Mwanza. Mfanyakazi wa kazi za nyumbani, Faima Twaibu (19), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza kwa tuhuma za kujaribu kumuua mtoto wake mchanga baada ya kujifungua.
Faima, mkazi wa Bulyehele wilayani Ilemela, amefikishwa mahakamani leo Jumatatu Machi 9, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Christian Mwalimu.
Katika shauri hilo namba 5112/2026, mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la jaribio la kuua, kinyume na Kifungu cha 211(b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Evance Kaiza akisaidiana na Clara Muhando umedai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 25, 2025.
Inadaiwa mshtakiwa alijifungua mtoto mchanga na kisha kumtupa juu ya paa la nyumba kwa lengo la kutoa uhai wake.
Akijibu swali la Hakimu Mwalimu aliyetaka kujua sababu ya kumtupa mtoto huyo juu ya paa la bati, mshtakiwa amedai kuwa alifikia uamuzi huo kwa hofu ya mwajiri wake asigundue kuwa alikuwa mjamzito na amejifungua.
“Sikutaka bosi wangu ajue kama nilikuwa mjamzito na nimejifungua mtoto” amesema Faima.
Hakimu Mwalimu ameeleza kosa hilo lina dhamana, ambapo mshtakiwa ametakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa (Nida) na barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa. Aidha, kila mdhamini alitakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh3 milioni.
Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na hivyo kupelekwa rumande.
Kuhusu hali ya mtoto aliyenusurika kifo ambaye kwa sasa ana miezi miwili na wiki mbili, yupo salama chini ya uangalizi wa maofisa ustawi wa jamii.
Shauri hilo limepangwa kutajwa tena Machi 23, 2026, kwa ajili ya kusomewa hoja za awali na kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri.