Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani ujumbe wa haki, usawa watawala

Dar/mikoani. Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yamefanyika kwa aina tofautitofauti nchini kwa wito wa haki na usawa ukitawala huku wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) wakikutana na vikwazo kila kona.

Bawacha walipanga kufanya maadhimisho yao kitaifa Musoma Mjini, Mkoa wa Mara lakini baadhi walijikuta mikononi mwa Jeshi la Polisi kwa misafara yao kuzuiwa kabla ya kufika Musoma, hawajaanza safari na wale waliokuwa wamefikia na kutaka kufanya maadhimisho wakitawanywa na mabomu ya machozi.

Wakati Bawacha wakikutana na vikwazo hivyo, Ngome ya Wanawake wa ACT-Wazalendo wao wamekutana Tunduru Mjini, mkoani Ruvuma kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya kongamano la kuwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha Oktoba 29, 2026.


Wenzao wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) walikusanyika kwa wingi ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa chama akiwemo Mwenyekiti wake, Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa na Katibu Mkuu, Salum Mwalimu wameshiriki na kutoa ujumbe mbalimbali.

Mbali na vyama hivyo, wakuu wa mikoa nchini, nao waliwaongoza wanawake waliojitokeza maeneo yaliyoandaliwa wakiwa kwenye sare, mabango yenye ujumbe wa kuhimiza malezi bora kwa watoto na ujumbe mwingine ukipinga ukatili wa kijinsia kama vile, ndoa za utotoni, vipigo kwa wanawake na unyanyapaa.

Katikati ya yote, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ujumbe wa siku hiyo akiwapongeza wanawake kwa kazi kubwa wanayoifanya akisema kamwe mwanamke huwa hakimbii majukumu, hubeba changamoto kwa ujasiri na hekima, kuzielekeza nguvu ya kuimarisha familia, jamii na Taifa.

Kauli mbiu ya maadhimisho hao kitaifa ni “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana, Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” huku kaulimbiu ya kimataifa ikiwa “Give to Gain,” kutoa ndio kupata.”

Katika ujumbe wa Rais Samia yeye amehimiza kuendeleza juhudi za kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki na usawa ili kuchochea maendeleo jumuishi ya Taifa.

Ameeleza siku hiyo ni muhimu kwa kutambua mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kaulimbiu hizo zinakumbusha maendeleo ya kweli ya jamii na Taifa yanajengwa katika misingi ya haki, usawa na ushirikishwaji.

“Kauli mbiu hizi zinatukumbusha kwamba maendeleo ya kweli ya jamii na Taifa letu yanajengwa katika msingi wa haki, usawa na ushirikishwaji, pamoja na moyo wa kujitoa, kushirikiana na kuwainua wengine,” amesema.

Rais Samia amesema katika maisha ya kila siku, mwanamke ana nafasi kubwa katika ustawi wa jamii na Taifa.

“Kwa asili, mwanamke ni mama, ni mlezi, ni kiongozi na ni mfariji wa familia, jamii na Taifa. Katika maisha ya kila siku, wanawake wanahimili kwa vitendo falsafa ya ‘Kutoa ndio Kupata’. Wanajitoa kwa familia zao, wanalea kizazi, wanahudumia jamii na wanachangia kwa namna mbalimbali maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Amesema hata wanapokumbana na changamoto, wanawake hubaki kuwa imara na hutumia hekima na uvumilivu kukabiliana nazo kwa manufaa ya jamii.

“Hata katika nyakati za changamoto, mwanamke hakimbii majukumu. Badala yake, hubeba changamoto hizo kwa ujasiri na hekima, kuzielekeza kuwa nguvu ya kuimarisha familia, jamii na Taifa. Mwanamke hulea familia, hulea jamii yake, hulea Taifa, hulea bara na hata hulea dunia,” amesema.

Rais Samia amesema mafanikio ya juhudi za wanawake yanategemea mshikamano wa wanawake na jamii kwa ujumla, akitoa wito kwa wanawake kote nchini kuendelea kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

“Ninawaalika wanawake wote wa Tanzania kuendelea kuwa sehemu ya juhudi hizi kujitolea kwa maendeleo na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii,” amesema.

Baadhi ya washiriki katika Siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya wanawake duniani, wakiwa katika maandamano.



Pia, ametoa wito kwa wanawake wa makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi wa sekta binafsi na umma, walimu, wahudumu wa afya, viongozi wa taasisi, wanahabari, wanasheria, wabunifu na wanafunzi kushirikiana katika kulinda afya ya mama na mtoto pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Amesisitiza kuwa kupitia mshikamano na vitendo vya kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake na watoto, jamii itaweza kuishi kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu ya “Give to Gain.”

Aidha, Rais Samia amewatakia wanawake wote nchini na duniani maadhimisho mema ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa duniani kote leo.

