Malalamiko ya wananchi Nkasi yamfikia Dk Mwigulu, aagiza hatua

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewaagiza mawaziri kuweka utaratibu wa kisheria ili watu wanaoajiriwa na makandarasi wanaopewa kazi na Serikali walipwe moja kwa moja na Serikali, tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi ya wananchi wanadhulumiwa fedha zao.

Maagizo hayo ya Dk Mwigulu ameyatoa leo Jumatatu, Machi 9, 2026 ni kufuatia malalamiko ya wananchi wa Nkasi mkoani Rukwa kudhulumiwa na makandarasi wanaowapa vibarua kwa kuzungusha malipo licha ya Serikali kutodaiwa na makandarasi hao.

Dk Mwigulu ambaye yuko mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi, baada ya kusikiliza kero ya wananchi hao amesema kumekuwepo utaratibu ambapo makandarasi wanapewa kazi, wanalipwa fedha zao na Serikali lakini hawalipi fedha kwa watu waliowapa kazi.

Kutokana na hilo, amesema Serikali inalalamikiwa na wananchi wakati mkandarasi ameshalipwa fedha zake.

“Ona huyu kijana amefanya kazi, Serikali ilishalipa hela zote, anatokea mtu anamfanyisha kazi bure. Haya mambo hayakubaliki ni wizi kama wizi mwingine. Mawaziri nataka muweke kwenye sheria jambo hili, ikiwezekana makandarasi wanapolipwa fedha zao, fedha ambazo si zao walipwe moja kwa moja wahusika,” amesema.

Dk Mwigulu amesema kitendo cha watu kufanyishwa kazi bila kulipwa ni kuwatia umaskini, akisisitiza makandarasi wa nje wanapocheleweshwa malipo yao huongeza riba lakini wao hawalipi fedha za watu wanaowafanyisha kazi, akisema huo ni wizi.

Mwananchi Patrick Mwanamboo akizungumza mbele ya Waziri Mkuu amelalamika kufanya kazi ya ujenzi wa msingi wa bweni kwa Sh2 milioni na tayari amelipwa Sh1.8 milioni, huku laki mbili zikibaki tangu mwaka jana.

Pia, amesema alijenga majosho manne lakini hadi sasa hajalipwa fedha zake na mkandarasi huyo hapatikani kwenye simu na akipatikana hapokei simu zake.

Changamoto kama hiyo imelalamikiwa pia na mkazi wa Paramawe aliyejitambulisha kwa jina la Justin akisema kampuni ya Genereal Power na Live Sport iliwapa kazi ya kulinda vifaa wakati wa utekelezaji wa mradi wao kwa miaka mitatu iliyopita kwa mkataba wa Sh100,000 lakini hawakuambulia chochote.

Amesema baada ya mradi wao kukamilika walihifadhi vifaa vyao katika ofisi ya Tanesco  (Shirika la Umeme Tanzania) mkoani humo na baadaye walirejea kuvichukua.

Amedai kuwa licha ya juhudi zao za kuzuia vifaa hivyo kutochukuliwa na mkandarasi huyo hadi walipwe, ilishindikana.

Baada ya hatua hiyo kufeli, amesema waliahidiwa kulipwa na kuambiwa wafungue akaunti benki lakini hakuna chochote walichopata licha ya kuzungushwa mara kwa mara.

Katika hilo, Dk Mwigulu ameagiza mkandarasi huyo kusakwa alipo na ofisi yao ipatikane.

“Kamanda msake huyu popote alipo alipe hizi fedha kwa sababu Serikali ilishalipa. Kama halipi asilete longolongo, kamata weka ndani hadi alipe hizo fedha.”

Mwananchi mwingine ambaye hakujitambulisha jina alilalamikia kutolipwa kifuta jasho tangu mwaka 2019 baada ya tembo kuingia kwenye makazi yao na kuharibu mazao.

Amesema mtendaji wa kijiji alipeleka malalamiko yao kwa maliasili na timu ya askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) walitumwa kufanya uchunguzi na kubaini kuwa eneo lililovamiwa na wanyama halikuwa chini ya hifadhi.

Tangu wakati huo hadi sasa amesema hawajalipwa wala kupewa taarifa zozote kuhusu malipo yao na wamekuwa wakizungushwa bila kupewa majibu.

“Mwaka jana tukapewa taarifa kuwa hizo fedha zitalipwa na mtendaji wa kata,” amesema.

Akijibu hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande amesema kuna changamoto ya wanyama wakali na waharibifu katika ushoroba unaotokea Katavi, Kalembo hadi Zambia.

“Wako wananchi 358 walipata changamoto ya kuharibiwa mazao yao na tayari Serikali imelipa Sh64 milioni kwa wananchi hao hadi Februari. Hivi karibuni Sh108 milioni kwa watu 418 watalipwa fedha zao na huenda mwananchi huyo atalipwa. Wote waliopata athari watalipwa kifuta machozi na Serikali.”

Amesema kwa upande wa Ziwa Tanganyika, Serikali ilikuwa na lengo la kujenga vizimba vinne na tayari viwili vimejengwa kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa ziwa hilo ili kuwanusuru na mamba.

Naibu Waziri huyo amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuishi vyema na majirani pamoja na kutumia mbinu mbalimbali kuwarejesha wanyama katika maeneo yao.

Vilevile amesema Serikali hivi karibuni inakwenda kujenga uzio wa umeme kuanzia Kabwe hadi Masolo na iko tayari kufanya kazi na wananchi hao.