Dar es Salaam. Chama cha Umoja wa Makandarasi na Watoa Huduma Shirikishi Tanzania (Tucasa) kinapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa Sheria ya Malipo (Sopa) kwa sekta ya ujenzi ili kulinda haki za makandarasi.
Chama hicho kimesema sheria kama hiyo, inayotumika katika nchi kama Australia, Uingereza, Singapore na Malaysia, huweka muda wa kisheria wa malipo lengo ni kuhakikisha mtiririko thabiti wa fedha katika mnyororo mzima wa sekta ya ujenzi na kuhakikisha miradi inaendelea bila kuvurugwa na matatizo ya kifedha.
Chama kimesema katika hizo nchi gharama za ujenzi zilishuka kwa kiwango kikubwa baada ya kutumika kwa sheria hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya chama mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa Tucasa, Samuel Marwa amesema chama kinatambua kauli za viongozi akiwamo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ambazo zimethibitisha dhamira ya Serikali ya kujenga na kuimarisha uwezo wa kampuni ya ndani katika sekta ya ujenzi.
“Kauli zinazofanana na hizo pia zimetolewa na viongozi wa mikoa, wakiwamo Mkuu wa Mkoa wa Njombe Januari 28, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Februari 3, 2026, ambao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa ndani katika sekta ya ujenzi.
“Viongozi hao pia walieleza mwelekeo huo wa sera unatokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kuhakikisha kampuni za ndani zanachukua nafasi ya mbele katika ujenzi wa miundombinu na maendeleo ya uchumi wa taifa,” amesema.
Amesema msimamo wa Serikali umekuja wakati muafaka na una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi kwamba, kuzipa kipaumbele kampuni za ndani zenye uwezo kunasaidia kujenga uwezo wa kitaifa, kukuza ujuzi na utaalamu wa ndani, kuhakikisha mitaji inayowekezwa inabaki.
Ikirejewa kauli ya Dk Nchemba Februari 15, 2026 mkoani Tanga alipokuwa akizungumza na wadau wanaohusika na mradi wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP).
Mradi huo wa bomba la mafuta, wenye urefu wa takribani kilomita 1,443 kutoka maeneo ya uzalishaji mafuta karibu na Ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania, ni uwekezaji mkubwa wa kikanda wa miundombinu.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuchunguza tuhuma za baadhi ya kampuni za kigeni zinazosajili kampuni kwa majina ya Watanzania ili kupata zabuni za Serikali kwa njia isiyo ya haki.
Alieleza vitendo hivyo vinaharibu ushindani wa haki na kupunguza fursa kwa makampuni halali ya ndani. Aidha alionya kuwa kampuni yatakayobainika kujihusisha na vitendo hivyo yanaweza kuzuiwa kushiriki katika zabuni za Serikali siku zijazo.
“Tucasa inaunga mkono juhudi hizi na kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa wazi na wa haki wa sera zilizopo za maudhui ya ndani (local content) pamoja na taratibu za ununuzi wa umma,”inaeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Tucasa, zipo changamoto za kimuundo ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikiathiri ukuaji wa makandarasi wa ndani, yaani ucheleweshaji wa malipo kwa kazi zilizokamilika na kuthibitishwa.
“Makandarasi wengi wa ndani hufanya kazi kwa kutumia akiba ndogo ya kifedha na upatikanaji mdogo wa mikopo nafuu. Hali ya kucheleweshwa kwa malipo ya hati za kazi (IPCs) kwa muda mrefu huwafanya makandarasi kulazimika kugharamia utekelezaji wa miradi kwa mikopo yenye riba kubwa.
“Hali hii hudhoofisha uwezo wao wa kifedha, huongeza gharama za miradi, na kupunguza uwezo wao wa kushiriki kikamilifu katika miradi mingine ya miundombinu. Katika baadhi ya matukio, hata kampuni zenye uwezo mzuri hukabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha kutokana na ucheleweshaji wa malipo, na mengine hata kuishia kufilisika na kufungwa,” inaeleza Tucasa.
Katika hilo chama kinaishauri Serikali kuharakisha utekelezaji kamili wa mifumo salama ya malipo kidjitali ili kufanikisha manufaa yaliyokusudiwa katika mfumo wa ununuzi ya umma.
Hata hivyo, mifumo ya kidijitali huongeza uwazi na ufuatiliaji, uzoefu wa kimataifa unaonesha kuwa maboresho ya kudumu katika utaratibu wa malipo mara nyingi huhitaji pia kuwepo kwa mfumo wa kisheria unaolazimisha utekelezaji wa wajibu wa malipo.
Tucasa inaamini kuimarishwa kwa usalama wa malipo kutachangia kwa kiasi kikubwa uimara wa wakandarasi wa ndani, kupunguza hatari za kifedha katika sekta ya ujenzi na kusaidia kufikiwa kwa lengo pana la kujenga sekta imara na shindani ya ujenzi inayomilikiwa na kuendeshwa na wazawa.