Twiga Stars kurejea leo | Mwanaspoti

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Twiga Stars, kinarejea leo kutokea Falme za Kiarabu kilipokita kambi kwa ajili ya kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026.

Twiga Stars ilikuwa UAE ikishiriki mashindano ya kujipima nguvu ya Pink Ladies Cup ambayo yalikuwa ni maandalizi ya WAFCON 2026 yaliyotarajiwa kuanza Machi 17, 2026 nchini Morocco, kabla ya kusogezwa mbele hadi Julai 25, 2026.

Katika mashindano hayo ya kujipima nguvu, Twiga Stars ilicheza mechi  dhidi ya Urusi ikapoteza kwa mabao 4-2, lakini ilitarajiwa kucheza mechi mbili zingine dhidi ya Hong Kong na Ghana ambazo zote zilijiondoa kutokana na hofu ya kiusalama inayosababishwa na mzozo wa Iran, Israel na Marekani.

Mmoja ya wachezaji wa Twiga Stars, aliliambia Mwanaspoti kuwa baada ya kupelekwa mbele mashindano hayo, sasa timu hiyo inarejea leo jioni kutokea UAE.

“Timu inarudi kesho (leo Jumapili), hatuna cha kufanya huku kwa sababu tuliweka kambi kwa ajili ya maandalizi na mashindano yenyewe yamesogezwa mbele, hivyo tunarudi nyumbani kujiandaa na ligi,” amesema mchezaji huyo.

Kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime amesema kusogezwa mbele kwa WAFCON 2026, sio taarifa nzuri kwa upande wao, kwani tayari walikuwa wamejipanga kwa ajili ya mashindano hayo.

Aliongeza kuwa, uamuzi huo unaweza kuwa na faida na hasara kwa upande mzuri, timu inaweza kupata muda zaidi wa kuendelea kujiandaa na kuboresha baadhi ya maeneo kabla ya mashindano kuanza.

“Sio taarifa nzuri sana kwa upande wetu kwa sababu tulikuwa tayari, tulishajenga timu na hata kiakili tulikuwa tayari kwa mashindano. Inaweza kuwa jambo zuri kwa upande mmoja na baya kwa upande mwingine,” amesema kocha huyo na kuongeza.

“Zuri ni kwamba tunaweza kupata muda zaidi wa kujiandaa, lakini pia kuna hasara kwa sababu baadhi ya wachezaji wetu wanacheza nje ya nchi, hivyo watalazimika kurudi kwenye timu zao.”

Twiga Stars imepangwa kundi B itakapokabiliana na Afrika Kusini, Ivory Coast na Burkina Faso ikiwa mara ya tatu timu hiyo kucheza WAFCON baada ya 2010 ilipoishia hatua ya makundi na 2024 ilipomaliza mkiani kwenye kundi C na pointi moja.