Marietha anavyojitegemea kupitia kazi ya bodaboda

Dar es Salaam. Akiwa amekulia katika mazingira ya kawaida ya kifamilia mkoani Manyara, alilazimika kuagana na nyumbani kwao, ndugu na marafiki, akibeba matumaini moyoni, akiamini kuwa jiji kubwa la Dar es Salaam lingeweza kufungua ukurasa mpya wa maisha yake.

Hakukuwa na uhakika wa kazi wala ndugu wa karibu wa kumtegemea, kilichomsukuma ni shauku ya kujitegemea na imani kuwa mafanikio hayaji kwa kusubiri bali kwa kuthubutu.

Alipofika Dar es Salaam, hakukutana na ‘barabara za dhahabu’ kama wengi wanavyodhani, bali alikuta ushindani, gharama za maisha na mapambano ya kila siku ya kuisaka shilingi.

Lakini ndani ya changamoto hizo ndipo alipoanza kuijenga hadithi yake ya kuwa mmoja wa madereva wachache wa bodaboda wanawake katika eneo la Kibada, Wilaya ya Kigamboni.

Leo, Marietha Gurahe si tu jina, ni miongoni mwa waendesha bodaboda wa Kibada ambaye ni ishara ya mwanamke aliyethubutu kuvuka mipaka ya hofu na kuandika upya simulizi ya maisha yake.

Safari yake kutoka Manyara hadi pwani ya Bahari ya Hindi ni mwanzo wa mapambano yaliyomgeuza kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wanaotamani kujitegemea.

Anasimulia kuwa wazo la kuwa dereva wa bodaboda lilianza mwaka 2022, na halikuja kwa bahati mbaya, lilizaliwa ndani ya tafakari nzito ya maisha. Awali alikuwa akifanya kazi nyingine, lakini mambo yakabadilika. Fursa zikapungua, kipato kikawa hakitoshi na hitaji la kujitegemea likawa kubwa zaidi.

“Siku moja nililala nikawaza sana kuhusu maisha yangu, nikajiuliza, nitaendelea kusubiri au nitachukua hatua kwa kufanya kazi binafsi na si ya kumtegemea mtu?” swali alilojiuliza Marietha.

Anasema asubuhi iliyofuata aliamka na uamuzi wa kuanza kwenda kijiweni na kuomba pikipiki za watu ili ajifunze kuendesha, kwa kuwa alikuwa na ujuzi wa kuendesha pikipiki tangu akiwa Manyara, japokuwa hakuwa vizuri sana.

Mwanadada Marietha Gurahe akiwa amkekaa juu ya bodaboda yake.



“Nilijifunza kuendesha pikipiki si kwa ajili ya kufanyia kazi, lakini nilivyochukua uamuzi wa kujiajiri nilihitaji ujasiri wa hali ya juu ili kutumia fursa ambayo ingenitoa kimaisha,” anasema Marietha.

Anasema baada ya siku kadhaa alinunua pikipiki iliyokuwa ya mkataba kutoka kwa mmoja wa dereva wa bodaboda aliyemfahamu, na alimuuzia kwa Sh1.5 milioni.

Hatua hiyo anasema ilikuwa muhimu kwa sababu ilimpa uhuru zaidi wa kupanga mapato na matumizi yake.

“Nilipopata nafasi ya kununua pikipiki, nilijisikia nimepiga hatua kubwa. Nilijiambia moyoni sasa najua nafanya kazi kwa ajili yangu mwenyewe na wadogo zangu nyumbani,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kuwa mwanzoni hakujua vizuri utunzaji wa pikipiki kwa kuchelewa kufanya matengenezo kwa wakati, jambo lililosababisha pikipiki yake kuharibika mara kwa mara.

“Nilikuwa najua kuendesha tu, si kufanya matengenezo ya mara kwa mara. Hali hii ilinipa somo, sasa najua kuwa matengenezo ni sehemu ya kazi. Usipoyazingatia, utapata hasara,” anasema.

