Dar es Salaam. Kifo cha kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kilichotokea Februari 28, 2026, wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, kinaashiria moja ya mabadiliko makubwa zaidi katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mrithi wake, mwanaye, Mojtaba Khamenei, anawakilisha kwa wakati mmoja mwendelezo na pia mkanganyiko ndani ya mfumo wa mapinduzi ulioanzishwa baada ya mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979.
Kinachowekwa hatarini si tu nani ataiongoza Iran, bali pia kile ambacho Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa karibu nusu karne baada ya mapinduzi yaliyokuwa na ahadi ya kumaliza utawala wa kifamilia.
Mojtaba Khamenei ni nani?
Mojtaba Khamenei ni kiongozi wa kidini (mwanazuoni wa Kiislamu) ambaye ametumia sehemu kubwa ya kazi yake nje ya nafasi rasmi za serikali lakini akiwa karibu sana na mamlaka, akifanya kazi ndani ya Ofisi ya Kiongozi Mkuu.
Mmmpoja wa wananchi akiwa amebeba bango lenye picha ya Mojtaba Khamenei mtoto wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei. Picha na Mtandao
Mara nyingi alionekana kama mlinzi wa lango la mamlaka na mpatanishi wa nguvu za kisiasa kuliko kuwa mwanasiasa wa wazi mwenye wadhifa rasmi.
Akiwa na umri wa miaka 17, aliwahi kwa muda mfupi kushiriki katika vita ya Iran–Iraq. Alianza kuvutia umakini wa umma mwishoni mwa miaka ya 1990, wakati mamlaka ya baba yake kama kiongozi mkuu yalipokuwa tayari yameimarika.
Kadiri muda ulivyopita, sifa yake imejengwa juu ya mambo mawili makuu: Kwanza, uhusiano wa karibu na vyombo vya usalama vya Iran, hasa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pamoja na mitandao yake yenye msimamo mkali. Pili, upinzani mkali dhidi ya siasa za mageuzi na juhudi za kushirikiana na nchi za Magharibi.
Wakosoaji wamemuhusisha na ukandamizaji wa maandamano yaliyotokea baada ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2009 uliokuwa na utata.
Pia, inaaminika kuwa alikuwa na ushawishi katika shirika la utangazaji la serikali ya Iran, jambo lililompa udhibiti usio wa moja kwa moja juu ya sehemu ya mfumo wa habari na simulizi rasmi za serikali nchini humo.
Mwaka 2019, awamu ya kwanza ya Rais Donald Trump ilimuwekea vikwazo dhidi ya Mojtaba, ukimtuhumu kufanya kazi kwa niaba ya kiongozi mkuu licha ya kutokuwa na wadhifa rasmi serikalini.
Katiba ya Iran inaeleza kwamba Baraza la Wataalamu chombo cha wanazuoni wa dini 88 ndicho kinachochagua kiongozi mkuu.
Baraza hilo huorodhesha sifa za kidini, kisiasa na za uongozi kwa wagombea wanaowezekana. Hata hivyo, kwa vitendo, si chombo huru kabisa cha uchaguzi. Wagombea wa baraza lenyewe hupitia mchakato wa kuchujwa na taasisi ambazo hatimaye ziko ndani ya ushawishi wa Kiongozi Mkuu, na mijadala yao hufanyika kwa siri.
Hali hii huunda mazingira ya kawaida katika siasa za Iran: katiba inaweka taratibu za kinadharia, lakini taasisi za usalama na za kidini ndizo huamua mwelekeo halisi wa mamlaka.
Akiwa mwanazuoni wa kiwango cha kati, Mojtaba alipewa cheo cha Ayatollah mwaka 2022. Cheo hicho ni muhimu ili mtu aweze kuwa Kiongozi Mkuu, hivyo kupandishwa huko kulionekana kama ishara kwamba alikuwa anaandaliwa kuchukua nafasi ya baba yake aliyekuwa akizeeka na kuugua.
Aliyekuwa kiongozi mkuu wa Iran, Ali Khamenei enzi za uhai wake. Picha na Mtandao
Hadithi ya msingi ya mapinduzi ya Iran ilikuwa wazi kupinga utawala wa kifamilia. Baada ya kumuondoa madarakani Shah, viongozi wa mapinduzi walikataa mfumo wa urithi wa kifalme.
Kwa Wairani wengi, mtoto kumrithi baba yake kama kiongozi mkuu kunaonekana kama kurudi nyuma kiitikadi. Mfumo huo unaonekana zaidi kama ufalme wa kidini badala ya dhana maarufu ya ulinzi wa sheria za Kiislamu.
Hata hivyo, mifumo ya kisiasa inaweza kuwa ya kifamilia bila kubadilisha katiba. Matokeo ya aina hiyo hutokea pale ambapo mitandao ya mamlaka isiyo rasmi kama uhusiano wa kifamilia, upendeleo wa kisiasa, uhusiano wa kiusalama na udhibiti wa vyombo vya habari humfanya mgombea mmoja aonekane wa kawaida, salama zaidi au hata asiyeepukika.
Mwanazuoni wa Kishia na mjumbe wa Baraza la Walinzi, Alireza Arafi, aliyechaguliwa kuwa mwakilishi wa wanazuoni wa sheria katika Baraza la Uongozi la Muda la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kwa miaka mingi, hiyo ndiyo imekuwa simulizi ya Mojtaba nchini Iran: mtu aliyekuwa akijenga ushawishi wake si kwa kushinda uchaguzi, bali kwa kudhibiti lango la kuingia katika ofisi yenye nguvu zaidi nchini humo.
Wakati huohuo, Rais wa Marekani, Donald Trump, amesisitiza tena kwamba angeweza kuwa na ushawishi juu ya kiongozi mkuu ajaye wa Iran, akisema kuwa yeyote atakayechaguliwa katika nafasi hiyo bila idhini ya Marekani hatadumu kwa muda mrefu.
Alitoa kauli hiyo Jumapili iliyopita, saa chache kabla ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuripoti kwamba Baraza la Wataalamu limechagua kiongozi mkuu mpya, Mojtaba Khamenei, mtoto wa Ali Khamenei, ambaye aliuawa saa chache baada ya Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran.
Trump hakujibu mara moja kuhusu uteuzi wa Mojtaba, lakini awali alisema kwa ujumla kuwa mtu yeyote atakayechukua nafasi hiyo atalazimika kupata idhini ya Marekani. Maofisa wa Iran wamekanusha kwamba utawala wa Trump umekuwa na ushawishi wowote katika uamuzi huo.
“Lazima apate idhini kutoka kwetu,” Trump aliiambia ABC News akimaanisha kiongozi mkuu mpya anayetarajiwa. “Kama hatapata idhini kutoka kwetu, hatadumu kwa muda mrefu.”