Dar es Salaam. Kamishna wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila ametaja sababu za kuchelewa kwa ujenzi wa barabara ya kulipia ya Chalinze hadi Morogoro ikiwamo kampuni zilizoomba zabuni hiyo kutokidhi vigezo.
Kafulila amesema hayo wakati akijibu hoja ya Alphonce Temba aliyehoji ni lini mradi wa barabara hiyo unaotarajiwa kugharimu Sh2 trilioni utaanza baada ya matamko ya muda mrefu.
Ameibua hoja hiyo katika kongamano la kujadili nafasi ya PPP katika kufanikisha mpango wa maendeleo ya Taifa lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo Machi 9, 2026.
Akieleza mkwamo wa mradi huo, Kafulila amesema licha ya kuchelewa, ni mradi muhimu katika usafirishaji nchini na Serikali ilifanya upembuzi yakinifu kwa kutumia Kampuni ya Korea na Afrika Kusini kabla ya kupelekwa sokoni ili kampuni zishindane.
Amesema baada ya kufika sokoni kampuni tisa zilizoonesha nia ya kufanya huo mradi ulioanza kuzungumzwa tangu mwaka 2017 huku nane zikiwa za China, moja ya Uturuki na hakukuwa na hata moja ya Tanzania wala Afrika.
“Si jambo la ajabu kwani ni uhalisia wa dunia kuwa miradi inayohitaji mtaji mkubwa kampuni zinajichuja zenyewe na hakukuwa hata na kampuni yoyote kutoka Bara la Afrika,” amesema.
Pia, amesema baada ya mchujo zilibaki tano lakini nne zilikuwa za China na moja ya Uturuki huku tatu bora kati ya hizo zilibaki za China.
Amesema kati ya hizo tatu, kampuni mbili zilishindwa kuwasilisha nyaraka muhimu na ikabaki moja pekee ya SBRG; majadiliano yalipoanza hakukuwa na mbadala kuwa, akikosekana huyo atapatikana mwingine.
“Hiyo ndiyo sababu ya majadiliano haya kuchukua muda mrefu, hakukuwa na kampuni namba mbili ambayo unaweza kuichukua kama mbadala huyu mmoja asipokidhi vigezo, nyingine zilishindwa kukidhi vigezo vya kuleta nyaraka za manunuzi ya mradi huo,” amesema.
Amesema jambo lingine lililoweka ugumu ni gharama ya kutekeleza na uendeshaji zilizokuwa zimeainishwa walipokuwa wakilinganisha zile zilizotumiwa awali na Serikali na walizotaja wao.
“Kazi ambayo sisi tulifanya haikuwa inazidi Dola 560 milioni, lakini mwekezaji alikuja na gharama ya Dola zaidi milioni 900. Kwa kuwa ni tofauti kubwa, ikabidi kamati inayofanya makubaliano haya kuingia ndani kuangalia mchanganuo wa gharama, baadhi ya vitu gharama zake zimekuzwa, hivyo ikaonekana hakuna namna ya kuendelea na mwekezaji huyo,” amesema.
Kafulila amesema hali hiyo imefanya mchakato wa mradi huo kuanza upya wakati ambao uhitaji wa barabara hiyo unazidi kuongezeka. “Matarajio yetu yalikuwa, tungeweza kufikia makubaliano hayo huenda ujenzi mwaka jana ungeanza.”
Aidha, amesema kutokana na umuhimu wake katika uchumi, Waziri Mkuu na Wizara ya Ujenzi waliingilia na kuweka muundo mpya na wawekezaji wengine.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ameeleza kuwa ili kufikia lengo la uchumi wa Dola 1 trilioni za Marekani mwaka 2050 Serikali imeandaa mpango wa nne wa maendeleo wa miaka mitano kati ya mwaka 2026/27 na 2030/31.
Katika huo mpango huo, Serikali imepanga kutekeleza malengo manne makubwa yatakayoiwezesha nchi kuwa na mwelekeo mzuri kuelekea 2050.
“Kwanza, tumelenga kuimarisha utulivu wa uchumi na kuchochea mageuzi ya kimfumo yatakayochochea ukuaji wa sekta binafsi kama injini ya ukuaji wa uchumi,” amesema Profesa Mkumbo.
Ameeleza kuwa, mwaka 2024, uchumi ulikua kwa asilimia tano, mwaka 2025 ukakua kwa asilimia 6, mwaka huu inatarajiwa utakua kwa asilimia kati ya 6.2 hadi 6.3, ifikapo 2028/29 ukue kwa asilimia zaidi ya saba.
“Lakini tumejiwekea lengo kuwa, kufikia 2031 uchumi wetu ukue kwa asilimia 10.5. Huu ni ukuaji mkubwa na tutahakikisha mfumuko wa bei wa Taifa unadhibitiwa na deni la Taifa kuwa stahimilivu,” amesema.
Pia, amesema Serikali imepanga kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji na mifumo wezeshi ya biashara huku ikihakikisha mageuzi katika sekta za uzalishaji ili kuzalisha ajira na kuongeza thamani na uwezo wa kushindana kama nchi katika kuuza bidhaa nje ya nchi.
Ili kuyatimiza malengo hayo, Profesa Mkumbo amesema ikifika 2031 zinahitajika Sh477.7 trilioni (Dola 183 bilioni), huku Serikali ikitegemea asilimia 70 ya fedha hizo zitoke sekta binafsi.
“Tunaamini pasi na shaka kuwa, ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ni muhimu katika kufikia malengo haya tuliojiwekea na ndio maana kwa kuliona hilo, Serikali imehuisha Sera ya PPP ya 2009 na kuunda sheria ya kusimamia mchakato huu,” amesema.