Kutokana na hali hiyo alijikuta anaitumia kwa muda mchache, hivyo aliamua kuiuza na kuingia kwenye pikipiki za mkataba kama wanavyofanya wanaume.

Anasema ilikuwa ngumu kuaminika kutokana na jinsia yake, hivyo alifunga mkanda kwa kumuomba mmoja wa wateja wake ambaye ni mstaafu akubali kuwekeza kwenye usafiri wa pikipiki.

“Nilimshawishi huyo mzee. Aliniambia ataongea na mkewe, akikubali atafanyia kazi. Baada ya siku mbili alinipigia simu kuwa ombi langu limekubaliwa, niende Kariakoo kuchagua pikipiki,” anasema.

Anasema baada ya kukamilika kwa vibali vyote aliingia rasmi kwenye mkataba ambao alitakiwa kuutumikia miezi 13 kwa kupeleka Sh10,000 kila siku, na alifanikiwa kumaliza ndani ya miezi 10.

Marietha anasema alikuwa anaulizwa amewezaje kumaliza mkataba haraka tofauti na wanaume; jibu lake lilikuwa moja ni kujiwekea malengo kwa kupunguza vitu ambavyo si vya umuhimu.

“Swali hili nimekuwa nikiulizwa na wanaume kwa kuwa nakaa nao kijiweni. Niliwaambia pesa zao zina matumizi mengi tofauti na mimi, na nimeweka malengo, situmii pesa kwa vitu ambavyo si vya umuhimu.”

Anasema kwenye kijiwe amekuwa akishuhudia baadhi ya madereva wakipakiza wanawake bure na kusahau kupeleka hesabu ya tajiri kila siku, hivyo wamekuwa wakichochea hasira za kuchukuliwa pikipiki.

Anasema hatua yake ya kuendesha pikipiki haikupokelewa kwa shangwe na kila mtu. Wapo waliomcheka, waliomwambia haiwezekani mwanamke kufanya kazi ya bodaboda na wengine walimtazama kwa mshangao kana kwamba amevunja sheria.

“Walisema hii kazi si ya wanawake, utashindwa, utaangusha abiria, lakini mimi nilijiamini. Nilijua kama najua kuendesha, basi naweza,” anasema.

Siku za mwanzo hazikuwa rahisi. Alisimama kituoni akisubiri abiria, lakini wengi walimkwepa, hasa wanaume walionekana kuwa na mashaka zaidi.

“Kuna waliokataa waziwazi, walisema hawawezi kupanda kwa mwanamke. Wapo walioniangalia tu wakaondoka, na wengine walikubali lakini waliendesha wenyewe hadi wanapokwenda, kisha kunilipa na kunirudishia pikipiki wakati wa kurudi,” anasema Marietha.

Anasema hali hiyo haikumkatisha tamaa, kwani aliamini muda na uthabiti vingebadili mtazamo wa watu na kuweza kumuamini kama wanavyoaminiwa wanaume.

Anasema kazi ya bodaboda si rahisi kwa mwanaume wala mwanamke. Kuna hatari za ajali, wizi na wakati mwingine vitisho vya usalama. Kwa mwanamke, changamoto huongezeka kwa sababu ya mitazamo ya kijinsia.

Anasema wakati mwingine hukutana na maneno ya dhihaka au mizaha isiyofaa, lakini amejifunza kuvumilia na kujibu kwa staha au kupuuza.

“Kuna siku nilipakia mwanaume. Tulipofika nyumbani kwake, mkewe alivyotuona hakutaka kuamini kama mimi ni bodaboda, bali alimwambia mumewe mimi ni mpenzi wake,” anasema.

Anasema inawezekana ilikuwa utani au ukweli hajui, kwa sababu mama huyo alimweleza mumewe kulikuwa na bodaboda wanaume, kwa nini amchague yeye.

Mbali na hilo, anasema abiria mwingine aliomba kushushwa hatua chache kabla ya kufika nyumbani kwake, akihofia kuhojiwa kwa kukubali kupakizwa na mwanamke, hivyo majibu yangetolewa kuwa ni mpenzi.

