Ceasiaa yapania pointi 18 nyumbani

KOCHA wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka amesema mipango ya timu hiyo ni kuvuna pointi 18 katika mechi sita za nyumbani zilizosalia ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza nne bora.

Ceasiaa iko nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikikusanya pointi nane kwenye mechi 11 ilizocheza, ushindi mara mbili, sare saba na kupoteza mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti Chobanka alisema malengo hayo yanawezekana iwapo wachezaji wake wataendelea kujituma na kupambana katika kila mechi watakayocheza.

“Kwenye mechi za nyumbani tunapaswa kuwa makini zaidi, malengo yetu ni kupata pointi 18 hizo mechi sita zilizosalia tutajua tunapambania wapi,” alisema Chobanka

“Tunao uwezo wa kupambania hilo kwenye mechi hizo 11, sita tuhakikishe tunachukua pointi nyumbani na tano za ugenini tuangalie tunatokaje hapo.”

Kocha huyo aliongeza ligi ya msimu huu imekuwa na ushindani mkubwa, jambo linalozifanya timu nyingi kupambana kutafuta pointi tatu kwa ugumu.