Wataalamu walaani kuwanyima watoto haki za msingi

Tanga. Wataalamu wa malezi na makuzi ya watoto mkoani Tanga wametahadharisha kuwa kuwanyima watoto haki zao za msingi za kucheza, kupumzika na kukua katika mazingira salama na yenye afya kunahatarisha maendeleo yao ya kimwili na kiakili.

Wataalamu hao wanasema vitendo hivyo vinaweza kuathiri si tu ukuaji wa kimwili wa watoto, bali pia maendeleo yao ya akili na ustawi wa kijamii.

Wametaka wazazi, jamii na wadau kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kufurahia utoto wake kwa huru na kwa usalama.

Hali hiyo ilielezwa jana Jumamosi Machi 7, 2026 wakati wa warsha ya siku mbili kuhusu Malezi, Ukuaji na Maendeleo ya Mtoto katika umri wa awali, iliyohudhuriwa na maofisa kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Akizungumza katika warsha hiyo, mtaalamu wa maendeleo ya mtoto, Bruno Ghumpi amesema mjamzito anapaswa kupata lishe bora kwa kuwa, afya na ustawi wa mtoto hutegemea hali ya mama yake wakati wa ujauzito.

“Ili mtoto aweze kukua katika utimilifu wake, mjamzito anapaswa kupata lishe bora na huduma za afya. Baada ya kuzaliwa pia mtoto anahitaji ulinzi, usalama pamoja na fursa ya kujifunza kupitia malezi yenye mwitikio kutoka kwa wazazi na walezi,” amesema Ghumpi.

Amebainisha kuwa, kuna mambo nane muhimu yanayochangia ukuaji mzuri wa ubongo wa mtoto ambayo ni lishe bora, kucheza, kupumzika, maji safi na salama ya kunywa, afya bora, ulinzi na usalama wa mtoto, uchangamshwaji wa awali pamoja na upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa watoto.

Ghumpi pia ameonya kuwa watoto wengi hasa katika baadhi ya shule binafsi wanakabiliwa na mzigo mkubwa wa masomo unaowanyima muda wa kupumzika na kucheza.

“Watoto wengi wanatumia muda mwingi darasani na wanaporudi nyumbani wanapewa kazi nyingi za nyumbani hata wakati wa likizo. Bila kucheza na kupumzika, tunawanyima nafasi ya kukua na kuwa watu wazima wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Lishe wa Mkoa wa Tanga, Sakina Mustapha amesema lishe timilifu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya mtoto tangu akiwa tumboni.

 “Lengo la programu hii ni watoto kuanzia umri wa sifuri hadi miaka nane. Hivyo, tunaanza kumuangalia mtoto akiwa tumboni mwa mama yake kwa kuhakikisha mama anahudhuria kliniki na anapata vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mtoto,” amesema Sakina.

Ameongeza kuwa, mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo kabla ya kuanza kupewa vyakula vya ziada.

“Tunasema mtoto anyonye maziwa ya mama pekee hadi miezi sita. Baada ya hapo anaweza kuanza kupewa vyakula mchanganyiko kwa sababu maziwa ya mama pekee hayawezi kukidhi mahitaji yote ya lishe,” amesema.

Amesema mtoto anapaswa kuendelea kupata lishe bora hadi kufikisha angalau miezi 24 huku akiendelea kukua na kuanza hatua mbalimbali za maendeleo.

“Baada ya kufikisha miaka miwili mtoto anaweza kuanza shule za awali huku akiendelea kula vyakula mchanganyiko. Tunashukuru Mkoa wa Tanga una vyakula mbalimbali vinavyoweza kusaidia lishe ya mtoto,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa United Help for Tanzania Children (UHTC), Regis Temba amesema taasisi yao imepanga kuanzisha maeneo maalumu ya kucheza na kuchochea ukuaji wa akili za watoto katika vituo vitano vya afya ndani ya Jiji la Tanga.

Amesema maeneo hayo yatasaidia kubadilisha mazingira ya kliniki kuwa rafiki kwa watoto wanaofika kupata huduma pamoja na wazazi wao.

“Tunataka watoto wanapokuja kliniki wasione ni sehemu ya sindano na matibabu pekee, bali waweze pia kucheza na kujifunza kupitia michezo mbalimbali inayochochea ukuaji wa ubongo,” amesema Temba.