), ambao ni Mahmoud Ashour wa Misri.
Wengine watakaosimamia teknolojia ya mwamuzi msaidizi wa video (VAR), mbali na Mahmoud Ashour wa Misri ni Letticia Viana wa Eswatini na Lahlou Benbraham kutoka Algeria, wakihitimisha orodha ya waamuzi wanane wa Afrika watakaochezesha Kombe la Dunia.