Polisi Mkoa wa Mara wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Bawacha waliokuwa wanajaribu kukusanyika kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Awali, Bawacha walipanga kufanya maadhimisho hayo kitaifa mjini Musoma leo Jumapili, Machi 8, 2026 kabla ya Jeshi la Polisi kuzuia maadhimisho hayo kwa maelezo kuwa kuyafanya ni ukiukwaji wa makusudi wa amri ya mahakama iliyokitaka chama hicho kisimamishe kufanya shughuli za kisiasa hadi kesi yao ya madai ya mgawanyo wa mali na upande wa chama hicho Zanzibar itakapomalizika mahakamani.

Wafuasi na wanachama wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha).



Mabomu hayo yamepigwa saa 5 asubuhi wakati wanawake hao wakitoka kwenye ibada ya Jumapili waliyoshiriki katika Kanisa Kuu Katoliki lililopo Mjini Musoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo.

Katika hekaheka hizo, Polisi iliwatia nguvuni 34 akiwemo Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Pamela Maasay.  

Awali, wanawake hao walisali katika kanisa hilo ambapo pamoja na mambo mengine waliombea umoja wao ili uweze kuwa na mshikamano daima.

Baada ya misa hiyo walitoka nje na kufanya mazungumzo ambapo wakiwa wanaendelea kiongozi mmoja wa kanisa aliwataka kutoka nje ya geti la kanisa.

“Tayari tumemaliza misa na mmewasilisha nia yenu, niwaombe mtoke nje ya geti ili muendelee na taratibu zingine kwani hapa sio eneo sahihi,” amesema kiongozi huyo.

Baada ya agizo hilo, wanawake hao walianza kutoka nje ya geti kwa maandamano huku wakiimba nyimbo mbalimbali za chama chao, lakini kabla hawajafika mbali walisimamishwa na polisi waliokuwa nje ya geti la kanisa.

Polisi hao waliwataka wanawake hao kutawanyika agizo ambalo hata hivyo hawakulitii.

Baada ya muda mfupi polisi walianza kurusha mabomu ya machozi na kuwatawanya huku kukiwa na taarifa ya baadhi yao kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi.

Mwenyekiti wa Bawacha Jimbo la Musoma Mjini, Renatha Rafael amesema zaidi ya watu 10 wamekamatwa katika purukushani hizo.

Amesema hivi sasa wanashughulikia utaratibu wa kuwatoa kituo cha polisi (bila kukitaja) wanachama hao waliokamatwa.

“Wamekamatwa zaidi ya watu 10, kuna wengine wamepoteza simu, wamepoteana kwa ujumla taharuki ni kubwa ila tunawasubiria wanasheria wa chama wapo njiani ili tuendelee na mchakato wa kuwatoa wenzetu Polisi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na kadhia hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amekiri kuwepo kwa tukio hilo ingawa amesema mabomu yaliyorushwa ni machache na hivi sasa hali ni shwari mjini Musoma.

Kuhusu watu waliokamatwa Kamanda Lutumo amesema atatoa taarifa baadaye.

“Mabomu yamerushwa kama mawili tu lakini kuhusu watu kukamatwa hebu nipe muda ila kikubwa ni kwamba Musoma hali ni shwari tunaendelea na majukumu yetu kama kawaida,” amesema.

Awali, Bawacha walipanga kutumia viwanja vya matumaini kwa vijana mjini Musoma kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Hata hivyo, siku mbili kabla ya maadhimisho hayo uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma ambao ndio wanaomiliki uwanja huo waliwaandikia barua kueleza kusitisha matumizi ya uwanja huo kutokana na maelekezo waliyopewa na vyombo vya usalama.

Baadaye Chadema kupitia Brenda Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho ilitoa taarifa kwa umma ikisema kimeungana na wanawake wa Tanzania na dunia kuadhimisha siku hiyo ya wanawake, kikituma salamu za pongezi huku kikisisitiza umuhimu wa haki na usawa kwa wanawake katika jamii.

Kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema, haki na usawa, ukitoa umepata, chukua hatua, bila shaka kauli mbiu hiyo itachochea ari na nguvu zaidi katika kuwaunganisha wanawake wa Tanzania ili kudai haki huku wakitimiza wajibu wao kama raia wazalendo wanaolipenda Taifa lao,”

Chadema imesema maadhimisho ya wanawake wa chama hicho yamefanyika katika mazingira tofauti na yaliyotarajiwa baada ya baadhi ya wanachama wa Bawacha kuzuiwa au kukamatwa katika maeneo mbalimbali walipokuwa wakielekea Musoma.

Taarifa ya chama hicho ilidai baadhi ya wanawake hao walikamatwa wakiwa ndani ya mabasi na kupelekwa katika vituo vya polisi huku wengine wakirudishwa walipotoka walipokuwa wakisafiri kuelekea Musoma.

