Teknolojia ya tiba mwanga inayopambana na magonjwa sugu

Dar es Salaam. Tiba mpya inayotumia mwanga maalumu inayojulikana kama phototherapy imeanza kuibua matumaini mapya kwa wagonjwa wa magonjwa sugu, ikiwamo kisukari, shinikizo la damu na matatizo ya figo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, phototherapy ni aina ya matibabu yanayotumia mawimbi maalumu ya mwanga kuchochea mwili kuanza mchakato wa kujirekebisha na kupona.

Teknolojia hii inaingia nchini wakati ambapo mfumo wa afya wa Tanzania unakabiliwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).

Tiba hiyo tayari imekuwa ikitumika katika mifumo ya afya ya nchi zilizoendelea, hususan kutibu homa ya manjano kwa watoto wachanga na baadhi ya magonjwa ya ngozi kama psoriasis na eczema.

Huduma hiyo nchini inatolewa na Dk Samson Magesa, baada ya kufanya utafiti uliochochewa na changamoto alizokutana nazo wakati akifanya kazi hospitalini.

Takribani muongo mmoja uliopita, Dk Magesa alipokuwa akihudumu katika wodi za Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, alishuhudia wagonjwa wengi wa kipato cha chini wakirudi hospitalini mara kwa mara wakiwa na matatizo yaleyale ya kiafya.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Dk Magesa amesema hali hiyo ilimfanya aanze kutafakari uwezekano wa kuwepo njia mbadala za kusaidia wagonjwa zaidi ya matibabu ya kawaida.

“Nilijiuliza kwa nini watu wetu wanaendelea kuteseka na magonjwa ambayo yanaweza kudhibitiwa kwa njia salama zaidi na zisizo na maumivu makali. Swali hilo ndilo lililonisukuma kuanza safari ya utafiti,” amesema Dk Magesa ambaye ni mwanzilishi wa Kampuni ya Lifewave Tanzania Limited.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa tiba, kutoka wizara ya afya, Dk Hamad Nyembea, phototherapy inatumika katika tiba kama vile kuponesha manjano kwa watoto.

“Ni kweli hii ni moja ya aina ya matibabu yanayotumika kwa baadhi ya magonjwa kama ya watoto kwa kutumia mionzi ya jua. Hivyo kama wataalamu wameamua kujikita katika matibabu haya ni vyema watu wakafahamu kuwa sio kila ugonjwa unatibiwa kwa njia hii,” amesema.

Katika miaka ya karibuni, tafiti zimeonesha teknolojia hii inaweza pia kusaidia katika kudhibiti maumivu sugu, kuharakisha kupona kwa vidonda, kusaidia wagonjwa wanaopata nafuu baada ya kiharusi, pamoja na matatizo ya kimetaboliki kama kisukari.

Tofauti na njia nyingi za matibabu ya kawaida, teknolojia hii haina matumizi ya kemikali na haihusishi upasuaji.

Wagonjwa hawalazimiki kumeza dawa nyingi au kuchoma sindano, jambo linaloifanya iwe rafiki zaidi kwa watoto, wazee na wagonjwa wanaohitaji matibabu ya muda mrefu.

“Duniani kote phototherapy imeanza kutambulika zaidi kwa sababu haiingizi kemikali mpya mwilini. Badala yake, inachochea seli za mwili kufanya kazi vizuri na kujirekebisha,” ameeleza mtafiti mwandamizi wa masuala ya tiba, Dk Halima Omari.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takribani theluthi moja ya vifo vyote nchini Tanzania, huku magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kisukari, saratani na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa yakiongoza.

Dk Omari anaamini kuwa teknolojia kama phototherapy inaweza kusaidia kupunguza mzigo huo.

“Hatuwezi kuendelea kutegemea dawa na upasuaji pekee. Ni wakati wa kuanza kuunganisha teknolojia mpya katika matibabu, hasa tunapoona ongezeko la magonjwa yanayohusishwa na mtindo wa maisha,” amesema.

Dk Magesa, aliyesoma katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na kuhitimu mwaka 2015, amesema wazo la kuleta phototherapy nchini lilianza katika miaka yake ya mwanzo kazini.

“Niliendelea kuona wagonjwa wanaotegemea dawa kwa miaka mingi, hasa wale wenye maumivu sugu, madhara ya kiharusi na matatizo ya kimetaboliki,” amesema.

Baada ya kukutana na teknolojia hiyo wakati wa shughuli zake za kitaaluma nchini Uingereza, aliamua kuchunguza uwezekano wa kuitumia Tanzania.

