Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku nne kwa upande wa Jamhuri katika kesi ya kughushi vibali vya kumiliki silaha inayowakabili watu tisa, wakiwemo maofisa sita wa Jeshi la Polisi.
Hatua hiyo inalenga kuipa Jamhuri muda wa kusajili na kupakia nyaraka za kesi hiyo katika mfumo wa kielektroniki ili washtakiwa waweze kusomewa hoja za awali (PH).
Uamuzi huo ulitolewa leo Jumatatu Machi 9, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Geofrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja hizo. Hakimu Mhini aliahirisha usomaji wa hoja za awali hadi Machi 13, 2026 ili kuipa Jamhuri muda wa kukamilisha usajili na upakiaji wa nyaraka kwenye mfumo wa mtandao kama sheria inavyoelekeza.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi namba PF.19931 Fredrick Malekela (45) mkazi wa Kilwa Road; E.4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54) mkazi wa Chanika; E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54) mkazi wa Kibamba; F.1126 Sajenti Robert Titus (47) mkazi wa Kisarawe; F.5092 Sajenti John Kaposwe (46) mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshi (30) mkazi wa Kisarawe.
Wengine wasiokuwa maofisa wa polisi ni Damson Mnyilenga (59) mkulima na mkazi wa Chanika; Simon Aloyce (60) mfanyabiashara mkazi wa Mwanza pamoja na Venrand Liberio (29) mfanyabiashara mkazi wa Tabata.
Hakimu Mhini alitoa uamuzi huo baada ya upande wa Jamhuri kueleza kuwa bado hawajapandisha nyaraka za kesi hiyo kwenye mfumo wa mtandao kama sheria inavyotaka.
“Upande wa Jamhuri nawapa siku nne kuanzia leo muwe mmeshapandisha nyaraka hizo kwenye mtandao, na Ijumaa kesi hii itaitwa tena mahakamani ili washtakiwa waweze kusomewa maelezo ya awali,” alisema Hakimu Mhini.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi Theresia Mtao alidai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali lakini bado hawajasajili nyaraka hizo mtandaoni.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya sheria, kabla ya washtakiwa kusomewa PH, upande wa Jamhuri unatakiwa kwanza kusajili nyaraka za kesi kwenye mfumo wa mtandao.
Wakili wa utetezi George Mwalali, anayewatetea washtakiwa sita wa kwanza, alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka. Naye wakili Nehemiah Nkoko, anayemtetea mshtakiwa wa tano, aliomba upande wa utetezi upewe nyaraka hizo mapema mara zitakapopakiwa mtandaoni ili wapate muda wa kuzipitia kabla ya kusomwa kwa hoja za awali.
Washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka katika kesi ya jinai namba 18451 ya mwaka 2025, washtakiwa wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 16 ya kughushi vibali vya kumiliki silaha kinyume na vifungu vya 333, 335A na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Inadaiwa walitenda makosa hayo kati ya Desemba 5, 2024 na Aprili 4, 2025 katika Jiji la Dar es Salaam. Wanadaiwa kutengeneza vibali vya uongo vya kumiliki silaha kwa majina ya watu mbalimbali wakiwemo Ahmed Ally, Omary Abdallah, Robert Koka, Fathi Ally, Mohamed Salim na wengine.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 28, 2025, ambapo walisomewa mashtaka hayo na wote walikana.