Changamoto zote hizo anasema ameishi nazo hadi sasa, lakini anaamini ni hali ya kawaida kwenye kazi hiyo, huku baadhi ya wanawake wakimkataa kwa madai kuwa atawaangusha.

“Unaita abiria, akifika anauliza dereva yuko wapi. Nikijibu ni mimi, wanakataa, wanasema hawawezi kuendeshwa na mwanamke. Kiukweli huwa najisikia vibaya, lakini sijawahi kukata tamaa. Najua ipo siku wataniamini,” anasema Marietha.

Licha ya kuwepo kwa changamoto zote hizo, anasema hajawahi kukutana na tukio kubwa la kumkatisha tamaa kama kushambuliwa au kuumizwa, lakini anaelewa hatari ipo na hutoa kipaumbele cha usalama kwanza.

“Wapo wateja wanaokuja kwa lengo baya, lakini kujiepusha nao huwa nawahi kuwashusha na kuwasamehe nauli zao kutokana na dalili wanazoanza kuonesha tunapofika maeneo walipotaka niwapeleke,” anasema.

Anasema wapo ambao hukataliwa na bodaboda wanaume kwa kuwa na nauli ndogo, anapojitolea kuwabeba, wakifika eneo la kushuka hugeuza kibao cha kutomlipa na kutishia kumpiga.

Kujenga imani kwa vitendo

Anasema kidogo kidogo hali ilianza kubadilika. Abiria wachache waliothubutu kupanda pikipiki yake walipata huduma nzuri na salama kila walipofika walikokwenda bila tatizo, walimpongeza na wengine wakaanza kumtafuta.

“Nilihakikisha nafanya kazi kwa umakini. Sitaki mtu aseme mwanamke ameangusha au amechelewesha,” anasema.

Kadri siku zilivyopita, anasema wateja walianza kumzoea, heshima ikaanza kujengeka. Wale waliokuwa wakimcheka wakaanza kumkubali, na sasa ana wateja wa kudumu wanaomwamini.

“Ukifanya kazi kwa uaminifu na uvumilivu, watu wanakuona na wanajua huyu yupo makini,” anasema.

Anasema akiwa katika harakati za kazi alipata ajali ya mguu kutokana na uzembe uliofanywa na dereva wa bajaji aliyekuwa akigeuza eneo ambalo halikuwa sahihi jirani na taa za Mjimwema, na yeye kujigonga na kuvunjika mguu.

“Nilipata ajali nikavunjika mguu. Nilikaa nyumbani zaidi ya miezi minne. Hiki kilikuwa kipindi kigumu kwangu, lakini namshukuru Mungu akiba yangu ilikuwa inanisaidia kujihudumia,” anasema.

Kabla ya kupata ajali alikuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba ya Sh20,000 kila siku, na ili kufanikisha hilo alikuwa anahakikisha kwa siku anaingiza Sh40,000 kwa kugawa pesa ya mafuta, kula na akiba.

Kutokana na kuwa na akiba ya kutosha, hata familia yake haikujua kama amepata ajali, lakini mwisho wa siku aliwaambia kinachoendelea, na wao walimkumbushia kuwa kazi yake inahatarisha maisha.

Anasema kupitia kazi hiyo ameeza kujikimu na kusaidia familia yake kwa kusomesha wadogo zake wawili, kwani si kazi ya aibu bali ni kazi halali kama zilivyo nyingine.

“Cha muhimu ni kipato halali. Siangalii nani anasema nini. Maisha ni yangu na nimefanikiwa kusaidia familia yangu, na siku si nyingi nitaanza ujenzi,” anasema.

Anaamini kuwa jamii inapaswa kubadili mtazamo kuhusu kazi zinazodhaniwa kuwa za wanaume au wanawake pekee. Kwa mtazamo wake, uwezo hauamuliwi na jinsia bali na dhamira ya mtu.