……………
Na Saidi Lufune, Rukwa
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amesema Serikali inaendelea kulinda maisha ya wananchi dhidi ya uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu hususan Tembo na Mamba kwa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguuka Hifadhi
Mhe. Chande amebainisha hayo katika Halmashauri wa Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ikiwa ni mwendelezo wa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo sambamba na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi.
Mhe. Chande amebainisha kuwa Wilaya hiyo inapakana na Ushoroba wa Katavi – Lwafi – Kalambo – Zambia hivyo husababisha baadhi ya vijiji kukumbwa na kadhia ya wanyamapori kutoka katika ushoroba huo na kuvamia maeneo ya kilimo na makazi ya wananchi kwenye Wilaya hiyo
Amesema kutokana na kadhia hiyo, Serikali imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wanakuwa salama pamoja na mali zao ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria, kutoa elimu ya namna ya kujihami na wanyamapori hao; ujenzi wa vizimba pembezoni mwa Ziwa Tanganyika na matumizi ya teknolojia za aina mbalimbali ikiwemo vilipuzi na ndege nyuki kufukuza tembo na kuwarudisha katika maeneo ya hifadhi sambamba na mpango wa ujenzi wa uzio wa umeme kutoka Kabwe hadi Masolo ili kuzuia wanyamapori wasitoke nje ya eneo la hifadhi.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kulipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wananchi walioathirika ambapo hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, zaidi ya shilingi Milioni 64 zimelipwa kwa wananchi hao huku ikitarajia kulipa kiasi cha Shilingi Milioni 108 kwa waathirika wengine wa matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ili jamii iendelee kuwa na mtazamo chanya kuhusiana na Uhifadhi.





