Shule Ya Msingi Kiromo Yakarabatiwa Kwa Ufadhili Wa Airtel

Bakari Mahundu
March 9, 2026
0 Comments

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, Charles Kamoto, ametembelea Shule ya Msingi Kiromo kukagua maendeleo ya mradi wa ukarabati unaofadhiliwa na kampuni hiyo, wenye lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na walimu.

Katika ziara hiyo, viongozi wa Airtel walipata taarifa ya hatua za ukarabati wa miundombinu ya shule, unaolenga kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora na salama ya kusomea.

Akizungumza wakati wa ziara, Mkuu wa Sheria na Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, amesema kampuni itaendelea kusaidia sekta ya elimu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii.

Amesema pamoja na ukarabati unaoendelea, Airtel itatoa meza 250 mpya ili kupunguza changamoto ya uhaba wa samani madarasani na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Uongozi wa Shule ya Msingi Kiromo umeishukuru Airtel Tanzania kwa msaada huo, ukieleza kuwa maboresho ya miundombinu na upatikanaji wa vifaa yataongeza ari ya wanafunzi kusoma na kufikia malengo yao ya kielimu.

Stori Na Richard Bukosi, GPL