Simba Queens yarudi kambini kujiandaa mzunguko wa pili WPL

SIMBA Queens imeingia kambini mapema kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Wanawake nchini, huku benchi la ufundi likieleza lengo kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mechi zilizosalia.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Mussa Hassan Mgosi alisema kufanya maandalizi ya mapema ni muhimu kwa kikosi hicho ili kurejea uwanjani kikiwa na nguvu mpya ya kupambana.

Alisema kwa sasa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wapo kwenye majukumu ya timu ya taifa lakini wanatarajia kurejea kambini hivi karibuni ili kuungana na wenzao.

“Kwa sasa tunaendelea na maandalizi na baadhi ya wachezaji wetu wapo kwenye majukumu ya timu ya taifa, lakini tunatarajia wataungana na wenzao hivi karibuni ili kuendelea na kambi,” alisema Mgosi na kuongeza

“Ligi imekuwa ngumu hivyo tunapoanza kujiandaa mapema inapunguza presha kwani tukiwa hapa tunahitaji mechi za kujipima kuona wapi panashida turekebishe mapema.”

Kocha huyo alisisitiza lengo kubwa la Simba katika mzunguko wa pili ni kupambana kuhakikisha wanakusanya pointi tatu katika kila mechi watakayocheza.

Simba iko kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 31 lakini ikitofautiana pointi moja na Yanga yenye nazo 30.