“Niliamua kuwekeza akiba yangu mwenyewe kuleta vifaa na kuanza majaribio hapa nchini,” amefichua.

Hata hivyo, safari hiyo haikuwa rahisi

“Watu wengi walikuwa na shaka. Waliuliza inawezekanaje mtu kupona bila dawa au sindano? Lakini baada ya kuwahudumia wagonjwa wenye kiharusi, matatizo ya figo, uvimbe puani kwa watoto na maumivu ya viungo, tulianza kuona matokeo chanya,” ameeleza.

Kwa Amina Salum (58), mkazi wa Dar es Salaam aliyepata kiharusi kidogo mwaka jana, matibabu hayo yameleta mabadiliko makubwa maishani mwake.

“Nilikuwa nimepoteza nguvu upande mmoja wa mwili na hata kufanya shughuli za kawaida ilikuwa ngumu,” amesimulia.

“Baada ya vipindi kadhaa vya phototherapy nilianza kuona nafuu taratibu. Leo naweza kutembea bila msaada mkubwa. Sikuwahi kufikiria mwanga unaweza kusaidia kupona.”

Mgonjwa mwingine, Joseph Michael (42), mwalimu aliyekuwa akisumbuliwa na maumivu ya muda mrefu ya viungo, naye amesema alipata nafuu baada ya kujaribu tiba hiyo.

“Nilikuwa natumia dawa za maumivu kwa muda mrefu lakini zilikuwa zinapunguza maumivu kwa muda tu. Nilipojaribu phototherapy, baada ya wiki chache nilianza kuona tofauti,” amesema.

Ingawa tafiti zaidi za kisayansi bado zinahitajika, wataalamu wanasema ushuhuda wa wagonjwa unaanza kuongeza hamasa ya umma na kupunguza mashaka kuhusu teknolojia hiyo.

Tahadhari na matumaini ya wataalamu

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasisitiza ubunifu wa kitabibu lazima uambatane na ushahidi wa kisayansi.

“Phototherapy inaonesha matumaini, lakini ni muhimu kufanya tafiti na majaribio ya kina katika mazingira ya Tanzania,” amesema mtaalamu wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Bugando, Dk Joseph Lema.

“Wagonjwa wetu wana tofauti za kijenetiki, mitindo ya maisha na mazingira ambayo yanaweza kuathiri matokeo ya matibabu.”

Hata hivyo anaamini kuwa teknolojia, “Ikitumika kwa usahihi, inaweza kupunguza utegemezi wa dawa na madhara yanayotokana na matumizi ya muda mrefu ya dawa.”

Mustakabali wa teknolojia katika afya

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeanza kupiga hatua katika kutumia teknolojia mbalimbali kuboresha huduma za afya.

Hata hivyo, wachambuzi wa sera za afya wanasema teknolojia zinazosaidia kinga na matibabu yasiyo na madhara makubwa zinapaswa pia kupewa kipaumbele.

“Teknolojia katika sekta ya afya si anasa tena, ni hitaji muhimu,” amesema mchambuzi wa sera za afya kutoka Dar es Salaam, Flora Ndunguru.

“Kadri magonjwa yasiyoambukiza yanavyoongezeka, tunahitaji mbinu mbadala ambazo ni salama, nafuu na zinazoweza kupunguza wagonjwa wanaolazwa hospitalini mara kwa mara.”

Ameongeza kuwa ubunifu unaoanzishwa na wataalamu wa ndani una faida kubwa kwa sababu mara nyingi unalenga changamoto halisi zinazokabili jamii.

Kwa sasa, Dk Magesa ana matumaini ya kupanua huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kupitia ushirikiano na hospitali, taasisi za utafiti na serikali.

Pia, ana mpango wa kuwafundisha wataalamu wa afya matumizi ya vifaa vya phototherapy pamoja na kuongeza uelewa kwa umma kuhusu faida za tiba ya mwanga.

Lengo lake la muda mrefu ni kuona teknolojia hiyo ikiingizwa rasmi katika mfumo wa huduma za afya nchini.

“Dhamira yetu ni kuwasaidia watu kutoka katika mzunguko wa kutumia dawa maisha yote,” amesisitiza.

“Tunataka kuipa familia matumaini mapya, hasa zile ambazo zimeelemewa na gharama za matibabu, na kuonesha kuwa ubunifu unaweza kubadilisha maisha.”

Kadri Tanzania inavyoendelea kukabiliana na ongezeko la magonjwa sugu, ubunifu kama phototherapy unaweza kuwa sehemu muhimu ya safari kuelekea mfumo wa afya unaotegemea zaidi kinga, teknolojia na matibabu rafiki kwa wagonjwa.