Migogoro ya ardhi na mirathi inavyowatesa wananchi

Tanga. Imeelezwa kuwa, migogoro ya ardhi na mirathi imeendelea kuwa chanzo cha malalamiko kwa wananchi nchini, hali iliyosababisha maelfu ya watu kutafuta ushauri kupitia kliniki za sheria zinazoendeshwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kupitia kliniki hizo, mawakili hushughulikia mashauri mbalimbali kwa kutoa ushauri wa kisheria na kuelekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili wananchi wapate haki zao.

Huduma hiyo inalenga kusogeza huduma za kisheria karibu na wananchi ili kuwasaidia kuelewa haki zao na namna ya kuzitetea pindi zinapokiukwa.

Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Simiyu waliojitokeza wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki mkoani huo latika mjini Bariadi. Picha na Samwel Mwanga.



Akizungumza leo Jumatatu, Machi 9, 2026 Mkurugenzi wa Uratibu wa Huduma za Ushauri, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Neema Ringo wakati wa uzinduzi wa kamati za ushauri wa kisheria na kliniki ya sheria mkoani Tanga, amesema katika mikoa saba waliyoizungukia kutoa huduma hizo, wananchi 8,680 wamejitokeza kuwasilisha changamoto zao za kisheria.

Amesema migogoro ya ardhi na mirathi inaongoza kwa wingi wa malalamiko.

Mikoa ambayo wameshapita ni Dodoma, Manyara, Singida, Simiyu, Kilimanjaro, Mwanza na Dar es Salaam iliyoongoza kuwa na migogoro mingi ya ardhi na mirathi na walisikiliza mashauri 544.

Ringo amesema kupitia huduma hiyo mawakili wa Serikali na wa kujitegemea, wamekuwa wakisikiliza kero za wananchi na kuwasaidia kupata majawabu.

Baadhi ya wanawake wa mkoa wa Dodoma wakipatiwa huduma ya upataji wa hati za umiliki wa ardhi jijini humo.



“Katika mikoa saba tuliyopita, tumekutana na wananchi waliofika kuwasilisha changamoto zao za kisheria. Kero nyingi zilihusu migogoro ya ardhi na mirathi, ambazo zimekuwa zikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu,” amesema Ringo.

Amesema mawakili wa Serikali wanaotekeleza majukumu yao katika taasisi mbalimbali za umma hufanya kazi chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ringo amesema Ibara ya 59 ya Katiba inampa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  jukumu la kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria, huku Ibara ya 8 ikisisitiza kuwa, Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ambako mamlaka ya Serikali yanatokana na wananchi.

“Kwa msingi huo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeona umuhimu wa kuanzisha kliniki za sheria ili kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwasaidia kupata haki zao,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amesema migogoro ya wananchi inapaswa kutatuliwa katika ngazi za mkoa na wilaya badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa wanapopita ndipo wananchi watoe malalamiko yao.

Amesema kuanzishwa kwa kamati hizo kutasaidia kusikiliza na kutatua kero za kisheria za wananchi mapema kabla hazijafika katika ngazi za juu za uongozi.

Wanawake jijini Tanga wakisubiria huduma kukamilika  kwenye mtandao  kwa ajili ya kupatiwa hati zao za kumiliki ardhi kwenye Samia Ardhi Kliniki  ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha wiki ya wanawake duniani. Picha na Mbonea Herman



“Ni muhimu sana migogoro ya wananchi ikatatuliwa huku huku kwenye maeneo yetu, si vizuri wananchi kusubiri hadi viongozi wa kitaifa wanapokuja ndipo waanze kueleza kero zao. Tunapaswa kuwa na mifumo ya kusikiliza na kutatua changamoto hizo hapa hapa,” amesema Dk Batilda.

Dk Batilda amesema mara nyingi viongozi wa mkoa hupokea malalamiko ya migogoro mbalimbali kutoka kwa wananchi, lakini wakati mwingine huhitaji ufafanuzi wa kisheria ili kupata suluhisho sahihi.

Amesema kupitia kamati hizo, mawakili wa Serikali kutoka sekta tofauti wataweza kushirikiana kutoa ufafanuzi na mwongozo wa kisheria utakaosaidia kutatua migogoro hiyo.

Hata hivyo, amesema baada ya kliniki hiyo kumalizika, mawakili wataanza kushuka katika wilaya na kata mbalimbali za Mkoa wa Tanga kuwasikiliza wananchi moja kwa moja na kuwasaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zao za kisheria.

“Kuanzia Jumatano ijayo timu hizi zitakwenda katika maeneo mbalimbali ya mkoa na wilaya na watashuka hadi katika kata zote kwa kukutana na wananchi, kusikiliza na kutatua kero zao ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba amesema kero nyingi ambazo wamekuwa wakipokea ni ardhi na mirathi, hivyo uwepo wa kliniki ya sheria na kamati zake zitasaidia kuondoa kero hizo.

“Jambo kubwa tunalokutana nalo ni migogoro ya ardhi pamoja na mirathi, kwa hiyo kuja kwa kamati hizi tunaona ni mkombozi mkubwa,”amesema Kolimba.