Moshi. Hali si shwari, ndivyo unaweza kuelezea misuguano iliyopo ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Manispaa ya Moshi huku baadhi ya viongozi na wanachama wakigawanyika katika makundi mawili yanayosigana.
Ni kutokana na msuguano huo, kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho ambacho kiliketi jana Jumamosi Machi 7, 2026 katika ukumbi wa CCM mkoa almanusura kisifanyike, kama sio busara za Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi.
Kikao hicho kilichokuwa na ajenda ya kupokea taarifa ya utekelezaji ilani ya CCM, kilihuduriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava na mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo ambaye hata hivyo aliondoka kulipotokea tafrani.
Mwenyekiti wa CCM mkoa Kilimanjaro,Patrick Boisafi (kushoto) akitafakari jambo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Moshi Mjini, kilichofanyika Machi 7,2026. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava na Mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, Faraji Swai.
Tukio hilo linakuja takribani wiki moja tangu mlezi wa mkoa huo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid kuitisha kikao cha maridhiano kilichofanyika Machi mosi, 2026.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro (RC), Nurdin Babu, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Ibrahim Shayo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo.
Wengine waliohudhuria kikao hicho cha upatanisho ni na mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Seleman Mfinanga, Katibu mwenezi wa CCM Manispaa ya Moshi, Athman Ally na Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu.
Baada ya kufungua kikao, mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Moshi, Faraji Swai walijitokeza baadhi ya wajumbe wakimtaka apokee taarifa kabla ya taarifa ya utekelezaji wa ilani kuwasilishwa.
Wakati kundi hilo likipaza sauti likimtaka mwenyekiti apokee taarifa kabla ya kuendelea na kikao, liliibuka kundi lingine likipaza sauti kuwa hao wanaoleta tafrani waondolewe ukumbini, tafrani zilizodumu kwa takribani dakika 10.
Mwenyekiti huyo wa wilaya akalazimika kusimama na kueleza kuwa, “napenda niwafahamishe kwamba sina ajenda ya taarifa. Sina ajenda ya taarifa na sina taarifa ya kupokea kutoka kwenu. Huo sio utaratibu wa chama chetu.”
“Mimi nimetangaza rasmi kwamba nimefungua kikao changu, kikao kiendelee, chama chetu cha mapinduzi kina utaratibu wake na hawa vijana wamejipanga kuleta vurugu. Nakuomba (kiongozi wa usalama) uchukue nafasi yako,”amesisitiza.
Hata baada ya kauli hiyo, bado kundi lililokuwa likimtaka apokee taarifa kwanza lilisikika likipaza sauti kuwa “hakuna kikao hapa hadi upokee taarifa,” huku kundi lingine likitaka kundi hilo linaloleta tafrani liondolewe ukumbini.
Ni kutokana na tafrani hiyo, wakuu wa idara na wataalamu wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi waliokuwa wawasilishe taarifa ya utekelezaji walitoka nje na baadaye kurudi ukumbini baada ya hali ya hewa kutulizwa na Boisafi.
Akizungumza katika kikao hicho, Boisafi amesema kilikuwa ni mahsusi kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa miezi sita kuanzia Juni hadi Desemba 2025, huku akiwaomba radhi wataalamu wa halmashauri kwa kile kilichotokea ukumbini.
“Wataalamu hapa mmeona vitu ambavyo hamkuzoea kuviona lakini hizi ndio siasa. Hakuna jambo la ajabu limetokea ni jambo la kutafakarisha na nasikitika. Kikao hiki kina ajenda na ajenda ziko nne,”amesema mwenyekiti huyo.
Wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Moshi mjini wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika Machi 7,2026 katika ukumbi wa CCM mkoa wa Kilimanjaro.
“Kuna ajenda zinahusu utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo kwayo ninyi wataalamu mngekuwa mnawasilisha kwa kupitia kamisaa wetu, tukimaliza tungewaomba mtoke nje na waandishi wa habari pia wangetupisha,”amesema.
“Lakini yametokea yaliyotokea. Haya yatajadiliwa baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama chetu na ajenda itakayofuata na mwenyekiti wa wilaya ataisimamia,”amesisitiza Boisafi wakati akijaribu kuweka mambo sawa.
“Chama chetu kina taratibu zake. Unaandika kwa mamlaka, watasoma watakuiteni na kuwasikiliza na baadaye kujadiliana. Kukosoa na kukosolewa ni sehemu ya miongozo kwenye chama chetu,”amesisitiza Boisafi.
“Tusipoenda hivyo, mnajua hii wilaya ilikuwa wapi. Miaka 25 tumekataa maendeleo yetu wenyewe. Miaka mitano ya nyuma tukakubali tunataka maendeleo, miaka mitano hii (2025-2030) tukasema tunataka maendeleo.
“Lakini sasa kama mnataka kuturejesha kule tulipotoka. Niwaombe wajumbe wa Halmashauri Kuu wa Wilaya ya Moshi mjitafakari. Tunataka kurudi kule tulipotoka au tunataka kwenda mbele na kwenda mbele tunatakiwa tufanye nini.”
“Tunasema mamlaka yanatoka kwa Mungu, basi tuheshimu mamlaka. Tusikilize. Kama kuna ushauri tuutoe. Tusiposikilizwa ndio hatua zinazostahiki zilichukuliwe.
“Lazima tujue hilo, na kuonesha ukomavu, kukua kisiasa, kwenye maisha, kwenye uchumi na nini lazima muoneshe. Mlichokionyesha hapa mbele ya hawa watendaji, kesho kutwa mtaenda kukagua miradi pia,”amesema.
“Wameona pia mlivyojipambanua hapa. Sasa mkijipambanua tofauti mnawashauri nini. Kwa hiyo ninyi watendaji mjisikie hamjaona jambo la ajabu tuliopewa dhamana na wanachama wetu mjisike hamjafanya jambo zuri.”
Ingawa hadi kikao hicho kinafungwa taarifa hiyo haikutolewa, lakini taarifa za ndani zinadai wajumbe hao walitaka kauli ya chama juu ya ujumbe wa kigogo wa wilaya ambao aliutuma kwa bahati mbaya na kuuweka katika ‘status’ yake.
“Hii ndio habari ya mjini kaeni mkao wa kula. Tumeshawasha taa nyekundu hatutabakisha mtu tunawatoa wote,” unasomeka ujumbe huo na akawataka viongozi wawili kwa majina kuwa ndio walengwa.
Ukiacha ujumbe huo, kumekuwa na mvutano juu ya nani anapaswa kuunda mfuko wa jimbo, ingawa sheria iko wazi kuwa wajumbe ambao ni madiwani wawili, watendaji wa kata wawili na mjumbe wa Asasi za Kiraia wanateuliwa na madiwani.
Mkuu wa wilaya ya Moshi ambaye pia ni Kamisaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava akizungumza katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho Moshi mjini kilichofanyika Machi 7, 2026
Mbali na hilo, lakini kuna mgawanyiko mkubwa ulioanzia katika kura za maoni za mwaka 2020 katika nafasi ya ubunge na kuwagawa viongozi na wanachama katika makundi mawili na msuguano huo uliendelea katika kura za maoni 2025.
Msuguano huo ulikolezwa na mijadala hasi iliyokuwa ikiendelea katika makundi sogozi manne yaliyokuwa yakitumika kutukana na kuchafua baadhi ya viongozi.