Sowah anavyohesabu siku Simba | Mwanaspoti

MAISHA ya Jonathan Sowah yanapitia kwenye uzi mwembamba unaozuia pande hizo mbili kupita kwa pamoja, hatua ambayo inamfanya mshambuliaji huyo kuwa kwenye eneo gumu la kuendelea kuwepo kikosini msimu ujao.

Hiyo inakuja baada ya zile siku tatu alizopewa kujitetea kwa kile kilidaiwa makosa aliyofanya yaliyosababisha kusimamishwa kumalizika jana, huku taarifa zikibainisha kuwa nasubiriwa uongozi kutoa tamko la nini umeamua juu ya straika huyo raia wa Ghana.

Sowah alisimamishwa kwa madai ya utovu wa nidhamu huku akitakiwa kutoa maelezo kuhusu kuchelewa kwenye mikutano kadhaa ya timu, kukataa kufanya mazoezi ya ziada, kuchelewa mazoezini, kusafiri kwenda Angola kucheza dhidi ya Petro Atletico akiwa amevaa jezi ya SL Benfica badala ya mavazi rasmi ya klabu. Mwisho ni kufanya faulo za makusudi zinazoweza kusababisha kadi nyekundu, ikiwemo kwenye mechi dhidi ya Azam FC na Espérance.

Ikumbukwe kuwa, wakati Simba inamsajili Sowah, ilikuwa na hesabu ya kiwango cha mshambuliaji huyo alichoonyesha msimu uliopita, akifunga mabao 13 ndani ya mechi 14 za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara akiwa na Singida Black Strars.

Takwimu hizo zilivutia timu nyingi zilizoanza hesabu za kumsajili kutokana na kuonyesha ubora mkubwa wa kufunga akilingana na washambuliaji wengine kama Lionel Ateba, Steven Mukwala ambao walikuwa Simba na Prince Dube wa Yanga wote wakifunga idadi kama hiyo, lakini wao wakifanya hivyo kwa msimu mzima.

Simba iliamini kama Sowah alifunga mabao hayo akiwa Singida tena nusu msimu, basi anaweza kufunga zaidi akiwa kwao lakini matarajio hayo yamekuwa tofauti na kile ambacho kinaonekana sasa akiwa ndani ya jezi ya Wekundu wa Msimbazi.

Simba kwa sasa haioni kabisa mwanga wa kupata kile ilichokitarajia kwa Sowah na wakiona kama ni mchezaji ambaye anatoboa mtumbwi wakati safari inaendelea, hatua ambayo hivi karibuni imefikia kumsimamisha.

SOWA 01


Simba imefikia uamuzi huo kutokana na hatua za Sowah ndani ya muda ambao amekaa hapo kukumbana na matukio mawili ya kusimamishwa, akianza kukosa mechi za kwanza za ufunguzi wa ligi baada ya kupewa kadi nyekundu msimu uliopita kwenye mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB akiwa Singida akicheza dhidi ya Yanga.

Adhabu hiyo ilianza kuja kutumika akiwa Simba ambapo ilimfanya mshambuliaji huyo kukosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga na wekundu hao wakapoteza kwa bao 1-0, huku wakikosa huduma ya mshambuliaji ambaye waliamini angewasaidia.

Baada ya hapo akaja kusimamishwa na Kamati ya Usimamizi wa Ligi kwa mechi tano baada ya kumpiga kiungo wa Azam, Himid Mao, akakaa tena nje huku klabu yake ikiendelea kukosa huduma yake kwa mechi nne za ligi na moja Kombe la FA.

Kadi hizo ndani ya Simba zimechukuliwa kwa tofauti baada ya mabosi wa Wekundu kuona kama mshambuliaji huyo anazipata kirahisi hasa kutokana na kwamba yapo matukio ambayo hakupata adhabu kama hiyo lakini alionyesha kukaribia kukumbana na maamuzi ya namna hiyo.

SOWA 02


Ukiacha hilo, kiufundi Sowah ameshindwa kutoboa ndani ya kikosi cha kwanza cha Simba chini ya makocha watano msimu huu kuanzia Fadlu Davids, Dimitar Pantev, Hemed Suleiman, Seleman Matola na sasa Steve Barker.

Makocha wote wamekuwa wanaonyesha kutokukubaliana na kiwango cha Sowah ambapo hata alipoanzishwa alitolewa mapema bila ya mshambuliaji huyo kuonyesha kitu kikubwa sana uwanjani.

SOWA 03


Simba wao wanayaangalia hayo, lakini Sowah mwenyewe naye amekuwa na madai yake hasa kutokana na kutopata muda wa kutosha wa kucheza, akiona kama mpango huo unasukwa ili asiweze kufanya kile ambacho anataka kukifanya.

Ukizungumza na Sowah, anadai kuna wakati amekuwa akionyesha kufunga mabao huku akicheza vizuri tena akitokea benchi lakini kwenye mchezo unaofuata, kocha anarudi kumuanzisha tena benchi au hata kutopewa nafasi kabisa hatua ambayo imepunguza morali yake ya kuendelea kujituma zaidi.

Akiwa Simba, msimu huu timu hiyo ikiwa imecheza mechi 25 za mashindano tofauti kabla ya jana (Ligi ya Mabingwa 10, Ligi Kuu Bara 11, Kombe la Mapinduzi 3 na Ngao ya Jamii 1), Sowah amecheza mechi 11 kwa dakika 477.

Mechi hizo ni Ligi Kuu Bara (4), Ligi ya Mabingwa Afrika (6) na Kombe la Mapinduzi (1) ambapo Sowah amefanikiwa kufunga mabao matatu yote kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, JKT Tanzania na Mbeya City.

SOWA 04


Simba wakati inaendelea kutafuta suluhisho la namna ya kuachana na mshambuliaji huyo, zipo taarifa kwamba wakubwa wa klabu hiyo wameshaanza mchakato wa siri wa kutafuta mshambuliaji mwingine kwa mahitaji ya msimu ujao.

Tusubiri kuona kipi kitatokea kwenye sakata la mshambuliaji huyo raia wa Ghana akiendelea kupambabna mezani na mabosi wa klabu yake kwani lolote linaweza kutokea kwa pande hizo mbili kuachana.