Ibenge aziwaza Yanga, Simba | Mwanaspoti

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema licha ya sare mbili mfululizo ilizopata timu hiyo ugenini, lakini haijawatoa katika malengo yao ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Azam iliyowahi kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014, kwa sasa ipo nafasi ya tatu ikikusanya pointi 24 sawa na Simba iliyopo ya nne, zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Azam ikicheza mechi 12 na Simba 11.

Katika mechi mbili za ugenini, Azam imefululiza sare ikianza dhidi ya Pamba Jiji kwa mabao 2-2 huko jijini Mwanza, kisha 0-0 mbele ya Tanzania Prisons jijini Mbeya.

Timu hiyo iliyocheza mechi 12 na kuvuna pointi 24, imezidiwa pointi nane na vinara Yanga yenye 32 baada ya mechi 12.

Ibenge alisema licha ya wachezaji kuonyesha uwezo kwa kutengeneza nafasi nyingi, lakini umakini ulikuwa mdogo katika kuzitumia kupata mabao.

Alisema kwa sasa anaenda kusahihisha makosa eneo la ushambuliaji na kuongeza makali zaidi kuhakikisha michezo inayofuata wanafanya vizuri na hawajapoteza malengo katika vita ya ubingwa Ligi Kuu.

“Bado tuna mechi nyingi za kucheza na hatujapoteza malengo yetu, tatizo limetokea kwenye kutumia nafasi za mabao kufunga, nitalifanyia kazi, kiuwezo nawapongeza vijana kwa wanavyopambana.

“Katika mechi tatu nyuma tulifunga mabao saba, haikuwa mbaya.  Ligi ni ngumu lazima tuendelee kupambana na kila mchezo tunaokutana nao ili kufikia malengo,” alisema kocha huyo.

Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda alisema kupoteza pointi nne ugenini si matokeo mazuri kwao akiahidi michezo inayofuata watajitathimini na kurejesha ari ya ushindi.

Kuhusu vita ya ubingwa, Mwaikenda alisema bado wapo ndani ya malengo na jukumu lao ni kucheza kwa mipango katika michezo 16 iliyobaki kuhakikisha wanatimiza ndoto zao akiahidi timu hiyo itafanya vizuri.

“Pointi nne tulizopoteza ugenini ni nyingi, lakini bado tupo kwenye malengo, mechi zilizobaki ni kuzicheza kwa hesabu, tunaenda kujipanga upya kufikia malengo,” alisema staa huyo.