Dar es Salaam. Picha iliyotumwa kwa kuaminiwa kama ishara ya upendo, huenda ikageuka silaha ya fedheha, vitisho, visasi na kusababisha maumivu ya kudumu.
Katika zama hizi za teknolojia, simu janja na mitandao ya kijamii imekuwa chombo cha kuwasiliana lakini pia imeibua tishio jipya la kisaikolojia na kijamii kusambazwa bila ridhaa kwa picha na video za faragha.
Intaneti imeifanya dunia kuwa kijiji kwani urahisi wa kubadilishana picha za faragha kati ya wapenzi haufanyi kazi tumaini la mapenzi, bali pia linaweza kuwa njia ya kusambaza picha hizo kwa haraka na kusababisha madhara kwa mhusika.
Kufuatia hilo gazeti hili limezungumza na wanasaikolojia ambao wameonya kuwa kusambaza picha za faragha si tu kosa la kimaadili, bali ni aina mpya ya ukiukaji wa haki za binadamu unaoacha majeraha yasiyoonekana kwa macho.
Onyo hili limekuja baada ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kuwataka wanawake kuacha tabia ya kutuma picha zisizo na staha kwa wenza wao, kwa kile alichoeleza picha hizo hugeuka mwiba mapenzi yanapoisha.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika, “Mnapoanzisha uhusiano wa kimapenzi, msikubali kupigwa au kutuma picha ambazo hazina staha eti kwamba mnafanya uwekezaji au promo ya kuchochea mapenzi,’’ anasema na kuongeza:
“Hizo picha ambazo hazina staha mnazotumiana, kwa wengi wenu zimegeuka mwiba wa kukomoana mnapokorofishana na wanaothirika zaidi ni wanawake halafu wananiletea malalamiko ambayo kimsingi nawaomba muwe mnapeleka polisi kwa hatua za kisheria,”
Mwanasaikolojia tiba, Dk Elitruda Mlay anasema usambazaji wa picha za faragha ni aina mpya ya ukiukaji wa haki ya binadamu, na inaweza kusababisha madhara makubwa ya kisaikolojia na kijamii kwa mwathirika.
Anasema tukio hilo huibua hisia za aibu, hasira, wasiwasi uliokithiri na hata msongo wa mawazo.
“Waathirika wengi huzungumza kuhusu hisia ya kukosa thamani, kujilaumu na kushindwa kulala au kula kutokana na mawazo ya kuona picha zao zikisambaa kwa watu wasiowafahamu.Matokeo yake, waathirika wengi hupata shida ya kimawazo na kijamii ambayo inaweza kudumu kwa miezi au hata miaka,” anasema.
Akiweka msisitizo katika hilo mwanasaikolojia wa jamii, Amina Selemani, anaeleza kuwa madhara ya tukio hilo yanaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi ya watu wanavyodhani.
“Fedheha ya hadharani huathiri sana taswira binafsi.Mtu anaweza kuishi kwa hofu ya kudumu kwamba picha hizo zitajitokeza tena baadaye, labda wakati wa kuomba kazi au kuanzisha familia. Hiyo ni mizigo ya kisaikolojia inayobebwa kwa muda mrefu,” anasema.
Hata hivyo, Amina anaasema kukabiliana na hali hiyo kuna umuhimu wa jamii kuepuka kumgeuza mwathirika kuwa chanzo cha tatizo na badala yake kutafuta namna ya kumsaidia ili kumpunguzia machungu.
“Ni sawa kuhamasisha tahadhari, lakini tusisahau kuwa kosa la msingi liko kwa anayesambaza picha. Tukimlaumu zaidi mwathirika, tunachochea ukimya na kuzuia watu kuripoti vitendo hivi,” anaeleza.
Mshauri wa masuala ya uhusiano, Clara Jeremia anaasema mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na kutupiana picha za utupu, hivyo ni muhimu wanajamii wakaelewa hatari ya kufanya hivyo haiishii kwenye mapenzi.
