Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimeungana na wanawake wa Tanzania na dunia kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, kikituma salamu za pongezi huku kikisisitiza umuhimu wa haki na usawa kwa wanawake katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa leo Jumapili, Machi 8, 2026, maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “haki na usawa, ukitoa umepata, chukua hatua,” ambayo chama kinasema inalenga kuhamasisha wanawake kuungana kudai haki zao huku wakitimiza wajibu wao kama raia wazalendo.
“Chama cha Demokrasia na Maendeleo kinawatakia wanawake wa Tanzania na dunia kwa ujumla heri ya sikukuu ya wanawake.”
Kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema, haki na usawa, ukitoa umepata, chukua hatua, bila shaka kauli mbiu hii itachochea ari na nguvu zaidi katika kuwaunganisha wanawake wa Tanzania ili kudai haki huku wakitimiza wajibu wao kama raia wazalendo wanaolipenda Taifa lao,” inaeleza taarifa hiyo, iliyosainiwa na Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho.
Machi mosi, 2026, baraza hilo lilitangaza kwamba litaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika Kanda ya Serengeti, mkoani Mara.
Hata hivyo, jana Machi 7, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, alitangaza marufuku ya kufanyika kwa tukio hilo kwa kile alichodai linakwenda kinyume na amri ya Mahakama iliyokitaka chama hicho kisimamishe kufanya shughuli za kisiasa hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika mahakamani.
Hata hiyo, Bawacha kupitia Katibu Mkuu wake, Pamela Massay, ilieleza kuendelea na maandalizi, huku wanachama wake wakisafiri kutoka mikoa mbalimbali nchini kuelekea Musoma. Taarifa zinazosambaa mitandaoni zinaeleza, wanawake wa Bawacha walikamatwa na au kuzuiwa maeneo mbalimbali kabla ya kufika Musoma.
Leo ikiwa ni siku ya maadhimisho hayo, Polisi wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanawake wa Bawacha, Mjini Musoma kabla ya kwenda kushiriki maadhimisho hayo.
Baadhi ya wanachama na viongozi wa Bawacha akiwemo Katibu Mkuu wake, Pamela Massay wamekamatwa na Polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara (RPC), Pius Lutumo amekiri kuwepo kwa tukio hilo ingawa amesema mabomu yaliyorushwa ni machache na hivi sasa hali ni shwari mjini Musoma.
Kuhusu watu waliokamatwa Kamanda Lutumo amesema atatoa taarifa baadaye.
“Mabomu yamerushwa kama mawili tu lakini kuhusu watu kukamatwa hebu nipe muda ila kikubwa ni kwamba Musoma hali ni shwari tunaendelea na majukumu yetu kama kawaida,” amesema.
Taarifa ya Chadema ya maadhimisho ya wanawake wa chama hicho imesema yamefanyika katika mazingira tofauti na yaliyotarajiwa baada ya baadhi ya wanachama wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kuzuiwa au kukamatwa katika maeneo mbalimbali walipokuwa wakielekea Musoma mkoani Mara kushiriki kilele cha maadhimisho hayo.
Taarifa ya chama hicho ilidai kuwa baadhi ya wanawake hao walikamatwa wakiwa ndani ya mabasi na kupelekwa katika vituo vya polisi huku wengine wakirudishwa walipotoka walipokuwa wakisafiri kuelekea Musoma.
Ilidai wengine walizuiliwa hata kabla ya kuanza safari wakidaiwa kukiuka sheria inayozuia kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya wanawake waliokuwa wakielekea Musoma waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi huku wengine wakinyimwa dhamana.
Taarifa hiyo imedai kuwa miongoni mwa wanawake hao wapo wajawazito, wanaonyonyesha na wenye ulemavu.
Chama hicho kinasema jumla ya wanawake 6,912 walikuwa wakitarajiwa kushiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyopangwa kufanyika Musoma Machi 8, 2026.
Aidha, chama hicho kinadai zaidi ya wanawake 1,300 hawajulikani walipo baada ya kuzuiliwa katika maeneo mbalimbali walipokuwa wakielekea mkoani Mara.
“Kamatakamata hiyo ilianza Ijumaa Machi 6, 2026 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Pwani, Morogoro, Geita, Simiyu, Singida, Iringa na Mara,” inadai taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo, Chadema pia imelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia wanawake hao bila masharti ili waweze kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani wakiwa uraiani.
Hatua hiyo imewaibua Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ambao wametoa tamko wakieleza masikitiko yao kuhusu kile walichodai ni kuzuia wanawake waliokuwa wakielekea Musoma kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Katika tamko lake lililotolewa Machi 8, 2026, mtandao huo umesema Siku ya Wanawake Duniani ni muhimu inayotambuliwa kimataifa kwa ajili ya kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kitamaduni pamoja na kutathmini hali ya haki za wanawake duniani.
Hata hivyo, THRDC ilieleza kuwa imepokea kwa masikitiko taarifa za matukio yaliyotokea kati ya Machi 6 na 8, 2026 ambapo, kwa mujibu wa mtandao huo, baadhi ya wanawake wa Bawacha walizuiwa katika maeneo mbalimbali walipokuwa wakielekea Musoma kwa ajili ya maadhimisho hayo.
“Wanawake hao walizuiwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mlandizi, Dumila, Gairo, Geita, Dodoma na Bunda,” ilidai sehemu ya tamko hilo.
Katika tamko hilo, mtandao huo umeitaka Serikali na vyombo vya dola kuhakikisha wananchi wanaruhusiwa kushiriki katika maadhimisho ya siku za haki za binadamu zinazotambuliwa kimataifa na kitaifa bila vikwazo, huku ukisisitiza kuwa haki za wanawake ni sehemu ya haki za binadamu zinazopaswa kulindwa kwa wote bila ubaguzi.
Endelea kufuatilia Mwananchi