Mama mwenye nyumba agundua mwili wa mpangaji uliofukiwa chumbani

Kilosa. Mwili wa Lilian Danstan (27) umegundulika umefukiwa chumbani ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi na mpenzi wake katika Kijiji cha Changarawe, Wilaya ya Kilosa.

Kufuatia tukio hilo, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa kushirikiana na maofisa afya pamoja na taasisi nyingine leo, Machi 9, 2026 wamefanikiwa kuufukua.

Mwili huo umegundulika baada ya mama mwenye nyumba kwenda kufanya usafi katika nyumba hiyo, iliyokuwa imefungwa kwa zaidi ya miezi miwili tangu Lilian alipotoweka, katika mazingira ya kutatanisha.

Maofisa afya wilaya ya Kilosa wakiutoa mwili wa Lilian Danstan aliyeuawa na kufukiwa ndani ya nyumba katika kitongoji cha kipera kijiji cha Changarawe kata ya Masanze wilaya ya Kilosa, Morogoro. Picha Hamida Shariff



Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, Lilian alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtuhumiwa ambaye anatafutwa na kwamba walikuwa wakiishi pamoja kama mke na mume.

Hata hivyo, amesema Jeshi la Polisi limeshaanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiuchunguzi, hivyo amewataka wananchi kuonesha ushirikiano katika kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali ya kijiji na polisi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, amethibitisha kutokea kwa mauaji na kuwataka wananchi wa kijiji hicho na wilaya nzima kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi katika kutoa taarifa zitakazosaidia kumtafuta mtuhumiwa.

“Hakuna shaka Lilian ameuawa kwa sababu amefukiwa ndani ya nyumba. Kazi yetu sasa ni kuhakikisha wahusika wanakamatwa haraka ili sheria ichukue mkondo wake.”

Marehemu Lilian Danstan (27) enzi ya uhai wake.



Amebainisha kuwa hilo ni tukio la pili wilayani humo ndani ya miaka miwili, akitaja tukio la awali la mwanamke mwingine kuuawa na mtu anayedaiwa kuwa mume wake.

Shaka ameongeza kuwa, matukio haya ni ya kikatili na yasiyokubalika, na kuwataka wananchi kutoa taarifa ili wahusika wapatikane haraka.

Mwili wa Lilian uligundulika baada ya mama wa mwenye nyumba kwenda kufanya usafi katika nyumba hiyo, iliyokuwa imefungwa kwa zaidi ya miezi miwili tangu mwanamke huyo alipotoweka, katika mazingira ya kutatanisha.

Akisimulia namna alivyogundua tukio hilo, mama  mwenye nyumba aliyejitambulisha kwa jina la Maria Joram amesema baada ya Lilian kutoweka pamoja na mume wake nyumba hiyo ilifungwa na kukaa muda mrefu.

Maria amesema ilipofika Juzi Machi 7, 2026  alipokwenda kufungua mlango kwa ajili ya kufanya usafi, ndipo alipokuta kifusi chumbani ambacho kilifunikwa na kipande cha godoro.

“Nilikuja kufanya usafi ili niishi kwenye nyumba hii ya mwanangu baada ya kukaa muda mrefu bila ya kukaliwa na mtu, nilianza kufanya usafi nje kwa kulima majani na baadaye nikaingia ndani na kuanza kufagia.

“Nilipofika chumbani nikakuta kifusi cha udongo mithiri ya tuta, kikiwa kimefunikwa na kipande cha godoro nikampigia simu mwanangu na mara moja akaja na kuanza kusawazisha kile kifusi na ghafla ndipo tulipoona sehemu ya kichwa na mkono wa binadamu,” amesema Maria.

“Baada ya kuona viungo vile vya binadamu tukapata wasiwasi na kwa kuwa tayari tulishasikia kuwa Lilian amepotea basi tukahisi huwenda ndio yeye aliyefukiwa, tukatoa taarifa Serikali ya kijiji na baadaye polisi walikuja na wataalamu wao na kugundua kuwa ni mwili wa binadamu.”

Mama wa Liliana Danstan aliyeuawa na kufukiwa ndani ya nyumba akilia mara baada ya mwili wa mwanae kufukiwa katika nyumba hiyo aliyokuwa akiishi na mwanaume wake. Picha Hamida Shariff



Amesema awali alipotoweka binti huyo, mwanaye pamoja na familia walitoa taarifa sehemu mbalimbali, lakini hawakuweza kumpata.

Akieleza tukio hilo baada ya kazi ya ufukuaji iliyochukia zaidi ya saa mbili, baba mzazi wa Lilian aliyejitambulisha kwa jina la Danstan Manga amemtaja mwanamume huyo aliyekuwa akiishi na binti yake kuwa ni Khalid Mavuze na kwamba walikuwa wakiishi kinyumba kwa zaidi ya miezi mitatu kabla ya tukio hilo la mauaji kutokea.

Manga amesema mara ya mwisho binti yake alionekana kijijini hapo Desemba 11 mwaka jana na baada ya hapo hakuweza kuonekana tena na kwamba jitihada mbalimbali za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio.

Amesema ilipofika Machi 8 mwaka huu ndipo alipopata taarifa kuwa binti yake ameuawa na kufukiwa ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi na mwanaume huyo.

“Binti yangu hakuwa na mume na mimi sikuwa nafahamu undani wa maisha ya binti yangu na huyo mwanaume kwa sababu hakuwahi kumleta nyumbani kumtambulisha.

“Alipoondoka nyumbani kwenda kuishi na mwanamume huyu (mtuhumiwa) aliwaacha watoto wake wawili pale nyumbani, nilimshauri sana kuhusu suala la kumleta mwanamume wake huyo nyumbani kujitambulisha lakini haikuwezekana,” amesema Manga.

Nyumba aliyokuwa akiishi Lilian Danstan (27) aliyeuawa na kufukiwa ndani ya nyumba hiyo katika kitongoji cha kipera kijiji cha Changarawe kata ya Masanze wilaya ya Kilosa. Picha Hamida Shariff



Akieleza tabia ya binti yake, Manga amesema hakuwa na ugomvi na mtu na alikuwa akifanya shughuli zake ndogondogo za kilimo na hakuwahi kufika kwenye nyumba hiyo aliyokuwa akiishi na mwanaume huyo.

Ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kumsaka mtuhumiwa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Mmoja wa majirani hao Pili Rashid amesema Lilian alikuja hapo kufuatia mwanamume ambaye ndiye alikuwa mpangaji katika nyumba hiyo na kwa kuwa aliishi kwa muda mfupi hawakuweza kugundua jambo lolote baya lililoashiria kuhatarisha maisha.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kipera, Shaibu Samata amesema baada ya binti huyo kutoweka miezi miwili na nusu iliyopita walitangaza maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusambaza picha yake vijijini kwenye vijiwe vya bodaboda, kwenye mitandao ya kijamii lakini hawakuweza kutoa taarifa polisi.

“Binti huyu katika uhai wake aliondoka hapa kijiji na kwenda maeneo mbalimbali kutafuta maisha hivyo tuliamini huwenda yupo kwenye shughuli za utafutaji na ipo siku atarudi kama anavyorudi.

“Tukio hili limetushtua na kutuhuzunisha, kikubwa tumeanza kupata hofu juu ya mabinti zetu dhidi ya vijana wa kiume wanaokuja hapa kijiji kwa ajili ya kutafuta wachumba,” amesema Samata.