MASHINDANO YA QURAN KUZIKUTANISHA NCHI 26 DUNIANI KUFANYIKA MAC 31 TANZANIA

I

****

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, amesema mashindano ya Quran yanayotarajiwa kufanyika nchini ni sehemu ya ushirikiano kati ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Wizara ya Dini ya Saudi Arabia.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuhamasisha na kuendeleza usomaji wa Quran kwa Waislamu, huku pia ukitoa fursa kwa wasomaji kuonesha vipaji vyao.

Akizindua rasmi tuzo za mashindano hayo, Sheikh Zubeir alisema awali yalipangwa kufanyika ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir akimzungumza Wakati akizindua mashindano ya Quran.

Hata hivyo, alieleza kuwa yameahirishwa hadi baada ya Ramadhani ili kuruhusu waumini wengi zaidi kushiriki na kufuatilia mashindano hayo.

Alisema mashindano hayo yataanza Machi 31, 2026 na kumalizika Aprili 5, 2026.

Sheikh Zubeir alikumbusha kuwa Quran ni mwongozo muhimu wa maisha ya Muislamu kila siku na katika miezi yote ya mwaka.

Alisisitiza kuwa Waislamu wanapaswa kuendelea kuisoma na kuzingatia mafunzo yake katika maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tuzo za mashindano hayo, Othman Kaporo, alisema mwaka huu mashindano hayo yatashirikisha washiriki na wageni kutoka nchi 26.

Mwenyekiti wa tuzo za mashindano hayo, Othman Kaporo.

Alisema hali hiyo inatarajiwa kuongeza ushindani pamoja na kuipa hadhi kubwa zaidi hafla hiyo ya kimataifa.

Kaporo aliongeza kuwa tukio hilo litahudhuriwa pia na maimamu kutoka Masjid al-Haram na Al-Masjid an-Nabawi, watakaokuja maalum kushiriki na kuhamasisha mashindano hayo.

Aidha, amesema washiriki watashindania zawadi ya jumla ya dola za Marekani 30,000.

Alifafanua kuwa zawadi hizo zitatolewa kwa washindi wa makundi ya watoto na watu wazima kulingana na utaratibu maalum utakaotangazwa na waandaaji.