Serengeti. Mahakama ya Rufaa imebatilisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyokuwa imetolewa dhidi ya watu wanne wa familia moja waliopatikana na hatia ya mauaji, baada ya kubaini kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa na mapungufu na utata uliotia shaka juu ya hatia yao.
Walioachiwa huru ni Yohana Tega, Seni Tega, Maganga Tega na Paulo Tega, waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Julai 31, 2023 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Mwandu Kwilasa.
Hukumu ya kuwaachia huru ndugu hao wa familia moja akiwemo baba na watoto wake, ilitolewa Machi 5, 2026 na jopo la majaji watatu la Mahakama ya Rufaa, ambao ni Ferdinand Wambali, Omar Othman Makungu na Agnes Mgeyekwa.
Jaji Mgeyekwa amesema baada ya kupitia mwenendo wa kesi na hoja za pande zote, mahakama ilikubaliana na baadhi ya hoja za warufani na kubaini kuwa kulikuwa na makosa katika namna ushahidi ulivyopokelewa na kutathminiwa.
Mahakama ilibainisha kuwa ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu ilisomwa mahakamani kabla haijapokelewa rasmi kama kielelezo, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuatwa wakati wa kupokea ushahidi wa maandishi.
Amesema utaratibu sahihi unataka hati iwasilishwe kwanza mahakamani na mahakama iamue kuhusu kukubalika kwake kabla haijasomwa hadharani.
Kutokana na kasoro hiyo, Mahakama ya Rufaa iliamua kuiondoa ripoti hiyo ya uchunguzi wa mwili wa marehemu katika ushahidi uliokuwa umetegemewa katika kesi hiyo.
Aidha mbali na kasoro hiyo, mahakama pia ilibaini kuwepo kwa utata katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka ambapo ilielezwa kuwa kulikuwa na tofauti katika maelezo kuhusu idadi ya washambuliaji waliodaiwa kushiriki katika tukio hilo.
Jaji alitolea mfano, shahidi mmoja alidai washambuliaji walikuwa 12, wakati mwingine alisema walikuwa 11 na pia kulikuwa na tofauti kuhusu muda wa tukio hilo, ambapo shahidi mmoja alisema shambulio lilidumu kwa dakika chache, huku mwingine akidai lilichukua hadi dakika 15.
Mahakama ilisema tofauti hizo si ndogo kwa kuwa zinahusu mambo muhimu ya tukio lenyewe na zinaweza kuathiri uaminifu wa ushahidi uliotolewa ambapo pia ilibaini kuwepo kwa mkanganyiko kuhusu nani hasa alianza shambulio hilo na nani aliyekuwa na silaha ya chuma wakati wa tukio.
Kuhusu utambulisho wa washambuliaji, mahakama pia ilitilia shaka ushahidi uliotolewa na mashahidi na kuwa ilibainika kuwa, rekodi iliyopo mahakamani haikuonyesha kuwa shahidi aliyedai kushuhudia tukio alitaja mara moja majina ya washambuliaji alipotoa taarifa yake ya kwanza.
Kutokana na mapungufu hayo pamoja na utata uliobainika katika ushahidi wa upande wa mashtaka, Mahakama ya Rufaa iliamua kuwa kesi dhidi ya warufani haikuthibitishwa bila shaka yoyote kama inavyotakiwa katika sheria za jinai.
Hivyo, mahakama ilifuta hukumu ya hatia pamoja na adhabu iliyokuwa imetolewa na Mahakama Kuu na kuamuru warufani waachiliwe huru mara moja.
Katika rufaa hiyo, warufani waliwasilisha sababu nne kuu za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.
Sababu hizo ni kupokelewa kimakosa kwa ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, kutokuwa wa kuaminika kwa ushahidi wa utambulisho wa shahidi wa pili, kuwepo kwa ushahidi unaopingana kutoka kwa mashahidi wa upande wa mashtaka na kushindwa kuthibitishwa kwa kesi dhidi yao bila shaka yoyote.
