Musoma. Polisi Mkoa wa Mara wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi na wanachama wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), waliokuwa wanajaribu kukusanyika kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Awali, Bawacha walipanga kufanya maadhimisho hayo kitaifa mjini Musoma leo Jumapili, Machi 8, 2026 kabla ya Jeshi la Polisi kuzuia maadhimisho hayo kwa maelezo kuwa kuyafanya ni ukiukwaji wa makusudi wa amri ya mahakama.
Mabomu hayo yamepigwa saa 5 asubuhi wakati wanawake hao wakitoka kwenye ibada ya Jumapili waliyoshiriki katika Kanisa Kuu Katoliki lililopo Mjini Musoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Awali, wanawake hao walisali katika kanisa hilo ambapo pamoja na mambo mengine waliombea umoja wao ili uweze kuwa na mshikamano daima.
Baada ya misa hiyo walitoka nje na kufanya mazungumzo ambapo wakiwa wanaendelea kiongozi mmoja wa kanisa aliwataka kutoka nje ya geti la kanisa.
“Tayari tumemaliza misa na mmewasilisha nia yenu, niwaombe mtoke nje ya geti ili muendelee na taratibu zingine kwani hapa sio eneo sahihi,” alisema kiongozi huyo.
Wafuasi na wanachama wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha).
Baada ya agizo hilo, wanawake hao walianza kutoka nje ya geti kwa maandamano huku wakiimba nyimbo mbalimbali za chama chao, lakini kabla hawajafika mbali walisimamishwa na polisi waliokuwa nje ya geti la kanisa.
Polisi hao waliwataka wanawake hao kutawanyika agizo ambalo hata hivyo hawakulitii.
Baada ya muda mfupi polisi walianza kurusha mabomu ya machozi na kuwatawanya huku kukiwa na taarifa ya baadhi yao kukamatwa na kupelekwa kituo cha polisi.
Mwenyekiti wa Bawacha Jimbo la Musoma Mjini, Renatha Rafael amesema zaidi ya watu 10 wamekamatwa katika purukushani hizo.
Amesema hivi sasa wanashughulikia utaratibu wa kuwatoa kituo cha polisi (bila kukitaja) wanachama hao waliokamatwa.
“Wamekamatwa zaidi ya watu 10, kuna wengine wamepoteza simu, wamepoteana kwa ujumla taharuki ni kubwa ila tunawasubiria wanasheria wa chama wapo njiani ili tuendelee na mchakato wa kuwatoa wenzetu Polisi,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na kadhia hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara (RPC), Pius Lutumo amekiri kuwepo kwa tukio hilo ingawa amesema mabomu yaliyorushwa ni machache na hivi sasa hali ni shwari mjini Musoma.
Kuhusu watu waliokamatwa Kamanda Lutumo amesema atatoa taarifa baadaye.
Wafuasi na wanachama wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha).
“Mabomu yamerushwa kama mawili tu lakini kuhusu watu kukamatwa hebu nipe muda ila kikubwa ni kwamba Musoma hali ni shwari tunaendelea na majukumu yetu kama kawaida,” amesema.
Awali, Bawacha walipanga kutumia viwanja vya matumaini kwa vijana mjini Musoma kwa ajili ya maadhimisho hayo.
Hata hivyo, siku mbili kabla ya maadhimisho hayo uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma ambao ndio wanaomiliki uwanja huo waliwaandikia barua kueleza kusitisha matumizi ya uwanja huo kutokana na maelekezo waliyopewa na vyombo vya usalama.
Endelea kufuatilia Mwananchi