Unafahamu chimbuko la Siku ya Wanawake Duniani?

Dar es Salaam. Kila mwaka ifikapo Machi 8, dunia huadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Katika nchi nyingi siku hii huambatana na mikutano, maandamano, kampeni za kijamii na tafakuri kuhusu mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii pamoja na changamoto zinazowakabili.

Hata hivyo, nyuma ya maadhimisho haya kuna historia ndefu ya mapambano ya kijamii na kisiasa yaliyoanza zaidi ya karne moja iliyopita, yakiongozwa na wanawake waliodhamiria kubadilisha mfumo uliowatenga katika haki za kisiasa, ajira na ushiriki katika uamuzi wa jamii.

Mwanzo wake huko Marekani

Moja ya matukio ya mwanzo kabisa yanayohusishwa na siku hii lilitokea Marekani mwaka 1909. Chama cha Kisoshalisti cha Marekani kiliandaa maadhimisho yaliyoitwa National Woman’s Day, Februari 28, 1909 mjini New York.

Maadhimisho hayo yalihamasishwa na wanaharakati wa haki za wanawake waliokuwa wakipinga mazingira magumu ya kazi kwa wanawake katika viwanda na ukosefu wa haki za kisiasa kwa wanawake.

Mwanaharakati wa wafanyakazi, Theresa Malkiel ambaye alikuwa miongoni mwa waandaaji wa siku hiyo, alisema wanawake walipaswa kusimama na kudai haki zao waziwazi ili kufikia usawa huo.

Katika maandiko yake aliwahi kueleza wanawake wafanyakazi walipaswa kupewa nafasi sawa katika jamii na si kuendelea kubaki pembezoni mwa uamuzi wa kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yakifanywa na wanaume pekee.

Wazo la siku ya wanawake duniani

Hatua muhimu zaidi katika historia ya siku hii ilitokea mwaka mmoja baada ya tukio hilo la Marekani, mwaka 1910, katika mkutano wa kimataifa wa wanawake wanaharakati uliofanyika Copenhagen, Denmark.

Mkutano huo uliwakutanisha zaidi ya wanawake 100 kutoka nchi 17 waliokuwa wanaharakati wa vyama vya wafanyakazi, vyama vya kisiasa na harakati za haki za wanawake.

Katika mkutano huo mwanaharakati wa Kijerumani, Clara Zetkin alipendekeza kuanzishwa kwa siku maalumu ya kimataifa ya wanawake.

Katika hoja yake alisema,

“Kila mwaka katika kila nchi kunapaswa kuwa na siku maalumu ya wanawake ili kuhamasisha madai yao ya haki na usawa.”

Pendekezo hilo liliungwa mkono kwa kauli moja na wajumbe wote wa mkutano huo, jambo lililoweka msingi wa kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake Duniani.

Maadhimisho ya kwanza ya kimataifa

Mwaka uliofuata wa 1911, maadhimisho ya kwanza ya kimataifa ya Siku ya Wanawake yalifanyika katika nchi kadhaa za Ulaya, zikiwemo Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi.

Zaidi ya watu milioni moja walishiriki katika mikutano na maandamano yaliyoanzisha maombi ya haki za wanawake kupiga kura, kushika nyadhifa za umma, na kufanya kazi bila ubaguzi.

Katika hotuba zilizotolewa wakati wa mikutano hiyo, wanaharakati walisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kuwa na haki sawa za kushiriki katika maamuzi ya jamii kama ilivyo kwa wanaume.

Mapinduzi ya Urusi na Machi 8

Tukio lingine muhimu lilitokea mwaka 1917 nchini Urusi wakati wanawake wafanyakazi wa viwanda vya nguo walipoanzisha maandamano wakidai mkate na amani wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia.

Maandamano hayo yalifanyika Machi 8 na yalikuwa na athari kubwa katika historia ya kisiasa ya nchi hiyo.

 Mwanamapinduzi Leon Trotsky aliandika katika kumbukumbu zake kwamba wanawake wanaweza kuleta mapinduzi makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Maandamano hayo yaliendelea na hatimaye yalichangia kuanguka kwa utawala wa kifalme nchini Urusi. Baada ya tukio hilo, serikali mpya iliyoundwa ilitambua rasmi Machi 8 kama siku ya wanawake nchini humo.

Kutambuliwa na Umoja wa Mataifa

Kwa miongo kadhaa, maadhimisho ya Siku ya Wanawake yaliendelea zaidi ndani ya harakati za kijamii na vyama vya wafanyakazi.

Hatua kubwa ya kimataifa ilitokea mwaka 1975 wakati Umoja wa Mataifa ulipotangaza mwaka wa kimataifa wa wanawake na kuanza kuadhimisha rasmi Siku ya Wanawake Duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Kurt Waldheim, alisisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja katika kuendeleza usawa wa kijinsia. Katika ujumbe wake wa kuitambua rasmi siku hiyo, alisema, “ushiriki kamili wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ni muhimu kwa maendeleo ya dunia.”

Baadaye, mwaka 1977, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililozitaka nchi wanachama kuadhimisha siku ya haki za wanawake na amani duniani kwa mujibu wa historia na mila za kila Taifa.

Mkutano wa Beijing na mchango wake kwa harakati za wanawake

Mwaka 1995, Umoja wa Mataifa uliandaa kongamano lililoitwa Fourth World Conference on Women katika jiji la Beijing, China, lililowaleta pamoja wajumbe wa serikali, wanaharakati, na mashirika ya kiraia kutoka zaidi ya nchi 180 kujadili haki na maendeleo ya wanawake duniani.

Mkutano huo ulipitisha waraka muhimu uitwao Beijing Declaration and Platform for Action, ulioweka mikakati ya kimataifa ya kuimarisha usawa wa kijinsia katika maeneo muhimu kama elimu, afya, uchumi, uongozi wa kisiasa, na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake.

Tangu wakati huo, ajenda za mkutano wa Beijing zimekuwa msingi wa sera nyingi za kimataifa kuhusu wanawake na hujadiliwa kila mwaka katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kama kipimo cha maendeleo ya haki na usawa wa kijinsia.

Maana yake katika dunia ya leo

Leo zaidi ya miaka 100 tangu wazo la siku hii kuzaliwa, wadau wa masuala ya wanawake wanakiri Siku ya Wanawake Duniani imekuwa jukwaa muhimu la kimataifa la kuzungumzia maendeleo na changamoto zinazowakabili wanawake.

Katika nchi nyingi, wanawake wamepiga hatua kubwa katika elimu, ajira, na uongozi wa kisiasa. Hata hivyo, changamoto kama ukosefu wa usawa wa kipato, ukatili wa kijinsia, na mimba za utotoni bado zinaendelea kujadiliwa katika majukwaa ya kimataifa.

Kwa maana hiyo, Siku ya Wanawake Duniani si tu siku ya sherehe bali pia ni kumbukumbu ya mapambano ya kihistoria yaliyolenga kubadilisha nafasi ya wanawake katika jamii, bali pia ni siku inayokumbusha dunia kuwa haki nyingi wanazofurahia wanawake leo zilipatikana kupitia ujasiri wa wanaharakati waliothubutu kusimama na kusema kwa sauti kwamba wanawake wanastahili usawa, heshima, na nafasi sawa katika maisha ya binadamu.