Pamoja na kufuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Mbeya City imefuta gundu katika Uwanja wa Sokoine kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Bandari FC inayoshiriki First League.
Tangu kuanza msimu huu Mbeya City ilikuwa haijaonja ushindi ikicheza uwanja wa nyumbani, Sokoine na leo imeweka rekodi ya kwanza kwa kuwafumua wapinzani wao hao na kuwatibulia rekodi.
Iko hivi Bandari inayonolewa na nyota wa zamani wa Yanga, Toto Africans na Ndanda FC, Omega Seme katika msimu huu ilikuwa haijapoteza mchezo wowote wa mashindano huku ikijivunia kuifunga KMC kwa penalti 4-3 katika Kombe la Shirikisho na kuitoa hatua ya 32.
Mbeya City kati ya michezo 15 iliyocheza Ligi Kuu Bara, sita imekuwa nyumbani katika Uwanja wa Sokoine ikipata sare tatu na kupoteza tatu ikishika nafasi ya 14 kwa pointi 13.
Kwa upande wa Bandari FC, katika michezo minane ya First League haijapoteza mchezo wowote ikishinda sita na sare mbili ikiwa kinara katika kundi B kwa pointi 20, na sasa safari yao ya matumaini Kombe la Shirikisho imeishia Sokoine.
Katika mchezo huo ambao ulionekana kuwa wa ushindani, mabao mawili yalifungwa na Vitalis Mayanga huku la tatu likijazwa wavuni na Lifati Hamis, japokuwa kipa Beno Kakolonya hataisahau Bandari kwa misukosuko waliyompa kuokoa hatari nyingi.
Baada ya mchezo huo, Mbeya City itabaki Sokoine kuisubiri Singida Black Stars katika mchezo wa Ligi Kuu wa kiporo, huku Bandari ikiwavaa Nyumbu walio nafasi ya pili katika First League kwa pointi 15 na michezo nane.
Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mecky Maxime amesema walihitaji ushindi ili kurejesha ari mpya kikosini na kwamba walicheza kwa kuwasoma wapinzani na kuwanyima kugusa mpira mara nyingi mpango ambao uliwapa ushindi.
“Tuliwachezea sana pasi kuwakimbiza uwanjani. Niwapongeze vijana wangu kwa kazi nzuri na leo tumeondoa gundu kwenye uwanja huu. Walionyesha ushindani ila tuliwazidi,” amesema Maxime.
Kocha wa Bandari FC, Omega amezitakia safari njema timu zote zilizofuzu hatua inayofuata akieleza kuwa hawajaondoka kinyonge kwani walionyesha upinzani kwa timu za Ligi Kuu.
“Tulitamani kufika mbali, lakini hata hapa tunashukuru. Tuliwatoa KMC ya Ligi Kuu na tunatolewa na timu ya Ligi kuu. Niwashukuru vijana na sasa tunaenda kujipanga upya na ligi,” amesema Seme.