“Kuna dhana potofu kwamba kutuma picha za faragha ni ishara ya kujiamini au kuwekeza kwenye uhusiano. Ukweli ni kwamba mapenzi yenye afya yanajengwa kwa heshima, mawasiliano na uaminifu si kwa picha.
“Wengine hutuma kwa shinikizo, wakiamini wakikataa wataachwa. Hapo tayari kuna dalili za unyanyasaji wa kihisia,” anasema na kuongeza:
“Kabla ya kubonyeza kitufe cha ‘tuma’, kumbuka picha moja ni sawa na sura yako inaweza kuishi milele mtandaoni. Heshimu faragha yako, fahamu athari zake, na chukua hatua kuhakikisha dunia ya kidijitali inabaki mahali pa usalama na heshima sio tishio la kudhalilisha ustawi wako.”
Kwa upande wake, Geofrey Mbwana ambaye ni mshauri wa uhusiano, anaunga mkono kauli ya Dk Gwajima kuhusu tahadhari kwa wanawake, lakini pia anasisitiza elimu kwa jinsi zote.
“Ni kweli tunapaswa kuwa waangalifu. Lakini pia tuwafundishe vijana kuhusu ridhaa na heshima. Tatizo si teknolojia, tatizo ni matumizi mabaya ya teknolojia,” anasema.
Mbwana anasema jamii inapaswa kubadili mtazamo wake kwa waathirika…“Tunapocheka au kusambaza picha hizo kwa udadisi, tunakuwa sehemu ya tatizo,”.
Sababu wenza kutuma picha
Katika mahojiano ambayo Mwananchi ilifanya na watu kadhaa ilibainika sababu kuu zinazowasukuma wengi kutuma picha au video za maudhui ya utupu, ni pamoja na shinikizo la kiuhusiano, hofu ya kuachwa, kujaribu kudumisha ukaribu hasa katika uhusiano wa mbali, tamaa ya muda mfupi, kujiamini kupita kiasi, pamoja na ushawishi wa mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, wengi wao walikiri kuwa mara tu picha zinapotoka mikononi mwao, udhibiti hupotea na hapo ndipo hofu na majuto huanza pale mambo yanapoharibika katika uhusiano.
“Wakati mwingine ni shinikizo la moja kwa moja. Anakueleza kama unanipenda kweli nionyeshe.’ Unajikuta unatuma ili kulinda uhusiano. Unaogopa akihisi humwamini au humpendi vya kutosha ataondoka.”anasema Neema.
Mwingine ambaye hakutaka jina lake linukuliwe anasema: “Kwa upande wangu ilikuwa ni kujaribu kudumisha uhusiano wa mbali. Tulikuwa katika mikoa tofauti, mawasiliano mengi yalikuwa mtandaoni. Niliona kama ni njia ya kumfanya ajisikie karibu nami”.
Kwa upande wake, Asha Bilal anasema wakati mwingine wanawake hufanya hivyo kutaka kuthibitisha mvuto wao.
“Unataka aone bado anakutamani. Kuna presha ya mitandao pia unaona wengine wanafanya hivyo, unaona kama ni jambo la kawaida. Ni suala la kuamini kupita kiasi. Unamwamini mtu, unaona kama ni siri yenu tu. Huwezi kufikiria atakuja kugeuka adui,” anaeleza.
Jinsi ya kukabiliana na hali hii
Wataalamu wanashauri mtu aliyekumbwa na tukio la kusambazwa kwa picha zake, asijilaumu badala yake atambue kuwa yeye ni mwathirika.
“Ni muhimu kutafuta msaada wa kitaalamu kupitia ushauri nasaha ili kushughulikia mshtuko na kurejesha kujiamini. Pia, zungumza na watu unaowaamini ili usibebe mzigo peke yako,” anasema Dk Elitruda.
Kwa upande wake, mwanasaikolojia Amina anasema kupunguza matumizi ya mitandao kwa muda kunaweza kusaidia kulinda afya ya akili.