Uhamiaji yaanza kuuwinda ubingwa ZPL

WAKATI Ligi Kuu ya Zanzibar ikisimama kwa ajili ya kupisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani huku ikitarajiwa kuendelea Machi 28, 2026, Kocha Mkuu wa Uhamiaji, Abdul Saleh amesema timu hiyo itaanza mazoezi hivi karibuni.

Alisema timu hiyo inajinoa kwa ajili ya kujiandaa na mechi 10 za mzunguko wa mwisho wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu wa 2025-2026 wakiwa na malengo ya kuwania ubingwa.

“Tunaratajia kuanza mazoezi hivi karibuni ndani ya mwezi huu kujiandaa na michezo miwili ugenini dhidi ya Junguni United na Chipukizi United,” alisema.

Katika hatua nyingine, kocha huyo alisema bado anaumizwa na mechi aliyopoteza dhidi ya KMKM kwani kikosi chake kilitawala na kutengeneza nafasi nyingi lakini kilishindwa kutamba mbele ya mabaharia hao.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Zanzibar, Uhamiaji ilipoteza kwa mabao 2-0, endapo ingeshinda, basi ingekaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

“Katika tukio gumu kulisahau ni kufungwa na KMKM msimu huu kwa sababu tulipoteza mchezo ambao hatukustahili kupoteza,” alisema.

Alisema, timu hiyo inahitaji kutwaa ubingwa wa ZPL msimu huu au kuchukua Kombe la FA na watapambana katika kufanikisha hilo.

Timu hiyo imecheza mechi 20 za Ligi Kuu Zanzibar, kati ya hizo imeshinda 11, sare tatu, imepoteza sita na kuvuna alama 36 ikiwa nafasi ya nne katika msimamo, tofauti ya pointi mbili na kinara wa ligi, Fufuni yenye 38.