Dar es Salaam. Leo dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake, tukio linalotolewa heshima kwa wanawake kwa mchango wao katika familia, jamii na Taifa kwa jumla.
Hii ni fursa ya kuangalia jinsi wanawake wa mijini Tanzania wanavyobadilisha maisha yao, wakipambana na changamoto za kila siku huku wakiimarisha kipato na nafasi yao kiuchumi.
Katika mitaa ya jiji, kutoka Kariakoo hadi Mbagala, wanawake wengi wamejikita katika biashara ndogo ndogo, huduma, kazi za kitaaluma na biashara za mtandaoni.
Bidhaa zinazouzwa ni za kila aina, kutoka chakula na nguo, hadi bidhaa za urembo na mikono ya asili.
Mabadiliko haya yanathibitisha kuwa wanawake sasa ni nguzo muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Wanawake wafanyabiashara ndogondogo katika eneo la Tabata Mwananchi wakiendelea na shughuli zao leo ikiwa ni siku ya wanawake duniani.
Akizungumza na Mwananchi Asha Mtemvu, mama wa watoto wawili kutoka Mbagala, Dar es Salaam amesema kuadhimisha Siku ya Wanawake ni fursa ya kutafakari jinsi maisha yake yalivyobadilika.
“Nilianza kwa kuuza maandazi na chai asubuhi. Leo, biashara yangu imesambaa na naweza kuchangia gharama zote za familia. Siku ya Wanawake inanikumbusha jinsi juhudi zetu zinavyothaminiwa na jamii,” amesema Asha.
Mbali na biashara ndogo ndogo, mitandao ya kijamii na teknolojia imefungua milango mipya ya fursa mfano wa hilo ni Rehema Said, anayejishughulisha na biashara ya nguo mtandaoni, amesema teknolojia imebadilisha kabisa maisha ya wanawake.
“Nilianza kwa kuuza nguo chache kwa marafiki zangu kupitia simu. Leo nina wateja wengi na napokea oda kutoka maeneo mbalimbali. Faida yake ni kwamba leo ninaweza kuuza bidhaa zangu popote duniani bila kuondoka nyumbani. Siku ya wanawake ni fursa ya kuthamini nguvu hii ya kidijitali,” amesema.
Fatuma Juma, mkazi wa Dar es Salaam, anatumia mitandao ya kijamii kuuza bidhaa za urembo na kudumisha maisha ya familia yake.
“Nilipata wateja wangu wa kwanza kupitia WhatsApp na Instagram. Sasa biashara yangu inapanuka na hata nimeanza kutoa mafunzo kwa wanawake wengine kuhusu jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii kukuza biashara zao,” amesema Fatuma.
Kwa upande wake, Asha Mwinyi ameamua kutumia majukwaa ya mtandaoni kuuza bidhaa zinazotengenezwa kwa vifaa vya asili.
“Teknolojia imenisaidia kufikia wateja wengi zaidi kuliko ningeweza kufanikisha kwa dukani pekee. Pia, ninaweza kudhibiti biashara yangu wakati wowote, na hii imenifanya niwe huru kifedha na kuimarisha maisha ya familia yangu,” amesema Asha.
Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha wanawake wanachangia kiasi kikubwa katika sekta zisizo rasmi, ikiwamo biashara ndogo ndogo, huduma na biashara mtandaoni.
Sekta hii ni tegemeo muhimu kwa wanawake wa mijini kwani haihitaji mtaji mkubwa kuanza, ingawa changamoto za mitaji na masoko bado zipo.
Mchumi wa masuala ya kijamii, Neema Komba amesema mabadiliko ya maisha ya wanawake wa mijini ni ishara ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii.
“Wanawake wanapopata kipato, mara nyingi huwekeza zaidi katika elimu, afya na maendeleo ya familia zao. Kuwawezesha wanawake kibiashara ni kipaumbele cha taifa lolote,” amesema Komba.
John Kitomari, mchambuzi wa masuala ya maendeleo ya jamii, anaongeza kuwa mabadiliko haya yanaendana na mabadiliko mapana ya kijamii na kiuchumi yanayotokea kwenye miji mikubwa.
“Ukuaji wa miji na ongezeko la gharama za maisha vimefanya familia nyingi kutegemea kipande cha pande zote mbili, jambo linalowasukuma wanawake kushiriki zaidi katika shughuli za kiuchumi. Zamani mwanamke alionekana zaidi kama mlezi wa familia, lakini sasa hali imebadilika. Tumeona mwanamke akibadilisha maisha yake na familia yake kupitia biashara, uongozi na ajira. Hii ni hatua muhimu katika mabadiliko ya kijamii,” amesema Kitomari.
Hata hivyo, gharama za maisha mijini, kupanda kwa kodi za nyumba, na uwajibikaji mkubwa wa familia vinabakia kuwa mzigo kwa wanawake wengi.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi na ajira, Elena Mbise amesema wanawake wengi wanakabiliana na changamoto ya kusawazisha kazi na majukumu ya nyumbani.
“Pamoja na maendeleo ya kiuchumi, bado wanawake wanabeba mzigo mkubwa wa malezi na kazi za nyumbani. Ili mabadiliko haya yawe na tija, jamii na Serikali zinapaswa kutoa msaada wa kutosha wa kijamii na kifedha,” amesema Profesa Mbise.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii na wanawake, Halima Msuya amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa mtaji wa awali, upatikanaji mdogo wa masoko ya uhakika na changamoto za teknolojia kwa wanawake ambao hawana ujuzi wa kidijitali.
Wanawake wafanyabiashara ndogondogo katika eneo la Tabata Mwananchi wakiendelea na shughuli zao leo ikiwa ni siku ya wanawake duniani.
“Wanawake wengi wanakosa rasilimali za kutosha kuanza biashara zao mtandaoni. Pia, baadhi ya wanawake hawana ujuzi wa kutumia majukwaa ya mtandaoni kikamilifu, jambo linalowapunguzia wateja na faida,” amesema Halima.
Mkurugenzi wa asasi ya Wanawake na Ujasiriamali (WaU) Neema Lyimo amesema Serikali na sekta binafsi zinapaswa kushirikiana kuhakikisha wanawake wanapata mikopo, mafunzo ya biashara, na masoko ya uhakika.
“Wanawake wanapopewa rasilimali na mafunzo yanayowezesha kutumia teknolojia, wanakuwa huru kifedha na kudumisha maendeleo ya familia zao. Sera na mikakati inapaswa kuzingatia changamoto hizi ili kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma.”
Mbise pia amesema Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo ya vikundi, mafunzo ya biashara na sera zinazolenga kuimarisha usawa wa kijinsia katika ajira na uongozi.
“Endapo hatua hizo zikitekelezwa vizuri, zinaweza kusaidia wanawake wengi kupanua shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kipato cha familia zao,” amesema Mbise.