Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa amewataka wanawake ndani ya chama hicho kudumisha upendo na kukijenga chama hicho kifike mbali.
Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu ametoa mwelekeo wa chama hicho ikiwamo kuanza operesheni ya Katiba mpya itakayolenga kutoa elimu ya katiba kwa wananchi.
Akizungumza leo Jumapili Machi 8, 2026 katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026, Rungwe amewashukuru wanawake hao kwa kuendelea kukijenga chama hicho.
“Nawahukuru sana kwa jinsi mlivyojitokeza kwenye ukumbi huu kuadhimisha Siku ya Wanawake, nawapongeza sana. Huko nyuma tulikuwa hatufanyi, sasa chama kimepanuka na nawaomba mwakani mjitokeze zaidi watu waone Chaumma kinakuwa.
“Ninachowaomba wanawake muishi kwa upendo na kuendelea na moyo wa kujitolea na kushikamana ili chama chetu kifike mbali,” amesema Rungwe.
Pia amewasifu wanawake wa chama hicho kwa kujitolea kwa ajili ya chama, akisisitiza kufurahishwa na maandalizi ya mkutano huo.
Akizungumzia maadhimisho ya kamati kuu ya chama hicho kilichoketi Machi 4, 2026 kuhusu mwelekeo wa siasa ndani ya chama hicho, Mwalimu amesema chama hicho kitaanza operesheni maalumu ya Katiba mpya ya kuwaandaa wananchi kupigania katiba mpya.
“Pia, tutakuwa na uongozi kamili ngazi zote kuziba mapengo ya uongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya chama chetu na tutahakikisha viongozi wa chama chetu kwenye vyombo vya uamuzi wanapigania masilahi ya wananchi,” amesema.
Mwalimu ameeleza pia chama hicho kuendelea kutafuta rasilimali kwa ajili ya kujiendesha pamoja na kuanzisha programu ya ‘Chaumma Family’ kwa lengo la wanachama kusaidiana.
Mbali na hayo amesema chama hicho kitaanzisha programu maalum ya mafunzo kuwajengea uwezo viongozi wa chama hicho kuongoza kwa weledi.
Akizungumzia kaulimbiu ya Siku ya Wanawake, Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Bara, Devotha Minja, amesema kaulimbiu ya “Kutoa ni kupata’, wekeza kwa mwanamke kwa manufaa ya Taifa,” inaakisi chama chao kwani waliwekeza kwa wanawake na walipata kupitia uchaguzi wa 2025.
Amesema uamuzi wa Chaumma kuwekeza kwa wanawake ni kwamba ifikapo 2030 idadi yao kwenye uongozi itaongezeka, akikiomba chama chake kuendelea kuwalea.
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa katikati akiwa na viongozi wa Chaumma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chaumma Mkoa wa Dar es Salaam, Husna Masoud, akitoa salamu katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wanawake Chaumma Taifa, amesema siku hiyo ni mahususi kuamsha harakati za wanawake kupigania haki na maendeleo.
Akidokeza kuhusu uchaguzi mkuu, amesema baada ya uchaguzi kuisha wanaendelea kujiimarisha na wale wanaosema chama hicho kimekufa baada ya tukio hilo wafahamu uhai wa chama umeanza.
Ametoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za kuwapa wanawake kipaumbele katika kila sekta kwa kuwa wanawake bado wapo nyuma katika sekta mbalimbali.
“Tunataka awakumbuke wanawake wote wa Tanzania kwa kuwaongezea fursa kwenye elimu, mikopo, kuwapa nafasi katika vyombo vya maamuzi,” amesema.
Naye Katibu wa Vijana Taifa Chaumma, Mkola Abubakar amesema siasa ni nyenzo ya maamuzi na bila wanawake sera zinazogusa afya, elimu na uchumi wa familia zinakosa uhalisia.
“Kitengo cha Wanawake Chaumma (Kiwacha) kinasisitiza ushiriki wa mwanamke kwenye siasa unapaswa kuvuka mipaka ya uhamasishaji wa kina mama na kuingia kwenye uongozi wa kutoa dira,” amesema.
Ameeleza chama hicho kimeanza mchakato wa kuandaa wanawake wenye uwezo, maadili na uadilifu ili kushika nafasi za uongozi, lengo ni kuhakikisha uwiano wa kijinsia unazingatiwa kulingana na katiba ya chama na miongozo.
“Chama kimeanza mchakato wa kuandaa wanawake wenye uwezo, maadili na uadilifu ili kushika nafasi za uongozi, lengo ni kuhakikisha uwiano wa kijinsia unazingatiwa kulingana na katiba ya chama na miongozo ya kitaifa,” amesema.
Kwa niaba ya wanawake wabunge Chaumma, Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambat amesema chama cha siasa kinapofanya siasa lengo lake kuu ni kushika dola.
Amesema licha ya wabunge wao kuwa wachache bungeni (wako watatu), kazi wanayoifanya inaonekana kana kwamba wao ni wengi kuliko idadi yao halisi.
“Tutaendelea kusimama pamoja na changamoto za kina mama ili kuhakikisha sauti ya wanawake inasikika ndani na nje ya chama,” amesema.