WINGA Mbongo Morice Sichone anayeitumikia Gulf FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili ya Falme za Kiarabu ameanza vizuri akifunga mabao mawili licha ya hali ya taharuki inayosababishwa na machafuko ya vita yanayoendelea katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati.
Nyota huyo alijiunga na Gulf akitokea Trident FC ya Zambia alipocheza mechi 18 akifunga mabao sita na kutoa asisti nane.
Sichone alicheza dakika 180 katika mechi mbili alizocheza na kufunga bao moja katika kila mechi jambo linaloonyesha kuanza vizuri ligi.
Akizungumza na Mwanaspoti Sichone alisema “Kwa kweli kuanza vizuri kunanipa nguvu zaidi ya kupambana, nimefunga mabao mawili kwenye mechi mbili na hilo linanifanya nijiamini zaidi.”
“Natamani niendelee kufunga na angalau nifunge mabao saba kwenye mechi 12 zilizobakia za ligi hayo ndio malengo yangu kwenye msimu wa kwanza kama yatazidi haina shida.”
Kwa sasa zimebaki mechi 12 kutamatisha Ligi Daraja la Kwanza huku Sichone akiamini ana nafasi kubwa ya kufikia malengo hayo endapo ataendelea kupata nafasi na kuonyesha kiwango.