Dar es Salaam. Tanzania imelenga kuongeza tija ya uzalishaji wa kilimo katika mazao 13 ya kimkakati baada ya kusainiwa kwa makubaliano yanayolenga kuhakikisha wakulima wote walio katika vyama vya ushirika wanapatiwa mbegu bora na zenye tija kwa wakati.
Mkataba huo wa makubaliano wa miaka mitano uliosainiwa kati ya Shirikisho la Vyama Vya Ushirika Tanzania (TFC) na Wakala wa Mbegu za Kilimo ASA unalenga kurahisisha mnyororo wa usambazaji mbegu kufika kwa wakulima na kupunguza bei ambayo iliyokuwapo awali kutokana na kukosekana kwa usimamizi mzuri.
Taarifa ya kusainiwa kwa mkataba hiyo iliyotolewa leo Jumapili, Machi 8, 2026 inaeleza sasa vyama vya ushirika vitatumika kama njia kuu ya kusambaza mbegu bora kwa wakulima, tofauti na mfumo wa awali mbegu zilikuwa zinasambazwa kupitia maduka au kwa watu mmoja mmoja hali iliyokuwa ikiwafikia wakulima wachache.
Mtendaji Mkuu wa TFC, Fares Muganda amesema lengo la ushirikiano huo ni kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa wakati ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kuondoa malalamiko ya wakulima kuuziwa mbegu zisizo na tija.
“Kwa kawaida muundo wa vyama vya ushirika nchini unaanzia katika vyama vya msingi vilivyopo vijijini, kisha umoja wa vyama katika ngazi ya mikoa na hatimaye shirikisho la kitaifa, jambo linalorahisisha kuwafikia wakulima wengi kwa wakati mmoja,” amesema.
Kupitia mfumo huo, taarifa kuhusu upatikanaji wa mbegu na mahitaji yake katika maeneo mbalimbali zitaweza kufika kwa haraka kwa wakulima kupitia vyama vyao.
Aidha, ushirikiano huo unatarajiwa kupunguza mlolongo mrefu wa usambazaji wa mbegu ambao umekuwa ukichangia kupanda kwa bei ya pembejeo hizo kwa wakulima.
Hadi kufikia Juni 30, 2025, jumla ya vyama vya ushirika vilivyosajiliwa nchini ni 7,984. Huku baadhi ya mazao ambayo mbegu zake zitazalishwa yakiwa ni choroko, alizeti, miche ya matunda, mahindi, mpunga.
Mkurugenzi Mtendaji wa ASA, Leo Mavika amesema makubaliano hayo yatakwenda kujibu changamoto ya usambazaji mbegu waliyokuwa nayo kwa muda mrefu kutokana na kushindwa kuwafikia wakulima inavyotakiwa.
“Kuna mwaka tulizalisha mbegu lakini zilishindwa kufika kwa wakulima kwa sababu usambazaji ulikuwa changamoto kubwa, sasa kusainiwa kwa makubakiano haya inatufanya tuwe na uhakika wa mbegu kufika kwa wakulima kwa kiwango kinachotakiwa,” amesema.
Amesema kwa sasa mahitaji ya mbegu nchini ni tani 127,650 kwa mwaka wakati uzalishaji wa ndani ni takribani tani 70,000 pekee huku kiwango kinachobakia kikiagizwa kutoka nje ya nchi.
“Hivyo mnaona ni kwa kiasi gani kuongeza uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi kutasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni pamoja na kuongeza tija kwa wakulima ambao kwa sasa wengi wao hawapati mbegu bora kwa wakati,” amesema.
Amesema katika kuhakikisha uzalishaji wa mbegu unakuwa kwa kiwango kikubwa bila kukwamishwa na rasilimali Asa walilazimika kutumia kilimo cha mkataba kupitia hekta 17,000 za mashamba inayomiliki.
“Mashamba haya yanapatikana maeneo mbalimbali nchini na kupitia mfumo huu wa kilimo cha mkataba tumefanikiwa kuongeza tija jambo ambalo limetupunguzia mzigo wa majukumu ambayo wakati mwingine yalikuwa yanakwamishwa na upatikanaji wa fedha kwa wakati husika,” amesema.
Katika mfumo huo sasa wakulima huchaguliwa kwa vigezo maalumu na kupewa maelekezo ya namna ya kuzalisha mbegu bora huku wakisimamiwa katika hatua zote za uzalishaji.
“Baada ya kuvuna, mbegu hupimwa na kuthibitishwa ubora wake na taasisi maalumu kabla ya kuchukuliwa na ASA kwa ajili ya kusindika na kuingizwa sokoni,” amesema.
Njia hiyo imesaidia kuongeza tija na uzalishaji kwani inaendana na kalenda ya uzalishaji kwani wakulima wanakuwa na uhakika wa kupata mbegu.
“Mkulima anakuwa amejipanga na anazalisha kwa wakati kufuata kalenda na atapata mbegu ya kutosha, awali tulikuwa tunashindwa kutumia ardhi yote kwani ilifika wakati mnafanikiwa kulima eneo lote lakini mkitaka kupanda hakuna fedha inabidi msubiri wakati ambao mwaka wa kilimo hauwasubiri,” amesema.
Tathmini inaonesha kuwa katika msimu wa mwaka 2024 uzalishaji wa mbegu ulikuwa tani 4,500 lakini baada ya kushirikisha vyama vya ushirika umeongezeka hadi kufikia tani 9,303.
“Kwa msimu ujao, lengo ni kuongeza uzalishaji huo hadi kufikia tani 90,000 ili kupunguza pengo la mbegu nchini na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa wakati na kwa gharama nafuu,” amesema.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo pamoja na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumzia suala hili, Salim Salim ambaye ni mkulima amesema japokuwa mpango huu umekuja kwa kuchelewa lakini utasaidia kupunguza gharama za upatikanaji wa mbegu bora.
“Hii inamaanisha kuwa mbegu zitatoka moja kwa moja kwa mzalishaji kuja kaa mkulima kupitia vyama vya ushirika, itaondoa watu kati wengi ambao walikiwa wakisababisha mbegu kupanda bei,” amesema Salim.