Serengeti. Serikali imesema itatoa Sh 8.1 bilioni kwa ajili ya kurejesha vivuko na madaraja saba yaliyoharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ambazo zimeharibu miundombinu hiyo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema hayo leo Jumapili Machi 8, 2026 akizungumza katika Kivuko cha Mto Banagi, kilichopo hifadhini humo baada ya kukagua athari za mvua hizo hifadhini humo.
Amesema kuwa tathmini iliyofanywa katika maeneo hayo kumetolewa maombi ya fedha hizo kwa ajili ya kurekebisha madaraja na vivuko ambavyo vimeharibiwa na mvua hiyo.
“Sisi kama Serikali na kama wizara tunawaambia hiyo Sh8.1 bilioni tunawaletea Hifadhi ya Taifa Serengeti ili turejeshe vivuko vyetu na madaraja yetu katika uhalisia wake na zaidi tunataka tuboreshe viwe vivuko na madaraja bora kabisa ambayo hata tukipata mtikisiko aina gani visitikisike, hiyo ndiyo dhamira yetu, Serikali iko tayari kutoa hiyo fedha,” amesema.
Amesema katika kipindi hiki cha mvua kubwa za masika na mabadiliko makubwa ya tabia nchi, zimeathiri madaraja na vivuko saba hifadhini humo ambapo kati ya hivyo daraja moja halipitiki kabisa, huku vingine sita vikiendelea kutumika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, akipokea maelekezo katika Kivuko cha Bwawa la Nabi, kilichopo Hifadhi ya Taifa Serengeti leo Jumapili Machi 8, 2026 wakati alipokagua athari za mvua katika miundombinu hifadhini humo
“Daraja moja halipitiki kabisa na mengine sita yanapitika nipongeze timu Tanapa kurekebisha mawasiliano yaliyoleta shida kuanzia Machi 3 hadi 5 mwaka huu, na kazi zinaendelea kufanyika katika hifadhi yetu ikiwamo utalii na magari ya utalii tunayaona yanaendelea kupita kwa sababu barabara zimerekebishwa kwa muda mfupi.
“Nitoe pole kwa waongoza watalii wetu na wenzetu askari ndani ya hifadhi kwa mtiti waliopata ndani ya siku tatu, kikubwa niwaombe waongoza watalii, askari wetu wanafanya kazi kubwa kuwaongoza kwenye maeneo yaliyopata changamoto naomba madereva mfuate maelekezo mnayopewa,” amesema.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Massana Mwishawa, amewaondoa wasiwasi watumiaji wa barabara wakiwamo wa utalii na kuwa watatumia fedha hizo kuboresha miundombinu ya barabara.
“Tunatarajia tutaboresha miundombinu na kipaumbele cha kwanza ni hii iliyoharibiwa na mvua kubwa, niwaondoe wasiwasi watumiaji wa barabara Serengeti hasa sekta ya utalii, tunaenda kufanya makubwa zaidi kwenye hifadhi hii kwani tunajua bila kuwa na miundombinu mizuri hasa mtandao barabara na viwanja vya ndege hata watalii hawataweza kunufaika vizuri na vivutio vilivyopo,” amesema.