Awali, kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, siku ya tukio marehemu (Mwandu Kwilasa) alielekea kwenye shamba la familia akiwa pamoja na kaka yake, Paulo Kwilasa (shahidi wa pili), ambaye alikuwa akitembea mbele huku marehemu akiwa nyuma umbali wa mita 10.
Walipokaribia Mto Longa, shahidi huyo alidai aligeuka nyuma akamwona ndugu yake akiwa amezungukwa na kundi la takriban wanaume 12.
Alidai kuwatambua watu hao kuwa ni Paulo Tega, Yohana Paulo Tega, Seni Tega, Maganga Tega, Sosoma Masanja, Paulo Sosoma, Jisandu Masanja, Kumbila Masanja, Machia Sosoma, Mussa Sosoma na Nyimba Masanja.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, watu hao walikuwa na fimbo, vyuma na mpini vya jembe, na walimshambulia marehemu huku akidai kuona Sosoma Masanja akianzisha shambulio hilo huku wengine wakijiunga.
Kutokana na hofu shahidi huyo alidai kukimbia na kwenda kutoa taarifa kwa baba yake, Nyahiti Kwilasa (shahidi wa tatu), ambaye alimkuta nyumbani kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikonda, Jidai Myimbi (shahidi wa nne).
Shahidi wa tatu alidai kuwa wakati huo alikuwa ameenda nyumbani kwa mwenyekiti wa kijiji kutoa taarifa kwamba baadhi ya wanakijiji walikuwa wameenda kulisha ng’ombe katika shamba lake.
Amesema waliposikia kelele za wito walielekea eneo la tukio pamoja na wanakijiji wengine na walipofika aliona kundi la watu 11 wakimpiga marehemu.
Alidai kuwatambua baadhi yao kuwa ni Paulo Tega, Yohana Tega, Seni Tega, Maganga Tega, Sosoma Masanja, Paulo Sosoma, Jisandu Masanja, Kumbila Masanja na Nyimba Masanja, na kwamba Paulo Tega alikuwa akimpiga marehemu kwa chuma.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, shambulio hilo lilidumu kwa takriban dakika 15 kabla washambuliaji kutawanyika.
Shahidi wa nne, alidai kuwa ingawa hakushuhudia shambulio hilo moja kwa moja, alipewa taarifa kuhusu waliohusika na baadaye aliwaagiza wanamgambo kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa.
Shahidi wa kwanza, Dk Machunde Mtani, aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, alieleza kuwa aliufanyia uchunguzi Desemba 24, 2021 na kubaini kuwa ulikuwa na majeraha mengi makubwa.
Katika utetezi wake, mrufani wa kwanza alidai kuwa alikamatwa na mgambo na kupelekwa kituo cha polisi na akahusisha kukamatwa kwake na mgogoro wa ardhi uliokuwepo kati ya familia yao na ile ya marehemu.
Mrufani wa pili alidai kukamatwa kwao kulitokana na mgogoro huo wa ardhi na si tukio la shambulio, huku mrufani wa tatu akithibitisha maelezo hayo ya shahidi wa pili.
Kwa upande wake, mrufani wa nne alidai kuwa siku ya tukio alikuwa nyumbani kwake pamoja na wanawe wawili (mrufani wa pili na tatu) wakati mrufani wa kwanza alikuwa akichunga ng’ombe.
Amedai aliposikia kelele, wanawe walikimbilia eneo la tukio na yeye aliwafuata baadaye. Alipofika alikuta umati mkubwa wa watu na baadaye akagundua kuwa wanawe tayari walikuwa wamekamatwa wakihusishwa na shambulio hilo.
Alidai kutokana na wasiwasi juu ya usalama wao, alisafiri hadi Shinyanga kufuatilia suala la kukamatwa kwao na baadaye Julai 2022 alikamatwa na mgambo na kuhojiwa na Ofisa Mtendaji wa kijiji kuhusu mahali alikokuwa.
Alieleza kuwa alikuwa Shinyanga akifuatilia kesi ya wanawe na kusisitiza kuwa hakuwa na mgogoro binafsi na marehemu, akidai mvutano uliokuwepo ulihusiana na mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya baadhi ya wanakijiji na familia ya marehemu.