Michango mashuleni kikwazo kwa watoto wenye mazingira magumu

Dodoma. Walezi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wametaja wingi wa michango ya wanafunzi shuleni kuwa inawakwamisha katika kufikia malengo na kuomba Serikali iwasaidie kutoa mwongozo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Machi 8,2026 na Mkurugenzi wa Kituo cha kulea watoto yatima na wenye mahitaji maalumu cha Rahman Day Care Center,  Rukia Abllah wakati akipokea vyakula na mahitaji mengine kwa ajili ya watoto.

Mahitaji hayo ikiwamo vyakula, mafuta, vinywaji, nguo na taulo za kike vimetolewa na wanawake watumishi kutoka mamlaka ya Serikali mtandao (e-GA) katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Rukia amesema wamekuwa wakikutana na mtihani mgumu wa kuwalipia watoto michango ambayo wanadaiwa shuleni kila wakati, hivyo wanajikuta kwenye wakati mgumu kwani wanaishi na watoto ambao wengi huwapokea kutoka ustawi wa Jamii.

“Hawa watoto ni mali ya Serikali, sisi tunawapokea kutoka ustawi wa jamii na kuanza kuishi nao, tunawapeleka shule na wengine kuwapa mafunzo ya ufundi, leo tukidaiwa michango inatukatisha tamaa,” amesema Rukia.

Mkurugenzi huyo ameomba Serikali kuweka mwongozo kwa wakuu wa shule ili wanafunzi wanaotoka mtaani ambao wanatambuliwa kupitia ustawi wa jamii wasidaiwe michango.

Akizungumzia kituo hicho, amesema hadi sasa wamekuwa na watoto 120 na kwenye mafanikio yao wanajivunia uwepo wa vijana waliowalea ambao mmoja amemaliza shahada ya udaktari wa binadamu alioupata Sudani kwa ufadhili.

Kituo cha Rahman kilianzishwa 1998 kama sehemu ya mkusanyiko wa wanawake wa Kiislamu waliolenga kusaidiana, lakini mwisho wakaanzisha kitu ambacho kimekuwa miongoni mwa vituo vikubwa jijini Dodoma na kinachukua watoto wa dini zote.

Katibu wa kituo hicho, Abdallah Said amesema kwa sasa wanakabiliwa na wingi wa watoto lakini eneo wanamoishi limekuwa dogo jambo ambalo limesababisha watafute eneo lingine ili kukidhi mahitaji.

Akizungumzia mchango huo, Meneja Mawasiliano Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Subira Kaswaga amesema vifaa vilivyotolewa ni sehemu ya mchango wa mamlaka na michango binafsi kwa wanawake.

Kiswaga amesema e-GA imefanya uchunguzi wake katika vituo mbalimbali, ilibaini kuwepo kwa mahitaji muhimu kwa watoto hao ili waweze kuwasaidia kufikia ndoto zao.

“Tulipita katika vituo mbalimbali lakini tumeona kinamahitaji makubwa kuliko vingine, lakini wenzetu wa Dar es Salaam leo wamefanya hivi katika moja ya kituo pale Kibaha mkoani Pwani,” amesema Kiswaga.