Kabla ya kutangazwa kwa washindi, timu za wanafunzi zilipata mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu shiriki pamoja na wadau wa mfumo wa ubunifu.
Mafunzo hayo yalihusu uundaji wa mawazo ya biashara, kukuza biashara changa, mikakati ya kuingiza ubunifu sokoni na namna ya kujenga biashara zinazoweza kupanuka na kushindana sokoni.
Jumla ya biashara bunifu sita ziliingia fainali za mwaka huu ambazo ni Vestis, Naarad, CropIQ, Carbon Trace, Ecofy na Power Taka.
Mshindi wa jumla, Vestis, biashara iliyoanzishwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilipokea Shilingi milioni 15 kama mtaji wa awali. Jukwaa hilo la kidijitali linalenga kurahisisha ununuzi na uuzaji wa nguo mtandaoni na kuwasaidia watumiaji kuokoa muda na gharama za usafiri.
Mbali na mtaji huo wa awali, biashara hizo bunifu pia zitapata msaada endelevu ikiwemo fursa za kuwasilisha mawazo yao kwa wawekezaji, mafunzo ya masoko na uendeshaji wa biashara, ushauri elekezi pamoja na fursa za kujenga mitandao na wadau wa ubunifu na wawekezaji watarajiwa.
Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo, Meneja wa Mpango wa FUNGUO wa UNDP Tanzania, Joseph Manirakiza, alisema toleo la pili la mpango huo linaonyesha dhamira ya UNDP katika kukuza ubunifu kwa vijana nchini.
Alisema kupitia mpango huo, zaidi ya biashara bunifu 70 zinazoongozwa na wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali tayari zimenufaika.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji wa Teknolojia (COSTECH), Dkt. Erasto Mlyuka, alisema serikali inaunga mkono programu zinazochochea ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Alisema vyuo vikuu vinapaswa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa ujasiriamali ili wanapohitimu wawe tayari kuanzisha biashara zao badala ya kutegemea ajira pekee.
Akizungumza kwa niaba ya timu iliyoshinda, mwakilishi wa kampuni ya Vestis, Kelvin Erasto, alisema fedha hizo zitasaidia kupanua jukwaa la biashara hiyo na kuwafikia watumiaji wengi zaidi.
Alisema pia wanatarajia kuendelea kupata mafunzo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa vyuo vikuu ili kuimarisha mtindo wao wa biashara na kuharakisha ukuaji wake.
Mpango huo umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Vyuo Vikuu kama Injini za Ubunifu: Kujenga Njia Endelevu kutoka Maarifa mpaka Biashara.”
Katika mkutano huo wa siku tatu uliofanyika kuanzia Machi 4 hadi 6, wahadhiri wa vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa ubunifu walijadili namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kuchochea zaidi uanzishaji wa biashara bunifu, uendelezaji wa tafiti zenye tija kibiashara na ukuaji wa biashara zinazoendeshwa kwa ubunifu nchini Tanzania na Afrika Mashariki.
Kupitia ujenzi wa uwezo, ushauri elekezi na mtaji wa awali, mpango huo unalenga kuimarisha biashara bunifu zinazozaliwa vyuoni ambazo zina uwezo wa kuzalisha ajira, kutatua changamoto za maendeleo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa ubunifu nchini.








