Anapenda sana ‘mchezo’ nahisi kuishiwa nguvu

Anti siyo kama ninajihami ila naona kabisa ubavu wangu ni mdogo kumtosheleza huyu nimpendaye. Kwanza kila akikaa anasema anapenda mwanaume mwenye maumbile makubwa, nikitazama yangu nakataa tamaa kabisa. Pia anapenda sana mambo hayo, nisipojizungusha kutwa moja anaweza kuhitaji hiyo huduma zaidi ya mara tano. Mwanzoni nilijua ni ugeni, lakini tuna mwaka sasa kazi ni hiyo hiyo.

Kila nikijitafakari nakata tamaa ya kumuoa kwa kuona kabisa sitokidhi haja zake.

Kuna mtu aliniambia siku za mwanzo nikikaa naye baada ya muda ataacha tabia ya kupenda kujamiiana, ila naona inazidi.

Natamani kila mara niwe nimesafiri kikazi ili nipumzike maana akija nyumbani badala ya kufurahia nasema kimoyo moyo… kazi imeanza…

Nishauri niishi naye nyumba moja kabla ya kumuoa ili nione kama atakinahi kisha nimuoe kama atakuwa mambo ni hayo hayo nimuache maana sitomuweza. Au nifanye nini Anti nisije kuolea watu mke bure.

Katika uhusiano wa kimapenzi, suala la kujamiiana ni sehemu muhimu ya ukaribu wa kihisia na kimwili kati ya wapenzi. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo mmoja anaweza kuwa na hamu kubwa zaidi kuliko mwenzake, au mwenzake akahisi hana uwezo wa kuridhisha matarajio ya mwenzi wake. Tukianza na maumbile makubwa au madogo, nani amekuambia kama maumbile yako madogo. Pengine anasema hivyo akimaanisha anayapenda maumbile yako. Tafadhali acha kujitisha, hakuna maumbile makubwa wala madogo muhimu kujua jinsi ya kuyatumia. Ila hili ni darasa la siku nyingine.

Mara nyingi huwa ninasema kwenye mahusiano jambo muhimu ni kuzungumza na si kukaa kimya kuugulia moyoni.

Kaa na mpenzi wako na umueleze kwa utulivu jinsi unavyojisikia. Eleza kuwa unathamini uhusiano wenu na unatamani kumridhisha, lakini unakabiliwa na changamoto fulani (mfano siku zote unavyokutana naye zaidi ya raundi tatu unajitutumua sana na unaelekeza kuishiwa pawa). Mazungumzo ya wazi husaidia pande zote kuelewana. Mara nyingi, matarajio yasiyozungumzwa ndiyo chanzo cha hofu.

Unaweza kushangaa anakueleza hata yeye uhitaji mara nyingi akidhani ndiyo kitu unachokipenda. Kwa kawaida wanawake wengi hufanya mambo kwa kuwafikiria zaidi wenza/wapenzi wao, hivyo pengine anajitutumua ili kukushawishi umuoe kwa kumuona anayaweza mambo ya faragha.

Lakini ukaribu wa kimapenzi hauishii kwenye tendo lenyewe. Kujenga mazingira ya mapenzi kwa kuonyesha upendo, kugusana kwa upole, kupeana muda wa kimahaba na kuzingatia mahitaji ya kihisia ya mwenzi wako kunaweza kuongeza kuridhishana hata kabla ya tendo. Wakati mwingine, tatizo huwa si uwezo wa mwili pekee bali presha ya kufanya vizuri. Kuondoa presha na kulichukulia tendo kama sehemu ya upendo, si mtihani wa uwezo, husaidia sana.

Zaidi ya yote, usijione umeshindwa au hufai. Uwezo wa mwanaume au mwanamke haupimwi kwa tendo moja au muda fulani. Kujiamini, kuwa tayari kujifunza na kuboresha, pamoja na kuwa wazi kwa ushauri wa kitaalamu, ndizo hatua sahihi. Ikiwa mpenzi wako anakujali kwa dhati baada ya mazungumzo na ukamueleza changamoto uliyonayo, atakuwa tayari kushirikiana nawe katika kutafuta suluhisho badala ya kukuhukumu.

Kwa hiyo, badala ya kukata tamaa, chukua hatua ya kuwasiliana, kuboresha afya yako na kutafuta ushauri wa kitaalamu inapohitajika. Changamoto za kimapenzi ni za kawaida katika uhusiano, lakini kwa mazungumzo, subira na jitihada za pamoja, zinaweza kushughulikiwa na hata kuimarisha uhusiano wenu.