ALIYEWAHI kuwa kocha mkuu wa JKT Queens, Esta Chabruma amewaasa mabinti wanaocheza soka kuendelea kupambania ndoto zao bila kukata tamaa licha ya changamoto wanazokutana nazo njiani.
Akizungumza na Mwanaspoti kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Chabruma alisema wanawake wengi wenye vipaji hukata tamaa mapema kutokana na vikwazo wanavyokutana navyo akasisitiza mafanikio yanahitaji uvumilivu na kujituma.
Chabruma alisema hata yeye wakati anaanza safari yake ya soka alipitia changamoto nyingi, lakini hakuruhusu hali hiyo kumrudisha nyuma kufikia malengo yake.
“Hata mimi wakati naanza kucheza nilipitia changamoto nyingi na kila sehemu haikosi changamoto, ni vile tu wewe utawezaje kuzikwepa na kupambania kile unachokiamini,” alisema Chabruma.
Alieleza safari ya mafanikio kwa wanasoka au mwanamke yeyote katika jamii mara nyingi huwa na vikwazo mbalimbali, lakini kinachotakiwa ni kuwa na moyo wa kupambana na kutokata tamaa.
“Wakati sisi tunacheza haikuwa kama ajira moja kwa moja kwa sababu hata timu zenyewe hazikuwa nyingi na ligi haikuwepo, kwa hiyo sasa hivi mpira ni fursa ni ajira kwa wasichana ninachowaasa wasiache hata kama watakutana na changamoto ipi.”
“Katika kila kazi nidhamu ni kila kitu, ukiwa na nidhamu na kujituma utaweza kufika mbali zaidi na sio tu kwenye soka hata sehemu zingine unaweza kuwa na kitu kikubwa lakini nidhamu ikakuangusha.”
Kabla ya kuwa kocha Chbaruma aliwahi kuitumikia Sayari Queens moja ya timu za kwanza alizocheza Tanzania kisha akacheza Katodora FC (Sweden) alipoitumikia misimu mitatu akawa mchezaji wa kwanza wa kike kucheza soka Ulaya.