Wafuasi na wanachama wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha).



Ilidai wengine walizuiliwa hata kabla ya kuanza safari wakidaiwa kukiuka sheria inayozuia kusafiri kutoka eneo moja kwenda lingine. Taarifa hiyo imedai kuwa miongoni mwa wanawake hao wapo wajawazito, wanaonyonyesha na wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya wanawake waliokuwa wakielekea Musoma waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi huku wengine wakinyimwa dhamana.

“Kamatakamata hiyo ilianza Ijumaa Machi 6, 2026 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Pwani, Morogoro, Geita, Simiyu, Singida, Iringa na Mara,” ilidai taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Chadema pia imelitaka Jeshi la Polisi kuwaachia wanawake hao bila masharti ili waweze kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani wakiwa uraiani.

Mzee wa Ubwabwa akihutubia mamia ya wanawake wa Chaumma amewataka kudumisha upendo na kukijenga chama hicho kifike mbali.

“Nawashukuru sana kwa jinsi mlivyojitokeza kwenye ukumbi huu kuadhimisha siku ya wanawake, nawapongeza sana, huko nyuma tulikuwa hatufanyi sasa chama kimepanuka nawaomba mwakani mjitokeze zaidi watu waone Chaumma kinakuwa.


“Ninachowaomba wanawake muishi kwa upendo na kuendelea na moyo wa kujitolea na kushikamana ili chama chetu kifike mbali,” amesema Rungwe.

Akizungumzia kauli mbiu ya siku ya wanawake, Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Bara, Devotha Minja amesema ni kaulimbiu inaakisi chama chao kwani waliwekeza kwa wanawake na walipata kupitia uchaguzi 2025.

Devotha ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum amesema uamuzi wa Chaumma kuwekeza kwa wanawake, ifikapo mwaka 2030 idadi yao kwenye uongozi itaongezeka akiiomba chama chake kuendelea kuwalea.

Naye Mwenyekiti wa Ngome ya ACT Wazalendo, Janeth Rite akizungumza katika kongamano hilo amesema ngome hiyo itaongoza mapambano ya kupigania Katiba Mpya na Tume Huru ya Taifa Uchaguzi.

“Ngome ya wanawake inakipongeza chama kwa ushindi tulioupata katika Mahakama ya Afrika ambapo Serikali imetakiwa kufanya mabadiliko ya Katiba ili matokeo ya urais yapingwe mahakamani,” amedai Janeth.

Mkoa wa Mara wanawake waliadhimisha wilayani Serengeti ambapo mkuu wa mkoa huo, Kanali Evans Mtambi amesema vita dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ni ya jamii nzima hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anashiriki katika vita hiyo.

Amesema kuendelea kuwepo kwa mila hizo ndani ya mkoa huo ni ishara mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia bado yanatakiwa kuendelea ili kuwapa nafasi na fursa wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Baadhi ya wanawake wamesema vita dhidi ya ukatili wa kijinsia ni jukumu la kila mwana jamii huku wakiomba nguvu zaidi zielekezwe maeneo ya vijijini.

“Matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanatokea vijijini na hakuna hatua zinazochukuliwa hali hii inawaathiri sana wanawake na watoto hivyo niwaombe wadau wote sasa uelekeo uwe ni vijijini,” amesema Rhobi Marwa.

Amina Malumbo amesema mafanikio yalioanza kuonekana yanapaswa kuendlezwa na hatimaye kuondokana na changamoto hiyo ndani ya jamii mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian akiwaongoza wanawake wa mkoa huo katika Uwanja wa Shule ya Msingi Boma ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akihamasisha wanawake kutumia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri ili kujikwamua kiuchumi.

Balozi Burian amesema maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kusisitiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana ili kufikia maendeleo jumuishi ya Taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga akihutubia maelfu ya wanawake  kwenye kilele cha wiki ya wanawake  kimkoa katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga



Mmoja wa washiriki wa maadhimisho hayo, Sofia Juma amesema ipo haja ya jamii kuungana kupinga vitendo vya ukatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa wanawake na watoto ili kuhakikisha vitendo hivyo kinapungua kama sio kuisha kabisha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amewataka wazazi na walezi kuongeza malezi kwa watoto wao na kuwalea katika maadili ya dini zao na kuwafundisha yaliyokuwa mema na siyo kuwalea Kizungu kwa kuwaachia simu na luninga ambapo mtoto anaweza kuangalia chochote anachokitaka.

Zainabu amesema hayo katika Kijiji cha Mbekenyera yalipofanyika maadhimisho kimkoa akisisitiza, “Baba na mama tuna wajibu wa kulea watoto wetu wa kike na kiume na familia, na tujitahidi kuacha malezi ya Kizungu kwa kuwaachia simu wachezee au kuangalia luninga wao wenyewe.”