Dar es Salaam. Makundi yanayoendelea kukigawa Chama cha Wananchi (CUF) yameibuka tena, baada ya mwenyekiti mpya wa chama hicho, Mirambo Yusuf, kukosa mapokezi alipowasili Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma katika ziara yake ya kujitambulisha kwa wanachama na viongozi wa chama.
Mbali na hali hiyo, alishindwa pia kufanya kikao cha ndani cha kamati ya wilaya baada ya viongozi kutokuhudhuria kwa madai kuwa, hakutoa taarifa kabla ya kufanya ziara eneo hilo ambalo kwa muda mrefu limekuwa ngome ya chama hicho, ukiondoa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Mirambo, aliyechaguliwa Februari 22, 2026 kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, yupo kwenye ziara ya mikoa mbalimbali akijitambulisha na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama ngazi ya wilaya pamoja na wanachama.
Uchaguzi uliomweka madarakani uliibua mjadala mkubwa uliofanyika kufuatia maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uchaguzi uliomweka madarakani, mtangulizi wake, Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wenzake uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024.
Msajili alifuta matokeo ya uchaguzi huo akieleza kuwa, mshindi hakupata zaidi ya nusu ya kura za wajumbe waliopiga kura, hivyo uchaguzi ulipaswa kurudiwa ili kukidhi matakwa ya katiba ya chama hicho ya mwaka 1992 pamoja na kanuni zake.
Uamuzi huo ulizua mgawanyiko ndani ya chama, baadhi ya wanachama waliunga mkono hatua ya Msajili na kukubali kufanyika kwa uchaguzi mpya, huku wengine wakipinga wakidai uongozi uliopo haukupata ridhaa ya wanachama.
Katika hali iliyozua mshangao, ambao unaacha maswali namna ya kutibu migawanyiko ndani ya chama hicho, Mirambo jana Jumamosi, Machi 7, 2026 alifika Kondoa akitokea Dar es Salaam bila kupokewa na viongozi wa chama wilayani humo.
Wilaya ya Kondoa inaongozwa na Othman Dunga, aliyekuwa mshindani wa karibu wa Mirambo katika kinyang’anyiro cha nafasi ya mwenyekiti wa Taifa na ambaye hajakubaliana na ushindi wake, akidai baadhi ya wajumbe waliopiga kura hawakuwa halali.
Pia, alishawasilisha barua ya kupinga ushindi wa Mirambo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambayo bado uamuzi wake haujatolewa hadi sasa.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mirambo amesema hali hiyo ni sehemu ya siasa za zamani ambazo hazipaswi kuendelezwa ndani ya chama anachokiongoza kwa sasa.
“Kilichofanyika ni siasa za miaka ya 60. Kama mwenyekiti wa chama ninayetaka kukipeleka mbele, sikubaliani na mambo kama haya. Lengo langu ni kuona tunafanya maridhiano, lakini maridhiano ni hiyari ya mtu; huwezi kumlazimisha,” amesema.
Amesema pamoja na changamoto alizoanza kukutana nazo, anaamini atavuka salama kwa kuhakikisha anatuliza malalamiko ya wanachama waliojitenga na kukihamasisha chama kusonga mbele kwa pamoja katika harakati za kutafuta dola.
Amesema lengo la kufika Kondoa lilikuwa kuzungumza na viongozi wa chama wilayani humo, lakini kutokana na hali aliyoikuta aliamua kuendelea na safari kuelekea mkoani Singida anakotarajiwa kufanya kikao kabla ya kuendelea na ziara yake katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kigoma kwa ajili ya kujitambulisha na kuweka msingi wa maridhiano ndani ya chama.
Akizungumzia sababu ya Mirambo kutopokewa, Dunga amesema hakupatiwa taarifa yoyote rasmi kuhusu ujio wake, jambo analodai ndilo lililosababisha kutokuwepo kwa mapokezi.
“Sikuwa nimepewa taarifa kabla. Nimeshangaa kusikia amefika ndani ya wilaya yangu. Kwa kawaida kiongozi wa kitaifa anapotaka kufanya ziara ni lazima atoe taarifa mapema,” amesema Dunga.
Dunga, ambaye pia amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara, amesema kwa utaratibu wa chama, mwenyekiti wa Taifa anatakiwa kutoa taarifa angalau wiki moja kabla ya kufanya ziara katika wilaya husika.
“Hatukupata taarifa na hakuna kiongozi wa wilaya aliyeshirikishwa. Hii inaendeleza mfumo wa makundi ndani ya chama. Ingekuwa vizuri angetujulisha kabla badala ya kuja kimya kimya,” amesema.
Ziara hiyo ya Mirambo ni ya pili tangu achaguliwe kuwa mwenyekiti wa Taifa, lakini imeingia dosari.
Ziara yake ya kwanza aliifanya mkoani Tabora alikopata mapokezi makubwa, yakichangiwa na sababu kadhaa.
Kwanza, aliwahi kuwa kiongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya kwa miaka 10 kuanzia mwaka 2014 hadi 2024. Pili, alikuwa kocha msaidizi wa timu ya Tabora United. Tatu, ni mzaliwa wa eneo hilo, hivyo ziara hiyo ilikuwa kama kurejea nyumbani.