Musoma. Watu 38 ambao miongoni mwao walikuwepo viongozi, makada na wafuasi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokuwa wanashikiliwa na Polisi mkoani Mara, kwa madai ya kufanya vurugu na kuzua taharuki mjini Musoma wameachiwa kwa dhamana.
Watu hao akiwamo Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Pamela Massay walikamatwa mjini Musoma jana Jumapili, Mei 8, 2026 ikiwa ni katika jitihada za Jeshi la Polisi kuzuia maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyopangwa kufanyika kitaifa mjini Musoma chini ya uratibu wa Bawacha.
Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi na wanachama wa Bawacha waliokuwa wanajaribu kukusanyika kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Machi Mosi, 2026, baraza hilo lilitangaza kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika Kanda ya Serengeti, mkoani Mara, na kuwakutanisha wanawake wa chama hicho cha upinzani nchini.
Hata hivyo, Machi 7, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, alitangaza marufuku ya kufanyika kwa tukio hilo.
Katika tangazo lake, Kamanda Lutumo alisema Bawacha haitaruhusiwa kufanya tukio hilo kwa kuwa linakwenda kinyume na amri ya Mahakama iliyokitaka chama hicho kisimamishe kufanya shughuli za kisiasa hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika mahakamani.
Kutokana na tangazo hilo, misafara ya magari ya wanawake wa Bawacha ilizuiwa maeneo mbalimbali kabla ya kufika Musoma na mingine ikizuiwa kabla ya kuanza safari.
Waliokuwa Musoma na kutaka kufanya maadhimisho jana walijikuta wakitawanywa na Polisi kwa mabomu ya machozi. Baadhi walijikuta mikononi mwa jeshi hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Machi 9, 2026, Mwenyekiti wa Bawacha Jimbo la Musoma Mjini, Renatha Rafael amesema watu hao waliachiwa jana Jumapili saa 3 usiku.
Amesema baada ya wanasheria wa chama kukamilisha taratibu zote watu hao waliachiwa bila masharti yoyote na tayari wengine wameanza safari kurejea makwao.
“Jumla ya watu tuliowatoa ni 38, wanawake wakiwa ni 31 na wanaume wakiwa saba, baada ya wanasheria kukamilisha kila kitu polisi walituambia watu hao watatakiwa kuripoti polisi leo lakini baadaye wakasema waondoke tu,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Donald Mwembe akizungumza na wanachama hao jana baada ya kuachiwa aliwapa pole na kulipongeza baraza hilo la wanawake ambapo amesema licha ya changamoto walizokutana nazo hawakurudi nyuma, badala yake walishikilia msimamo wao hivyo kuiheshimisha taasisi yao.
“Ndio mmeiheshimisha taasisi katika siku ya mwanamke duniani, Mungu aendelee kuwatia nguvu katika mapambano tuliyonayo,” amesema.
Amesema baadhi yao walitoka sehemu mbalimbali za nchi kuja mjini Musoma kushirikiana pamoja katika siku ya wanawake duniani na pamoja na vitisho vyote vya mabomu ya machozi bado waliendelea kulinda na kuiheshimisha taasisi yao.
Amesema mahabusu ya polisi ilikuwa ni sehemu ya kuwakomaza katika hitajio la kusimamia haki na kuwataka waendelee na moyo huohuo wa kupigania haki za Watanzania.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo alisema watu hao walikamatwa kwa tuhuma za kufanya vurugu na kuzua taharuki katika mji wa Musoma kinyume cha sheria.
Alisema ya baadhi ya wajumbe wa Bawacha baada ya kumaliza ibada katika Kanisa Kuu la Katoliki Mjini Musoma waliungana na vikundi vya vijana na kuanza kufanya vurugu, na kusababisha taharuki iliyosababisha watumiaji wa barabara mjini Musoma kuanza kukimbia hovyo.
Alieleza chanzo cha vurugu hizo ni kufuatia Bawacha kuandaa maadhimisho ya siku ya wanawake waliyotarajia kuyafanya mjini Musoma tukio ambalo jeshi hilo lilipiga marufuku kwa maelezo ni kinyume cha sheria hasa ikizingatiwa kuhusu uwepo wa katazo la mahakama kuhusu Chadema kujihusisha na siasa hadi kesi ya msingi iliyopo mahakamani itakapomalizika.
“Katazo letu lilikuwa la kisheria na lilizingatia matakwa ya kisheria na athari ambazo zingetokea endapo wangefanya maadhimisho hayo mkoani Mara,” alisema.