Arusha. Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imezindua mpango wa kuanzisha chuo cha mafunzo ya ufundi stadi (Veta) katika Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuwasaidia vijana walioko hatarini kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi huo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Fadhili Maganya, amesema eneo lenye ukubwa wa ekari 6.5 linatarajiwa kujengwa chuo hicho baada ya kukamilika kwa mazungumzo na wadau, wahisani watakaosaidia kufanikisha mradi huo.
Maganya amesema ziara hiyo imelenga kujionea eneo hilo ili kupata uelewa wa kina kabla ya kuendelea na mazungumzo ya ufadhili wa mradi huo, ambao unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii.
“Nimekuja kuona eneo hili ili nitakapozungumza na wahisani kuhusu ufadhili wa mradi huu niwe na uelewa wa kina wa ninachokizungumzia,” amesema.
Ameeleza kuwa wazo la kuanzisha mradi huo limetokana na kuongezeka kwa changamoto ya mmomonyoko wa maadili na kupungua kwa uzalendo miongoni mwa vijana, hali inayochangiwa na upungufu wa malezi bora katika familia na jamii.
Kwa mujibu wa Maganya, baadhi ya vijana hujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na hatimaye kukumbwa na changamoto za afya ya akili, jambo linalohitaji hatua za pamoja za jamii na taasisi mbalimbali.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi ya CCM, Fadhili Maganya, akipanda miti katika eneo la ekari 6.5 lililoko kata ya Migungani, Wilaya ya Arumeru lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha VETA kusaidia vijana walioathirika na madawa ya kulevya. Picha na Bertha Ismail
Amesema pamoja na mafunzo ya ufundi, mradi huo pia utakuwa na kituo maalumu cha kuwahudumia vijana waliokumbwa na uraibu wa dawa za kulevya (sober house) ili wapate matibabu, malezi na ujuzi utakaowasaidia kurejea katika maisha ya kawaida.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Meru, Anankera Nanyaro, amesema wananchi wa Kata ya Migungani wamepokea kwa matumaini mpango huo kwa kuwa utasaidia kuimarisha maadili na kuwapatia vijana ujuzi wa kujitegemea kiuchumi.
Amesema eneo la mradi limetolewa na wananchi wa kata hiyo, huku wakitarajia pia kunufaika na fursa za ajira na vibarua wakati wa ujenzi na baada ya kukamilika kwa chuo hicho.
“Hii ni hatua muhimu katika kupambana na changamoto ya dawa za kulevya na kuhakikisha vijana wanakuwa tegemeo la maendeleo ya jamii,” amesema.
Naye mkazi wa Kata ya Migungani, Ana Nanyaro, amesema kuanzishwa kwa kituo hicho kutasaidia kupunguza tatizo la uraibu wa dawa za kulevya mkoani Arusha na kuwapa vijana nafasi ya kuanza maisha mapya.